WANAJESHI WALIOHUKUMIWA ADHABU YA KIFO KUKATA RUFAA
Na Happiness Katabazi
IKIWA ni siku moja tu tangu Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam, iwahukumu adhabu ya kifo askari wa wiwili wa jeshi la
Kujenga Taifa na mmoja wa Jeshi la Wananchi(JWTZ) baada ya kuwatia hatiani kwa
kosa la kumuua kwa kukusudia Swetu Fundikira, wafungwa hao jana wamewasilisha
katika mahakama hiyo hati ya kusudio la kutaka rufaa kupinga hukumu hiyo.
Wafungwa hao ni MT 1900 Sajenti Roda
Robert (42), MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni na MT 75854
Koplo Ally Ngumbe (37) wa kikosi cha JWTZ Kunduchi.
Wakili wa askari wa wafungwa hao Mluge
Karoli alisema ameishawasilisha mahakamani hapo jana kwa madai kuwa wateja wake
hawakubaliani na hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Zainabu Mruke ambaye
aliwatia hatiani kwa kosa kuua kwa kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha
Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Karoli alieleza kuwa sababu zilizomsukuma
yeye na wateja wake kuwasilisha hati hiyo ya kusudio jana ni kwamba kesi yoyote ya ugomvi haiwezi kuwa
na kusudio la kutaka kuua na kwamba hakuna shahidi wa upande wa jamhuri aliyefika
mahakamani hapo na kueleza kuwa wateja wake ndiyo wamemuua Swetu Fundikira na
kuongeza kuwa washitakiwa hawakuwa na jukumu la kuthibitisha kesi hiyo na
kusisitiza kuwa waliomua Swetu siyo wateja wake.
Aidha wakili huyo alieleza kuwa
aliyepambana na wateja wake ni Swetu Fundikira na uchunguzi wa daktari
unaonyesha jina la Swetu Ramadhani Fundikira hivyo ni watu wawili tofauti na
kwamba hakuna hata shahidi mmoja alifika mahakamani na kueleza aliwai
kuuona mwili wa marehemu au kuudhulia kwenye msiba.
Askari hao kwa pamoja walidaiwa kuwa walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka
huu saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye
kufariki dunia usiku huo huo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akisoma hukumu hiyo juzi , Jaji Muruke
alisema ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndio
waliomuua Fundikira, ushahidi uliotolewa na upande wa Mashtaka (Jamhuri)
ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza kuthibitisha mashtaka
hayo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 22 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment