Header Ads

WANAJESHI WALIOMUA SWETU FUNDIKIRA WAHUKUMIWA ADHABU YA KIFO




 Na Happiness Katabazi


HATIMAYE Mahakama ya Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana imewahukumu adhabu ya kunyongwa  na kamba hadi kufa Askari wa wawili   wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) na Mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi(JWTZ), baada ya kuwakuta na hatia ya kutenda kosa la kumuua kwa kusudia marehemu Swetu Fundikira,ambaye ni  mtoto wa mdogo wa Mwanasiasa Maarufu nchini Chifu Abdallah Fundikira.

Washtakiwa waliohukumiwa adhabu hiyo ni MT 1900 Sajenti Roda Robert (42) wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha Mbweni, MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Kikosi cha Kunduchi na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni.
Washitakiwa hao walikuwa wakidaiwa  kutenda kosa la kumpiga na hatimaye kumuua kwa makusudi Fundira Januari 23, majira ya saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na Fundikira dunia usiku wa kuamkia Januari 24 mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwaajili ya matibabu kutokana na majeraha aliyokuwa amepata kutokana na kupigwa na washtakiwa hao.

Hukumu hiyo ambayo inaonekana kusaidia kukomesha baadhi ya askari wanaojichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga raia ilitolewa na Jaji Zainabu Muruke ambaye jaji huyo alisema baada ya kusikiliza kesi hiyo mwanzo hadi mwisho amefikia uamuzi wa kukubaliana na ushahidi uliotolewa na mawakili wa upande wa jamhuri ambao ulidai kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo la mauji kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Akisoma hukumu hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa na ndugu na jamaa wa marehemu na washtakiwa,  Jaji Muruke alisema kuwa ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha washtakiwa hao kuwa ndiyo kweli walimua marehemu (Fundikira), na kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri ni wa mazingira na kwamba ushahidi huo uliotolewa na upande wa jamhuri umeiwezesha mahakama ione upande wa jamhuri imeweza kuthibitisha kesi yake.

“Sheria ipo wazi na inaanisha kuwa ukiondoka au ukionekana na mtu  kwa mara ya mwisho  na baadaye mtu huyo uliyeondoka naye ikaja kubainika amepata madhara au amekutwa amekufa, wewe uliyeondoka naye  ndiyo utawajibika kisheria kutoa maelezo  kuhusu madhara yaliyompata mtu huyo;

“Na mtuhumiwa huyo akitoa maelezo  ambayo  hayajajitoshelezi kuhusu tuhuma husika basi hiyo itakuwa ni  faida kwa upande wa jamhuri ambao utegemea pia kutegemea zaidi katika kesi ya aina hiyo katika ushahidi wa mazingira, na katika kesi iliyopo mbele yangu washitakiwa wote walitoa maelezo yasiyojitosheleza na yalioacha utata:
“Japo kuwa ushahidi ulitumiwa na upande wa jamhuri katika kesi hii ni wa mazingira lakini ambao umeweza kuthibitisha kesi yao ,upande wa utetezi nao umeweza kutoa ushahidi wenye matundu mengi na unaokatika katika sana na ambao umeshindwa kuudhoofisha ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri dhidi ya washtakiwa’alisema jaji Mruke.

Aidha alisema Jamhuri limeweza kuthibitisha kosa la mauji na hivyo mahakama imewaona washtakiwa wote wana hatia ya kumuua Swetu Fundikira na kuongeza kwa kuumuliza wakili wa serikali Kongola kama ana kumbukumbu za washtakiwa kama waliwai kutenda makosa mengine ya jinai hata hivyo wakili huyo Kongola alisema jamhuri haina kumbukumbu za washitakiwa hao kama waliwahi kutenda makosa yoyote ya jinai..

Hata hivyo Jaji Muruke kabla ya kutoa adhabu hiyo  alimpatia nafasi  wakili Karoli Muluge pamoja na washtakiwa kusema lolote kabla wanalo kabla hajaanza kuwapatia adhabu hiyo.

Wakili Muluge aliiomba Mahakama iwape adhabu ambayo ni nafuu, kutokana  na mazingira ya kesi hiyo, umri wa washtakiwa kwamba bado ni vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa na kwamba familia zinawategemea.

Naye mshtakiwa wa kwanza, Sajenti Robert aliiomba Mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa ana mama yake ambaye ni mjane anayemtegemea na hakuna mtu mwingine wa kumsaidia, ana watoto wadogo na kutokana na hali ya afya yake.

Hata hivyo Jaji Muruke alilazimika kumuamuru mshtakiwa wa pili, Koplo Ngumbe kukaa chini baada kuanza kujitetea kuwa japo ametiwa hatiani lakini hakuhusika na kwamba anamwachia Mungu tu.

Kwa upande wake mshtakiwa wa tatu Koplo Rashid aliiomba mahakama imuonee huruma na impunguzie adhabu akidai kuwa yeye bado ni mdogo na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza.

Akitoa adhabu Jaji Muruke alisema kuwa ni kweli maombi ya mshtakiwa wa kwanza yanatia huruma na kwamba mshtakiwa wa tatu hata kumbukumbu zinaonesha kuwa bado ni mdogo, na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza, lakini alisema pia kuna roho iliyopotea.

“Sheria ipo wazi  kabisa mshtakiwa yoyote anayepatikana na hatia  adhabu yake ni moja tu ambayo ni kunyongwa hadi kufa na hakuna mbadala wa adhabu hiyo…hivyo mahakama  hii kwa kauli moja inatamka kuwa washitakiwa wote wa tatu mahakama hii imewahukumu washtakiwa wote watatu adhabu ya kifo hivyo mtanyongwa hadi kufa.”, alisema Jaji Muruke:

Baada ya kutoa adhabu hiyo  Jaji Muruke alitoka katika chumba cha mahakama na ghafla ndugu wa marehemu Fundikira walipaza sauti kwa kwa vilio ndani ya ukumbi  wa mahakama, kama vile walikuwa msibani.

Ndugu wawili wa marehemu, Mwasiti Fundikira ambaye ni dada wa marehemu na Shelina Hamisi (mpwa wa marehemu) walianguka chini na kuzilai kwa muda hali iliyowalazimu kuwapatia huduma ya kwanza kwa kuwapepea upepo, hadi walipoanza kurejea katika hali zao za kawaida.

Hata hivyo mwanamke mmoja aliyejitambulisha kuwa mke wa marehemu ambaye marehemu alimwacha akiwa na mimba, aliyejitambulisha kwa jina la Lucy, alisema kuwa alilia kwa sababu hakuamini kama haki ingetendeka kwani mpendwa wao aliuwawa kinyama.

Hata hivyo wakili wa washitakiwa hao , Muluge alisema kuwa hakuridhika na hukumu hiyo na kwamba atakata rufaa haraka iwezekanavyo.

Wakili Muluge alisema kuwa hakuna shahidi hata mmoja aliyewaona wakimuua na kwamba hata hayo majeraha yaliyodaiwa kuwa ndio chanzo cha kifo cha Fundikira hakuna aliyeeleza kuwa ni jinsi washtakiwa hao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 21 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.