Header Ads

KESI YA ASKOFU KAKOBE KUSIKILIZWA MWAKANI


Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imesema itaanza kusikiliza rasmi kesi ya msingi ya ubadhilifu wa fedha za kanisa la   Full  Gospel Bible Fellowship (FGBC)   inayomkabili Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Zakaria Kakobe, April 2 mwaka 2012  mwaka ujao.

Amri hiyo imetolewa na Jaji Iman Abood ambaye amepangiwa kuanza kusikiliza kesi baada ya jitihada za usuluhishi  zilizofanywa na msuluhishi Jaji Agustine Shangwa kushindwa kuzaa matunda baada ya Kakobe kukataa usulushi ,mwishoni mwa wiki  wakati wa mkutano wa makubaliano wa jinsi gani ya kuendesha kesi hiyo.

Jaji Abood alisema mahakama yake inatoa siku 14 kwa pande zote  kuwasilisha  hoja zao na mambo wanayoyabishania ambayo pia  ndiyo yatakayotolewa ushahidi katika kesi hiyo.

Katika mkutano huo wa makubaliano ya namna ya kuendesha kesi hiyo, kila upande ulitaja idadi ya mashahidi wake.

Upande wa walalamikaji katika kesi hiyo ambao unawakilishwa na Wakili Barnabas Luguwa ulieleza kuwa unakusudia kuleta jumla ya mashahidi watano mbali na walalamikaji wenyewe, na upande wa utetezi unaowakilishwa na Wakili Miriamu Majamba, ulieleza kuwa utaleta mashahidi tisa.

Kesi hiyo namba 79/2011 ilifunguliwa Mei 26, 2011 na wachungaji watatu wa kanisa hilo, Mchungaji Deuzidelius Patrick, Mchungaji Angelo Mutasingwa na Mchungaji Benedict Kaduma.

Hata hivyo baadaye Mchungaji Kaduma aliamua kujitoa katika kesi hiyo kwa madai kuwa  ameshauriwa na  ndugu na daktari, baada ya kupata ajali na kulazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa  wa kichwa.

Baadaye, msimamizi wa kanisa hilo wilayani Liwale mkoani Lindi, Mchungaji Ignas Innocent naye aliwasilisha maombi mahakamani , kujiunga katika kesi hiyo, huku akidai kuwa ameamua kupigania haki na kwamba uwa kuna mambo ambayo anataka kuyaweka wazi kuhusu askofu  Kakobe. 

Wachungaji hao wanamtuhumu Askofu Kakobe pamoja na mambo mengine kwa ubadhirifu wa mali na pesa za kanisa hilo ambazo ni zaidi ya Sh.bilioni 14 na ukikukwaji wa Katiba ya kanisa hilo.

Awali Askofu Kakobe kupitia kwa wakili wake Miriamu Majamba aliwawekea pingamizi la awali walalamikaji hao  akidai kuwa hawana haki ya kumfungulia kesi, lakini juhudi zake ziligonga mwamba baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali pingamizi lake hilo.

Kakobe, katika pingamizi lake hilo pamoja na alidai kuwa walalamikaji hawana haki ya kisheria kumfungulia kesi  kwamba si wachungaji wa kanisa hilo, kwani walishafukuzwa tangu mwaka 2010, na kwamba hati  ya madai haikuwa na sababu za madai .

Hata hivyo  mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote, zilizowasilisha kwa njia ya maandishi, katika uamuzi wake Juni 16, 2012,Jaji Shangwa  ilitupilia mbali pingamizi la Kakobe na kuwapa ushindi walalamikaji, akisema kuwa wana haki ya kumfugulia Kakobe kesi hiyo.

Katika uamuzi huo, Jaji  Shangwa alisema kuwa kwa mtizamo wake, bila kujali kwamba walalamikaji  walifukuzwa ushirika wa FGBC au uchungaji, kwa vile mioyo yao bado inapendelea huduma, mafanikio na maendeleo ya kanisa hilo, wana haki ya kisheria kufungua kesi.

Pia alisema kuwa kwa mujibu wa hati ya madai ya walalamikaji kuna  madai ambayo  walalamikaji watapaswa kuyathibitisha, ambayo ni pamoja na ubadhirifu na Kakobe kuwafungisha watu ndoa bila kuwapa vyeti vya ndoa.

Kufuatia uamuzi huo, Jaji Shangwa aliwaagiza wadaawa (wadau) katika kesi hiyo kuwatafuta maaskofu wengine kutoka madhebu tofautitofauti ili kutoa ushauri kwa mambo mengine ya kidini, wakati wa  usuluhishi.

Hata hivvyo licha ya maaskofu hao kufika mahakamani siku ya usuluhishi, Kakobe alikataa usuluhishi huo, hatua ambayo ilimlazimu Jaji Shangwa kurejesha jalada la kesi hiyo kwa Jaji Mfawidhi lipangiwe jaji wa kusikiliza ushahidi katika madai ya msingi.

Katika hati ya madai yao, walalamikaji hao wanamtuhumu Kakobe kuwa amekuwa akikusanya pesa nyingi kutoka kwa waumini wake kwa madai ya kufanyia shughuli na miradi mbalimbali ya kanisa na kuzitumia kinyume cha malengo.

Mbali na kuzitumia pesa hizo isivyo kama vile kugharimia kampeni za kisiasa kinyume cha katiba ya kanisa hilo, pia wanadai kuwa Kakobe amekuwa hatoi taarifa ya mapato ya pesa anazozikusanya wala matumizi yake.

Kuhusu ukiukwaji wa Katiba ya kanisa hilo, walalamikaji hao wanadai kuwa katiba inataka kuitishwa kwa mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano ambao ndio chombo cha juu cha maamuzi lakini Kakobe hajawahi kuitisha mkutano huo tangu mwaka 1989.

Pia wanadai kuwa katiba hiyo inaelekeza kuwa kanisa liwe na Katibu Mkuu na Mweka Hazina ambao ndio watakaolinda mali za kanisa lakini Kakobe ndio amekuwa akifanya maamuzi na shughuli zote yeye mwenyewe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Novemba 26 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.