ESTER WASIRA:MWANSHERIA ALIYEJIUNGA CHADEMA KUONGEZA NGUVU YA MABADILIKO
HIVI Karibu Mwanasheria mchanga kwenye
tasnia ya Sheria nchini, Esther Wasira alijitumbukiza kwenye ulingo wa siasa na
alianza kwa kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).Mwandishi
wa Makala hii alilazimika kumtafuta Ester na kufanya nae mahojiano kwa kina ili
watu waweze kufahamu historia ya maisha yake na nini kilimsukuma kuingia kwenye
ulingo wa siasa,fuatana na mwandishi wa makala hii kwa simulizi zaidi.
Swali:Kwanini umeamua kujiingiza kwenye ulingo
wa siasa wakati wewe ni mwanasheria?
Jibu: Siasa ni kitu kisichoepukika. Kila
kinachonizunguka ni siasa. Haki na wajibu wa kila mtu kwenye jamii unategemea
na siasa ya nchi yake. Sasa kuliko kukaa pembeni, kunyamaza kimya na kuangalia
jinsi siasa zinavyoendeshwa na kuathiri maisha yangu na ya watanzania wenzangu
nimeona ni bora zaidi kuongea panapo fursa ili kuwaamsha na wenzangu kutoka
kwenye usingizi mzito wa kutokufikiri. Nadhani kama nilivyosema kwenye hotuba
yangu siku ya Kongamano la kumuenzi mwalimu Nyerere, Elimu tunayoipata
haitakiwi itengeneze “Robots” bali watu watakaoiuliza maswali serikali yao ili
iwajibike.
Kuwa
mwanasheria, kwangu nakuona kama ni Nyongeza “added advantage” kwasababu
kunanifanya niwe muangalifu zaidi katika kunena, kutenda na kutetea maslahi ya
watu kwa ujumla bila kuvunja sheria za nchi au kukiuka maadili yaliyowekwa
kwasababu najua uhuru wangu unapoanzia na mipaka yake,na haki na wajibu wangu.
Swali:Kwanini usingejiimarisha kwanza kwenye
fani yako ya sheria ndipo kwanza ukajiingiza kwenye siasa?
Jibu: Siasa kwa mtazamo wangu sio mtaji wala
sio hobby!! Kwangu ni jambo la msingi sana ambalo litaamua hatma ya maisha ya
watu kwenye ardhi yao. Katika vitu ambavyo sio vya kuhairisha ni utetezi wa
maisha ya mwanadamu na maslahi yake kwa ujumla. Na kwa hali ya nchi ya Tanzania
ilipofikia, kwangu ni kama “State of Emergency”. Kila mwenye “silaha” aingie
vitani. Umahiri wa sheria hautanifaa kitu kama sitashiriki mapema harakati za
kuleta mabadiliko kwenye nchi yangu na kumkomboa mtanzania wa hali ya chini
ambaye dira ya maisha yake imefutika na kesho yake ni kama ndoto. Sihitaji
Shahada ya pili ya Sheria kujua kuwa viongozi wengi wa kizazi cha sasa
wamepotoka na wanahatarisha maisha yetu na nchi yetu kwa ujumla. Wakati
uliokubalika ni sasa.
Swali:Kwanini umeamua kujinga na chama cha Chadema?
Jibu: Jibu liko wazi. Mpaka sasa Chadema ndiyo chama pekee
kinachoonesha dhamira safi ya kuiongoza Tanzania na kuleta matumaini ya kujenga
Tanzania mpya yenye Neema. Itikadi zake na falsafa zake na nia ya dhati ya
kiutendaji kwa viongozi mbalimbali wa chama hiki ni sehemu ya mambo
yaliyopelekea mimi kukichagua Chadema. Lakini nilishawahi kusema na nitarudia
haya, Chadema ni chama cha watu makini sana, kuanzia vijana mpaka akina mama;
ni fahari kubwa sana kujiunga na Chadema na tena ni Ushahidi wa mtu kujitambua
na kuondokana na ushabiki wa kihistoria usio na tija wala manufaa kwenye nchi
yetu wa kung’ang’ana na dhamira ya “chama kikongwe”. Ogopa sana mtu
anayeshindana na mabadiliko mahali ambapo hayana budi kuja.
Swali:Utawezaje kufanya kazi ya uanasheria wakati huo huo ni
mwanasiasa?
Jibu: Sheria hainizuii kufanya shughuli za kisiasa, lakini pia
ratiba yangu itabadilika kufuatana na majukumu husika. Changamoto hazina budi
kuja lakini ndiyo mwanzo wa kukua na kupanuka fikra na kiutendaji zaidi.
Swali:Una mahusiano gani na mzee wasira?
Jibu: Mzee Wasira yupi? Wapo Wazee Wasira Wengi
(hahaha). Ila utashi unaniongoza kuwa ni Mzee Stephen Wasira (MP) (Waziri wa
Nchi Ofisi ya Raisi Mawasiliano na Uratibu); huyo ni baba yangu mdogo
aliyenyang’anyanywa ziwa na baba yangu mzazi, Wakili George Wasira, ambaye pia
ni mmoja kati ya waasisi wa Chadema.
Swali:Una ujumbe gani kwa watoto wa kike hapa
nchini?
Jibu: Watoto wa kike nina mengi ya kuwaeleza,
ila kwa leo nitasema hivi: Katika dunia ambayo nguvu ya misuli haitumiki sana
na badala yake nguvu ya akili ndiyo inatakiwa zaidi, basi nafasi ya mwanamke
kwenye jamii ni kubwa sana. Angalia jinsi Michelle Obama wa Marekani kuanzia
mwanzo wa safari ya Barack Obama ya kisiasa anavyochukua nafasi kubwa kumsaidia
mumewe kwenye campaigns mpaka Obama anakiri kuwa mke wake amekuwa msaada mkubwa
sana.
Wanawake tuna
nafasi kubwa sana ya kuleta mabadiliko ya kweli kwenye nchi yetu kama tukiacha
uoga na tabia ya kupenda kusubiria chini ya ngazi ili tupewe vitu kwenye
visahani vya dhahabu. Mwenye fursa ya kusema amuongelee aliyekosa jukwaa la
kujielezea; tusijipende wenyewe kwasababu tumefanikiwa kuwa na “Vitz” na kuvaa
dhahabu. Inasikitisha mwanamke anapokosa huruma na kuamua kujiingiza kwenye
tafrani za rushwa!! Pia wale wamama wanaopewa kanga na Madera na shilingi elfu
kumi kumi ili kuingiza madarakani utawala mbovu, jaribuni kufikiria mbali na
muone ni mazingira gani mnawaachia watoto wa watoto wenu. Aibu gani hii?? We
are the mothers of this nation!! Hiyo siyo tabia ya mama! Wote tunaweza
kulikomboa Taifa letu kama tukiamua kwa dhati kusimama pamoja.
Swali:Tueleze mtazamo wako kuhusu mwenendo wa
siasa hapa nchini?
Jibu: Kwa ujumla, siasa ya sasa inaendeshwa kwa
mabavu, ubabe, hisia, hofu, hujuma, rushwa, mapambano, udini, ukabila, mipasuko
na huku sauti ya mabadiliko ikisikika kwa mbali. Aliyeshika mpini anatumia kila
mbinu anayoweza ili kuendelea kulima, na aliyedhani ameshika makali
yangemsaidia anajikuta kafungwa mikono. Ndio maana siasa wanaiita mchezo
mchafu. Huwezi kumuondoa jabali kwenye milki yake bila kupambana nae, jabali
ana dola, jabali ana fedha, jabali ana sauti, lakini mwisho wa siku, jiwe moja
tu litamuangusha Shujaa, maana lina “Sauti ya Watu” nyuma yake.
Swali:Ni kitu gani ambacho kiliwahi kukufurahisha au
kukusikitisha katika maisha yako?
Jibu: Kutekwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dr. Steven Ulimboka na
kisha kutelekezwa katika msitu wa Mwabwepande; pamoja na utata uliojitokeza
kuhusu suala hilo, na namna uchunguzi ulivyoendeshwa na hatua zilivyoshindwa
kuchukuliwa dhidi ya wale “wote” waliodaiwa kuhusika. Inaleta mashaka sana juu
ya hali ya Usalama wa nchi yetu na usalama wa watetea haki na usawa.
Swali:Nini matarajio yako ya baadaye katika medani ya siasa na
sheria?
Jibu: Matarajio yangu kisheria ni kujiendeleza zaidi kwasababu
ndio career yangu na kutafuta maarifa zaidi kulingana na malengo yangu
niliyojiwekea.
Lakini pia, kisiasa, kikubwa ni kutumia
fursa mbali mbali ili kutimiza azma ya kuiona Tanzania mpya inakuja na
mabadiliko yanakuwa halisi na sio dhana tena. Kwa sasa, ni kushawishi
watanzania kwamba Chadema imekomaa na iko tayari kushika dola na kufanya sauti
ya mtanzania wa kawaida isikike tena. Hapo baadae, nitaendelea na kazi ya
ujenzi wa chama na kufanya yale majukumu ambayo viongozi watanipangia kufanya;
ikiwemo kushauri, kujitolea, kuelimisha, na kuhamasisha watanzania kuhusu mambo
mbalimbali yahusuyo chama na taifa kwa ujumla.
Nataka nitoe
ufafanuzi kuwa, Vijana ni chachu ya mabadiliko na ndio maana mifano yote
aliyoitoa yeye alionesha kuwa kila “Revolutionary Attempts” yaani hatua
za kimapinduzi zilifanywa na vijana na baadae wazee ndio waliongoza nchi, yaani
watu wa makamo.
Kilio chetu ni kwamba,vijana ni lazima
waamke kwani wao ni nguvu kazi ya taifa lolote; wao wakilala basi na harakati
zote zitalala. Wazee wanaweza kubaki kuwa ngazi shauri lakini watendaji siku
zote ni vijana.
Lakini pia, kwenye ajira, vijana wapewe
nafasi za kazi pale ambapo wanastahili na hii itafanikiwa pale
watakaporekebisha sera za uajiri zenye kutaka uzoefu wa miaka 6 au 10 maana
hiyo inawapa tabu vijana wengi waliosoma kupata kazi.
Swali: Naomba kufahamu historia ya maisha yako?
Jibu: Nilizaliwa 1987 hapa hapa Dar es Salaam;
nikasoma shule ya Msingi Muhimbili (1992-1998). Elimu ya Sekondari (O-level)
pale Loyola High School (1999-2003) na (A-level) pale Shaaban Robert Secondary
School (2004-2006). Kisha nikaingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya
Sheria (Zamani Kitivo cha Sheria) (2006-2010.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili,
Novemba 18 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment