KESI YA PONDA YAIVA
*Masharti ya dhamana yatajwa
*Ulinzi mkali watanda Kisutu
*Hukumu ya Maranda yayeyuka
tena
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi
Kisutu Dar es Salaam, ndani na nje ya mahakama hiyo jana ilitawaliwa na ulinzi
mkali toka vyombo vya ulinzi na usalama
kwa ajili ya kuakikisha usalama unakuwepo katika eneo hilo wakati kesi ya uchochezi
na wizi wa mali za sh milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda Issa na wenzake 49 ilipokuja kwaajili ya
kutajwa.
Washitakiwa hao walifikishwa
jana saa moja asubuhi mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa Askari wa Jeshi
la Magereza waliokuwa wamebeba silaha nzito na kiunoni wakiwa wamebeba mabomu
ya machozi na wengine wakiwa wamevalia vifaa maalumu mwilini kwaajili ya
kujikinga na silaha (Riot Wear) wakati askari wa jeshi la Polisi wakiwa nao
wamebeba silaha nzito na wengine wakiwa na Mbwa zaidi ya saba ambao walikuwa
kwaajili ya kunusa mabomu na polisi wengine walikuwa wamepanda farasi wawili wakizungunga ndani na nje mahakama
hiyo huku askari wanaodhaniwa kuwa ni wa Idara ya Usalama wa Taifa(TISS), wao
wakiwa wameweka hema katika mlango wa kuingilia geti la mahakama hiyo pamoja na
kufunga vifaa maalum kwaajili ya kuwakagua watu waliokuwa wakitaka kuingia
ndani ya mahakama hiyo pamoja na ukuta wa mbele ya mahakama hiyo ulikuwa
umefungwa kamera ya CCTV.
Tanzania Daima liliwashuhudua washitakiwa wakiingizwa ndani ya viwanja vya mahakama hiyo
saa moja asubuhi huku wakiwa wamebebwa kwenye magari ya jeshi la Magereza
matatu yakiwa namba za usajili STK 4480, STK 916 na STK 9160 aina ya Ashoko
Layland ambayo yalitanguliwa na Defenda mbili za Polisi zenye namba za
usajili PT 2066,STK 4480 ,PT 1523,PT
2093 na gari lilobeba maji ya kuwasha ‘Kikojozi’ na magari mengine mengi ya
wanausalama ambao walikuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi
Ilala, Duani Nyanda na maofisa maofisa wengine toka Jeshi la Magereza na Usalama wa Taifa.
Washitakiwa hao saa waliingizwa moja kwa moja nyumba ya mahakama
hiyo na kisha kupandishwa katika
mahakama ya wazi mbele ya Hakimu Mkazi
Victoria Nongwa saa 2:05 asubuhi ambapo wakili Mwandamizi wa Serikali
Tumaini Kweka alianza kwa kuimbukusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja
kwaajili ya kutajwa na akadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hakimu Nongwa alisema
kwa mujibu wa mashitaka yote yanayomkabili Sheikh Ponda na wenzake 49
yana dhamana kwa mujibu wa sheria isipokuwa mahakama hiyo bado inaendelea
kufungwa mkono na hati ya kuzuia dhamana ya Ponda peke yake iliyowasilishwa
mahakamani hapo Oktoba 18 mwaka huu, na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),
Dk.Eliezer Feleshi chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa
ya Jinai ya mwaka 2002, ambacho kina mpa madaraka DPP kuwawasilisha hati hiyo
ya kufunga dhamana ya mshitakiwa yoyote wa makosa ya jinai hata kama mashtaka dhidi ya mshitakiwa huyo
yana dhamana na DPP anapoiwasilisha hati
hiyo mahakama inakuwa imefungwa mkono hadi pale DPP atakapojisikia kuiondoa
hati hiyo.
“Kwa sababu hadi leo
hii(jana) DPP bado hajaiondoa hati hiyo mahakamani hapa, mahakama hii haitaweza
kutoa masharti ya dhamana kwa Sheikh Ponda na hivyo basi leo haitazungumzia dhamana ya
Ponda na badala yake inatoa masharti ya dhamana kwa kuanzia kwa mshitakiwa wa
pili hadi 50 kama ifuatavyo”alisema Hakimu Nongwa.
Hakimu Nongwa alisema
kila mshitakiwa atatakiwa awe na
wadhamini wawili wa kuaminika na atasaini bondi ya shilingi Milioni moja na
wadhamini hao wawe na vitambulisho toka ofisi zinazotambulika na kwa anaiarisha
kesi hiyo hadi Novemba 15 mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya upande wa Jamhuri
kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao.
Baada ya hakimu huyo
kuairisha kesi hiyo saa 2:01 asubuhi maofisa usalama waliwaondoa ndani ya
ukumbi wa mahakama washitakiwa hao na kisha kuwapeleka nyuma ya mahakama hiyo
na kisha kuwaongoza kupanda mabasi ya jeshi la Magereza matatu huku washitakiwa
hao wakionekana kuwa na nyuso za upole tofauti na mara ya kwanza washitakiwa
hao walivyofikishwa mahakamani hapo na
kuondoshwa kupelekwa gerezani Oktoba 18
mwaka huu, walikuwa wakiimba na kupaza sauti ndani ya magari hayo kuwa ‘Taqbir
alhuqabal’.
Wakati muda huo ikiendelea
mahakamani na kuarishwa wanausalama zaidi ya 50 walikuwa wametanda ndani ya
viunga na nje ya jengo la mahakama hiyo huku wakiwa wamebeba bastora
viunoni,wengine mabomu ya machozi wameyafunga kiunoni,na wengine wamevalia
vifaa vya kujikinga na silaha (Riot Wear) na wengine wakiwa wameshikilia mbwa
wa kunusa mabomu na farasi wakiwa wakilinda usalama na kisha ilipofisa saa 2:46
asubuhi msafara wa uliokuwa umewabeba wa washitakiwa hao uliondoka mahakamani
hapo chini ya ulinzi mkali kwaajili ya kuwarudisha katika gereza la Segerea ,Ponda na wenzake
wote ambao wadhamini wao hawakuwa wamewahi kuja kuwadhamini.
Aidha msafara huo ulipoondoka
ndipo ndugu na jamaa wa washitakiwa na wananchi wengine waliokuwa wanataka kuja
mahakamani hapo kwaajili kusikiliza kesi zao na kuwadhamini washitakiwa
walianza kuwasili lakini hata hivyo walikuwa wakitakiwa na wana usalama geti
kueleza wanataka kwenda mahakama hapo kufanya nini na magari yalizuiwa kwa muda
kuingia ndani ya mahakama hiyo hadi pale washitakiwa hao walipoondoshwa
mahakamani.
Hata hivyo Tanzania Daima
liliwashuhudia ndugu na jamaa wa shitakiwa hao kuanzia saa tatu asubuhi
wakiwasili na wakakutana na wanausalama geti waliowataka wawaonyeshe hizo barua
za dhamana wanazotaka kuwazamani washitakiwa na wengine walikuwa hawana barua
hizo hivyo wana usalama waliwazuia wale
wote waliodai kuwa wamekuja kuwadhamini wakati hawana barua wasiingie ndani ya
geti hilo na walitii amri hiyo bila shuruti.
Lakini hata hivyo wanausalama
hao ambao walianza kutanda ndani na nje ya mahakama hiyo tangu saa 12 asubuhi
walizuia watu wasipite wala kukaribia eneo la uzuio wa mahakama hiyo kwasababu
za kiusalama hali iliyosababisha baadaye kuibuka kwa kikundi cha watu
waliojitambulisha kuwa wao ni waumini wa dini ya Kiislamu karibu na uzio wa
mahakama na kuanza kupaza sauti kuwa “Serikali inaonea waislamu, waislamu
wanagandamizwa, mahakama ni ya wakristo, hakuna haki’.
Hata hivyo askari wa kikosi
cha FFU na wale waliokuwa wamepanda Farasi walienda kukitanya kikundi hicho
kilichokuwa kikipaza sauti nje ya uzio wa mahakama karibu na Jengo la Maktaba
Kuu ya Taifa ambao walitawanyishwa kwa
Farasi wawili na kukimbia hadi Chuo cha Biashara(CBE). Pamoja na hali hiyo
shughuli za kimahakama ziliendelea kama kawaida kwani hazikuathirika na kesi na
hali hiyo ya usalama.
Baadhi ya watu waandishi wa
habari,wanasheria na wananchi wa kawaida waliipongeza serikali kwa hatua yake
ya kuimarisha ulinzi wa hali ya juu katika mahakamani hapo wakati kesi hiyo ya
Ponda na wenzake ilipokuja kwaajili ya kutajwa na kupendekeza ulinzi huo uwe ni
endelevu katika kesi hiyo na kwamba wanaviomba vyombo vya dola vikabiliane na
wale wote watakaoandamana leo.
Awali Oktoba 18 mwaka huu,
Wakili Mwandamizi wa Serikali Kweka alidai washitakiwa 49 wanakabiliwa na
makosa manne na Ponda ana kabiliwa na makosa matano. Makosa hayo ni kula njama
kutenda kosa ,kuingia kwa nguvu kwa nia ya kutenda kosa kuwa Oktoba 12 mwaka
huu huko Chang’ombe Markasi, wasipokuwa na sababu za msingi waliingia kwa jinai
kwenye kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya
Agritanza, kujimilikisha kiwanja
hicho kwa njia ya iloyopelekea uvunjifu wa amani,wizi ambapo
baada ya kufamia waliiba vifaa na malighafi ikiwemo nondo, kokoto zenye jumla ya thamani
ya Sh. 59,650,000 mali ya kampuni ya
Agritanza na kosa la tano ni la uchochezi ambalo linamkabili Sheikh Ponda peke
yake ambapo anadaiwa kutenda kosa
hilo Oktoba 12 mwaka huu ,katika eneo
hilo ambapo aliwaamasisha washitakiwa hao watende kosa hilo.
Wakati huo huo ,Mahakama hiyo imeairisha kutoa hukumu ya kesi ya wizi
wa Shilingi milioni 207 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya
Tanzania, inayomkabili Kada wa Chama cha Mapinduzi, Rajab Maranda,Faijala
Hussein, Ajay Somayi na maofisa wa BoT, Iman Mwakosya,Ester Komu,Sophia Lalika
kwasababu idadi ya jopo mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo halijakamilika.
Jaji Beatrice Mutungi alisema
kama inavyoeleweka kesi hiyo imekuwa ikisikilizwa kwa mtindo wa jopo la
mahakimu wa tatu yaani yeye Jaji Mutungi, Jaji Samuel Karua na Hakimu Mfawidhi
wa mahakama hiyo Ilvin Mugeta lakini Jaji Karua ambaye kituo chake cha kazi
kipo mkoani Mbeya walimtarajia afike jana Dar es Salaam, ameshindwa kufika
kwaajili amebanwa na shughuli za kikazi hivyo wanaiarisha hadi Novemba 22 mwaka
huu.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 2 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment