KORTI KWA KUSHAWISHI NA KUKOJOLEA Q'URAN
Na Happiness Katabazi
WAKAZI watatu wa eneo la Gongolamboto
jijini Dar es Salaam,jana walijikuta wakifikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu chini ya ulinizi mkali kwa makosa ya kudhalilisha kitabu cha dini
ya Kiislamu na kushawishi kutendeka kwa kosa hilo.
Wakili Mwandamizi wa Serikali
Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Bingi Mashabara aliwataja washitakiwa hao
kuwa ni David Kapaya(20) ambaye ni muumini wa dini ya Kikristo, Mussa Sule(26)
mbaye ni muuzaji wa Vocha za Kampuni ya Tigo na Haruna Mateno(17) ambao walikuwa hawana wakili wa kuwatetea.
Wakili Kweka alilitaja
shitaka la kwanza linamkabili mshitakiwa wa kwanza peke yake (David), ambalo ni
la kudhalilisha dini ya Kiislamu ambalo ni kinyume na kifungu cha 125 ambacho
kinasomwa pamoja na kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002
,kuwa Oktoba 20 mwaka huu, huko eneo la
Mogo, Mikongoro alidhalilisha dini ya Kiislamu
kwa kukikojolea kitabu cha dini
ya Kiislamu(Korani).
Alidai shitaka la pili
kwaajili ya mshitakiwa wa pili na watatu (Sule na Haruna) peke yao kuwa
wanakabiliwa na kosa la kumshawishi kutendeka kwa kosa la kudhalilisha dini ya
kiislamu.Kuwa mnamo Oktoba 20 mwaka huu, huko eneo la Mogo, Mikogore wakiwa na ufahamu washitakiwa hao
walimshawishi mshitakiwa wa kwanza(David) akojolee kitabu hicho cha dini ya Kiislamu huku
wakijua kufanya hivyo ni kosa na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika.
Hata hivyo washitakiwa
walikana mashitaka hayo.Na Hakimu Mashabara bila ya kutaja masharti ya dhamana
aliamuru washitakiwa wapelekwe mahabusu hadi Novemba 15 mwaka huu, kesi hiyo
itakapokuja kwaajili ya kutajwa.
Hii ni mara ya pili kwa
waumini wa dini ya Kikristo kufikishwa katika mahakama hiyo na kushitakiwa kwa
kosa la kudhalilisha kitabu cha dini ya Kiislamu.Mara ya kwanza ilikuwa ni
Oktoba 18 mwaka huu, ambapo mtoto mmoja mwenye umri wa chini ya miaka 18
alifikishwa katika Mahakama ya Watoto akikabiliwa na kosa la kudhalilisha dini ya
Kiislamu kwasababu alikikojolea katika Maeneo ya Mbagala mwezi uliopita.
Itakumbukwa ghasia kubwa na
mapambano baina ya baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu na jeshi la polisi
yalizuka jijini Dar es Salaam Oktoba 12 mwaka huu, na kusababisha makanisa manne
kuchomwa moto,uvunjifu wa amani kutoweka na mwishowe washitakiwa zaidi 70
wamefunguliwa kesi za unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi katika mahakama hiyo
ya Kisutu na kesi hizo zinaendelea
mahakamani hapo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Novemba 3 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment