Header Ads

PROFESSA LIPUMBA NI MBUMBUMBU WA SHERIA,ACHA SHERIA ICHUKUE MKONDO WAKE
NA HAPPINESS KATABAZI
KWA mara ya pili sasa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Professa Ibrahim Lipumba  amekuwa akiitisha mikutano na waandishi wa habari kuzungumzia vurugu za kidini zilizotokea hapa nchini hususani jijini Dar es Salaam.

Profesa Lipumba pamoja na mambo mengine amekuwa akisema tena kwa ujasiri kuwa kesi ya jinai namba 245/2012 inayomkabili Sheikh Issa Ponda na wenzake 49 iliyofunguliwa na upande wa jamhuri Oktoba 18 mwaka huu, ambayo ipo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Victoria Nongwa na inendwa na wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka wakati upande wa utetezi unatetewa na wakili wa kujitegemea Mansoor Nassor ilipaswa iwe ya madai na siyo jinai na kwamba eti Ponda alistahili dhamana na kuwa anafanya mpango wa kukutana na Rais Jakaya Kikwete amshauri serikali ifanye mazungumzo na Maimamu wa misikiti ili waweze kupata suluhu ya tatizo la vurugu hizo za kidini.

Binafsi ni mwandishi wa habari za mahakamani hapa nchini na kesi hii ni miongoni mwa kesi ambazo minaziudhulia siku ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza ,na hata  Novemba Mosi mwaka huu,kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajwa na wakili wa serikali Kweka aliieleza mahakama kuwa uplelezi wa shauri hilo umekamilika nilikuwepo tangu saa moja asubuhi mahakamani hapo, na  hata hiyo  Novemba 15 mwaka huu, panapo majaliwa ya mwenyezi mungu kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya upane wa jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa nitakuwepo ndani ya ukumbi namba moja wa mahakama hiyo kwaajili ya kuiripoti kesi hiyo kwa uweledi wa aina yake.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ya kesi hiyo inayomkabili Ponda na wenzake ambayo nakala yake ninayo, ina jumla ya mshitaka matano ambapo mashitaka yote matano yanamkabili Ponda na mashitaka manne yanamkabili mshitakiwa 2-50.

Kosa la kwanza  ni la kula njama kutenda kosa kinyume na kifungu cha  384 cha Sheri ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, ambapo washitakiwa wote wanaidaiwa kuwa Oktoba 12 mwaka huu katika eneo la Chang’ombe  Marksi walikula njama kwania ya kutenda kosa.Kosa la pili ni  kuingia kwa nguvu  kwa nia ya kutenda kosa  kinyume na kifungu  cha 85,35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ,kuwa Oktoba 12 mwaka huu,  katika eneo la Chang’ombe Markasi ,kwa jinai na wasipokuwa na sababu  waliingia kwenye kiwanja cha eneo hilo kinachomilikiwa na Kiwanda cha Agritanza.
Wakati kosa la tatu ni  la kujimilikisha kwa jinai kiwanja hicho kinyume na kifungu cha 86 na 35 cha Sheria hiyo  kuwa kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu, katika eneo hilo pasipo na uhalali washitakiwa wote  katika hali ya kupelekea uvunjifu wa amani,walijimilikisha  kwa nguvu ardhi ya kampuni ya Agritanza.

Shitaka la nne ni la wizi kinyume na kifungu cha 258 na 225 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu  ya mwaka 2002  kuwa washitakiwa wote kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu, waliiba vifaa,malighafi  kama nondo,matofali ,kokoto zenye jumla ya Sh 59,650,000 mali ya Kampuni hiyo.

Aidha shitaka la tano ni kwaajili ya Ponda peke yake ambalo ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni  ya Adhabu  ya mwaka 2002 kuwa Oktoba 12 katika eneo hilo la Chang’ombe  kwa maelezo kuwa yeye ni Katibu  aliwashawishi wafuasi wake ambao ni washitakiwa hao watende makosa hayo.Na washitakiwa wote walikanusha mashitaka hayo na Hakimu Nongwa akasema mashitaka yote yanadhamana kwa mujibu wa sheria na akatoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa 2-50 .

Na kusema ili wapate dhamana nilazima kila mmoja awe na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini bondi ya milioni moja, licha Hakimu Nongwa alisema mahakama yake haiwezi kutoa dhamana kwa Ponda licha anastahili dhamana kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi aliwasilisha mahakamani hapo hati ya kufunga dhamana ya Ponda kwa mujibu wa kifungu cha 148(4) cha Sheria Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.Na hati hiyo ya DPP inakuwa imeifunga mikono mahakama hadi hapo siku DPP atakapoona haja ya kuiondoa hati hiyo hivyo Ponda ataendelea kusota rumande hadi hati hiyo itakapoondolewa na DPP .
Kauli ya Profesa Lipumba kuhusu kesi ya Ponda imenifanya nianze kuamini kuwa hata ukiwa msomi wa hali ya juu kama Profesa Lipumba unaweza pia kutoa maoni ya kipuuzi ambayo hayapaswi kutolewa na msomi wa aina yake mbele ya umma.

Tumuulize huyu Lipumba kabla ya kutoa kauli hizo aliwasiliana na wanasheria wa chama chake wakampa ushauri wa kisheria wa nini cha kuzungumza mbele ya umma kuhusu kesi ya Ponda inayooendelea pale katika Mahakama ya Kisutu?Naamini hakupata ushauri  mzuri toka kwa wanasheria wa chama chake au kama alipata basi wanasheria huo waliamua kumpatia ushauri ambao umemdhalilisha Lipumba mbele ya jamii ya wasomi wa sheria na jamii inayoheshimu utawala wa sheria hapa nchini.

Profesa Lipumba kwanza kabla ya kutoa kauli hizo kuhusu kesi ya Sheikh Ponda kuwa kesi hiyo ya jinai namba 245 /2010 eti ilipaswa iwe ya jinai, ungeitafuta hati hati ya mashitaka ungeisoma vizuri na ungeweza kuelewa makosa wanayoshtakiwa nayo ni ya madai au jinai  halafu ungeenda kuisoma Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code;2002),Sheria ya Mashauri ya Madai(Civil Procedure Code:2002) na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act, RE:2002) na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naamini vingekupa mwongozo mzuri sana kwa kufahamu mashitaka yanayowakabili, kifungu gani kimetumika kufunga dhamana ya Ponda na ni kwanini dhamana yake imefungwa na pia ungeweza kufahamu vyema majukumu ya mahakama ni ya pili nay a serikali ni yapi.

Na hapo ndipo ninapokubaliana na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa mwishoni mwa wiki  ambayo inawataka wanasiasa waache unafki kwani wao wanaisasa wanaishi maisha kifahali na uhuru wakati wale wafuasi wao wanaishi maisha ya tabu na wamekuwa wakiwapandikisha uongo wafuasi wao.
Sasa kwa kauli hiyo ya Kikwete minaona katika matamko hayo ya Lipumba inamgusa pia, kwani uenda Lipumba anataka kujipatia umaarufu chee wa kisiasa kupitia kesi ya Ponda ila hafahamu kuwa mahakama haiendeshwi wala haisikilizi kauliza wanasiasa  pindi inapofanyakazi zake kwa mujibu wa sheria.

Wewe Lipumba kwakuwa unasema kesi ya jinai ya Ponda ilipaswa iwe ni ya madai, hivi ni kwanini unashindwa kuomba kazi ya kuwatetea washitakiwa hao kama (Bush Lawyer )mahakamani hapo na siku kesi ikianza kusikilizwa ukawasilisha hilo pingamizi lako lakutaka kesi hiyo ya jinai ifutwe kwani imefunguliwa kimakosa ilitakiwa washitakiwa hao wafunguliwe kesi ya madai).
Maana unapozungumzia kesi hiyo kwenye majukwaa na mbele ya waandishi wa habari haimsaidii Ponda kwa lolote zaidi zaidi unazidi kumgandamiza Ponda bila wewe kujua?

Profesa mzima tena wa uchumi unayeheshimika nchi mbalimbali unashindwa kufahamu mtu anayetuhumiwa kwa kosa la wizi au kuingia kwa nguvu kwenye kiwanja au chochezi basi mtu huyo makosa hayo yataangukia kwenye jamii ya makosa ya jinai? Lakini wewe sijui kwa upotoshaji au unalako jambo unadiriki kujitokeza adharani kuuposha umma kwa kusema walipaswa washitakiwe kwa kesi ya madai?

Mwenyekiti mzima wa chama kikubwa kama CUF,ambacho chama hicho chini ya uongozi wako ni miongoni mwa chama kilichokuwa kidai Tanzania iandike Katiba mpya kwa madai kuwa Katiba ya sasa imepitwa na wakati,na kwa maana hiyo unaifahamu vyema ibara za Katiba hiyo , unashindwa kuifahamu Katiba ya nchi ambayo Ibara ya 59B(1)  inayosomeka hivi; “Kutakuwa na Mkurugenzi wa Mashtaka  ambaye atateuliwa  na Rais,kutoka miongoni  mwa watu wenye  sifa zilizoanishwa  katika ibara ndogo (2) ya ibara  59 na amekuwa  na sifa hizo mfululizo kwa muad  usiopungua  miaka kumi.
Ibara ya 59(4) inasema; ‘Katika kutekeleza  mamlaka yake,Mkurugenzi wa Mashitaka  atakuwa huru ,hataingiliwa  na mtu yeyote  au mamlaka yeyote na atazingatia mambo yafuatayo; (a) nia ya kutenda haki, kuzuia matumuzi mabaya ya taratibu  za utoaji  haki na maslahi ya umma.

Na kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai, kina mpa mamlaka DPP kufunga dhamana ya mshitakiwa na ndiyo kifungu hicho kilichotumia na DPP kufunga dhamana ya Ponda.

Ni kweli dhamana ni haki ya kila mtu ila kuna baadhi ya makosa hayana dhamana na mfano kesi ya mauji, utakatishaji fedha haramu( Money Laundry),unyang’anyi wa kutumia silaha(Amry Robbery) mauji,uhaini na ugaidi (Terrorisms)  lakini kama kifungu hicho cha 148(4) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, kinampa mamlaka DPP kumfungua dhamana mshitakiwa anayekabiliwa na makosa yanayodhaminika.

Sasa kwa mtiririko huo ,misimwelewi Lipumba ana ajenda gani iliyojificha kwenye hii kesi ya Ponda.Kwani Ponda na wenzake bado ni watuhumiwa kama wengine tub ado hajaukumiwa.DPP ametumia madaraka aliyonayo kufunga dhamana ya Ponda na  kuwafungulia mashitaka ya jinai washitakiwa hao ,sasa sijui tabu inatoka wapi.

Mbona viongozi wa iliyokuwa Taasisi ya Upatu (DECI) walivyofunguliwa kesi pale Mahakama ya Kisutu mwaka 2009, na makosa yanayowakabili yalikuwa yanadhaminika kwa mujibu wa sheria lakini  DPP huyu huyu Dk.Feleshi aliwasilisha hati ya kuwafungua dhamana na vigogo ambao kesi yao iliyopo mbele ya Hakimu Stewart Sanga imefikia hatua ya wao wameanza kujitetea,aliwafungia dhamana na walisota gerezani kwa zaidi ya miezi mitatu, mbona hatukuwasikia wanasiasa wala waumini wa dini ya Kikristo au wewe Lipumba na wale wafuasi wengine mnaondamana kila Ijumaa kushinikiza Ponda aachiliwe huru, hamkuandamana kushinikiza waachiliwe huru na kwamba kesi yao vigogo wa DECI ni ya madia?

Tuachane na uhuni huu unaofanywa na wasiasa waliopoteza dira na mwelekeo na waliofirisika kisiasa ambao wao masuala hatarishi na yanayoingilia uhuru wa mahakama ambao uhuru wa mahakama umeainishwa wazi katika Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inasomeka hivi; “Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki ,mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia  tu masharti ya Katiba na Sheria za Nchi’.

Na ibara 107A (1) ya Katiba ya nchi inasema “Mamlaka yenye mamlaka ya mwisho ya utoaji  haki katika jamhuri ya Muungano  itakuwa ni Mahakama.

Kwahiyo kama  kesi inayomkabili Ponda ni ya madai , si jukumu la wewe Lipumba sasa kusema hilo ni jukumu la Mahakama siku ikifika itasema hivyo.

Mwisho napenda kuwaasa wale wanaojiita wafuasi wanaojiita wao ni wafuasi wa  Ponda na sheikh Farid waache kushiriki kwenye vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kisingizo cha kuishinikiza serikali na mahakama imwachilie huru Ponda kwani kufanya hivyo ni wazi wakae wakijua watakuwa wanafunja sheria za nchi watajikuta wanaingia matatani na wao waishia kwa kufunguliwa kesi za jinai mahakamani na kutupwa jela.

Na wale wahuni wachache ambao ni wazi wamechoka kuishi Tanzania kwenye amani wanaoleta vurugu za kidini kwa kisingizio eti wanaitetea dini ya kiislamu, wakome mara moja na kwa uwezo wa mungu hiyo dhamira yao mbaya na kishetani ya kutaka kuingiza Tanzania kwenye machafuko haitafanikiwa nao mwisho wa siku wataambulia kipigo kutoka kwa wanausalama wetu na kufikishwa mahakamani na mwishowe kupelekwa kupumzika katika gereza la Segerea,Keko na kula ugali wa bure na kuwa chini ya ulinzi.

Naendelea kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwadhibiti wahuni hawa wachache wanajaribu kutaka kuatarisha usalama wa taifa letu kwa visingizio visivyokuwa na kichwa wala miguu.Na ninaviomba vyombo vya dola viwashughulikie kikamilifu wale wote wanaoleta vurugu kwa kisingizio cha kutetea dini ya kiislamu wakati bado wakristo,waislamu na wapagani hapa nchini tunaishi kwa upendo,tunafanyakazi pamoja.

Mwisho nimalizie kwa kuwataka waandishi wa habari wenzangu na wanaharakati na wanasiasa ambao huko nyuma tulikuwa mstari wa mbele sana kushikilia bango hadi kuandaa maandamano na kutengeneza mabango na fulani za kulaani tuhuma za ufisadi katika Mkataba wa Dowans,Richmond, mauji ya mwanahabari mwenzetu David Mwangosi,kufungiwa kwa vyombo mbalimbali vya habari.
Mbona wanahabari wenzangu wengi,wanaharakati,na wanasiasa machahari mbona tumeonekana kuwa wapole sana katika matukio haya yanayotaka kuleta chochoko za kidini? 

Hivi  je matukio haya yanayoashiria chokochoko ya udini siyana madhara ya haraka,wazi ambayo yasingezibitiwaharaka na vyombo vya dola na hekima ya viongozi wa dini ya Kikristo na wale wa kiislamu leo hii Tanzania ingekuwa imeingia kwenye machafuko ya kidini?

Tuache unafki,amani ni kitu muhimu sana pote pale duniani na chenye kipaumbele halafu hayo mambo mengine yanafuata.Kwani bila ya kuwepo na amani huo ufisadi usingenyika.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com; Novemba 5 mwaka 2012.

1 comment:

Dave Mwera said...

Mimi nafikiri watu huwa wanakurupuka kusema yale yaliyo kwenye vichwa vyao hata kama siyo sahihi.

Professor Lipumba alipaswa kujua maswala ya mahakama na siyo kuropoka. Je angepewa dhamana ya kuongoza nchi ingekuwaje? Mimi mpaka hapo nina maswali mengi sana.

Kweli wanaharakati, wanasiasa na Wanahabari wamekaa kimya kuhusu hizi chokochoko za kidini ambazo zinataka kuleta uvunjifu wa amani katika nchi yetu.

Nakumbuka huko nyuma ilikuwa vigumu kuibua mambo ya kidini kwasababu kila mtu alikuwa anaheshimu dini ya mwingine. Sasa hivi mambo yanaenda yakibadilika polepole tutajikuta tumefika mahali pabaya kiasi kwamba kurudi itakuwa vigumu.

Eee Mungu Tusaidie!!!!!!!!!!!

Powered by Blogger.