Header Ads

HASANOO SASA AKIMBILIA KORTI KUU KUSAKA DHAMANA 

Na Happiness Katabazi

MWENYEKITI wa Chama cha Soka mkoa wa Pwani (Corefa), Hassani Othman maarufu kama Hasanoo (43)  na wenzake watano ambao wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo kosa la uhujumu uchumi  na kusafirisha Pembe za ndovu zenye thamani ya Sh.bilioni 1.1 kwenda Hong Kong nchini China, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana aliwasilisha ombi la kuomba apatiwe dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.


Hassanoo ambaye anatetewa na wakili wa kujitemea Richard Rweyongeza ndiye aliyewasilisha maombi hayo jana kwanjia ya maandishi kwa niaba ya mshtakiwa hayo ambaye anasota gerezani tangu alipofikishwa katika mahakama ya Kisutu Ijumaa iliyopita akikabiliwa na kesi hiyo mpya ya kusafirisha pembe za ndovu.

Wakili Rweyongeza alifikia hatua ya kuwasilisha ombi hilo jana kwasababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na pia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi hakutoa kibali cha kuruhusu kesi hii isikilizwe katika Mahakama ya Kisutu.

Novemba 23 mwaka huu, siku ambayo kesi hii ilifunguliwa Wakili Mwandamizi wa  Serikali, Shedrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mbando alidai kuwa mbali na Hassanoo washtakiwa wengine ni  Ally Kimwaga, Dastan Mwanga, Godfrey Mwanga, John Mlai na Khalid Fazaldin.

Kimaro alidai shtaka la kwanza ni la kula njama na kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha nyara za serikali bila leseni ambalo walilitenda  kati ya Septemba Mosi na Novemba 20, mwaka huu, Dar es Salaam na Hong Kong kinyume na kifungu cha 384  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Katika shtaka la pili,ni kwamba washtakiwa hao  kwa nia ovu walipanga,wakatekeleza,wakasimamia  na kuwezesha  kifedha  kufanyika kwa biashara hiyo haramu ya kutorosha vipande 569 vya Pembe za ndovu, vyenye uzito wa kilogramu 1330 na thamani ya Sh 1,185,030,000 kwenda Hong Kong, kosa ambalo walilitenda walilitenda kati ya Septemba Mosi na Novemba 20 mwaka huu, kusafirisha nyaraka hizo toka Dar es Salaam , kwenda Hong Kong.

Aidha alidai shtaka la tatu kuwa siku hiyo ya tukio ,washtakiwa walijihusisha  na biashara hiyo ya nyara za serikali  kinyume na kifungu cha 80 na 34 ya uhifadhi wa Wanyama Pori namba 5.

Aliongeza kwa kudai kuwa, washtakiwa hao kwa nia ovu waliendesha biashara hiyo ya nyara za serikali bila ya kuwa na kibali halali kinachowaruhusu kufanya biashara hiyo.

Baada ya wakili Kimaro kumaliza kuwasomea mashtaka hayo , Hakimu Mmbando aliwaambia washtakiwa hao kuwa, kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi, Ritha Tarimo ambaye hayupo na kwa sababu hiyo, na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo washtakiwa hawatatakiwa kujibu chochote.

Wakili Kimaro alidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa ambapo kesi hiyo inakuja leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwaajili ya kutajwa.

Mbali na kesi hiyo, Hasanoo aliyewahi kuwa kiongozi wa Simba pia anakabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa tani 26.475 za madini aina ya Shaba zenye thamani ya Sh333, 467,848.13 kutoka Zambia kinyume na kifungu cha 258, 265 na 269 (c) vya kanuni ya adhabu mali ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania Ltd ambayo ilifunguliwa mahakamani hapo na DPP, mwaka jana na imefikia hatua ya kuanza kusikilizwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 28 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.