Header Ads

DPP ALIA NA LIYUMBA

*Apinga kupunguziwa masharti ya dhamana
*Amtuhumu hakimu kwa kupotosha ukweli

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo inaanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, kupinga uamuzi wa kulegezewa masharti ya dhamana.


Rufaa hiyo namba 44 ya mwaka 2009, itasikilizwa mbele ya Jaji Geofrey Shaidi.
Katika maombi yake, DPP anapingana na uamuzi uliotolewa Mei 28 na Hakimu Mkazi Nyigumalila Maseba wa Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam, wa kumpunguzia masharti ya dhamana mtuhumiwa huyo.

Katika maelezo yake, DPP amebainisha kwamba, Hakimu Maseba, amepotosha na kukiuka matakwa ya kifungu cha 148 kifungu kidogo cha 5E cha sheria za makosa ya jinai iliyorekebishwa mwaka 2002, inayomlazimu mtuhumiwa kulipa kama dhamana, nusu ya mali anayodaiwa kuiba.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, aliieleza mahakama kwamba, kifungu hicho hakiangukii kwenye makosa yanayomkabili Liyumba. Hivyo alitangaza kumwachia kwa dhamana ya sh milioni 300 badala ya sh bilioni 50 kama ilivyokuwa awali.

Kabla ya kusoma uamuzi wake kwa Liyumba anayekabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, Hakimu Maseba, alikumbusha kuwa katika shauri hilo dhamana ilikuwa haibishaniwi bali kilichokuwa kikibishaniwa ni masharti ya dhamana.

“Kwa uamuzi huu, Liyumba sasa atatakiwa atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 300, wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh milioni 50 kila mmoja, zuio la kutoka nje ya Dar es Salaam hadi kwa kibali maalum na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani,” alisema.

Masharti hayo ni tofauti na yale ya awali, alipotakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao wangesaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya nusu ya kiasi cha sh bilioni 221, anachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara.

Sharti lingine la awali, lilikuwa ni kuacha hati za kusafiria mahakamani hapo, kuripoti katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kila Ijumaa na zuio la kutoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali maalum cha mahakama.

Hata hivyo, uamuzi wa kulegezewa masharti ya dhamana, ulimfanya Liyumba apumue, hasa pale Hakimu Maseba aliposema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kulazimika kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kwamba, ni kweli kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka mapya yanayomkabili mshitakiwa huyo.

Alisema, hakuna ubishi kwamba mashitaka yanayomkabili Liyumba ni yale ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 221, hivyo mashitaka hayo ni tofauti kabisa na yanayoainishwa kwenye kifungu hicho.

“Nakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa, kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka yanayomkabili mshitakiwa na kwa sababu hiyo, natupilia mbali ombi la upande wa mashitaka lililotaka mahakama hii itumie kifungu hicho katika kumpatia dhamana mshitakiwa na endapo upande wa mashitaka haujaridhika na uamuzi wake, unaweza kukata rufaa,” alisema Maseba Mei 29 katika Mahakama ya Kisutu na kusababisha mawakili wa serikali kujiinamia.

Liyumba anakabiliwa na makosa mawili ya jinai katika kesi namba 105/2009 kwa matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006 akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Aidha, anadawa kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha kosa linaloangukia kwenye shitaka la kwanza.
Liyumba alisomewa mashitaka mapya baada ya Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, kuwaachia huru baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa ina makosa kisheria.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, walikamatwa tena na Liyumba kusomewa mashitaka mapya, huku Kweka akiendelea kuhojiwa na Takukuru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano,Juni 10,2009

No comments:

Powered by Blogger.