Header Ads

KESI YA ZOMBE KUUNGURUMA TENA JUNI 15

Na Happiness Katabazi

KESI ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake, imepangwa kuanza kunguruma tena Juni 15, Tanzania Daima imebaini.


Vyanzo vya kuaminika toka ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, vimelihakikishia gazeti hili jana kuwa, kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa Juni 15 hadi 19 na itasikilizwa mfululizo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, tayari ratiba ya vikao vya kesi za mauaji ambayo ndani yake imepangwa kesi ya Zombe, tayari imeishaanza kugawiwa kwa mawakili wanaowatetea washitakiwa na wale wa serikali.

‘Ni kweli kesi ya Zombe itakuwa tarehe hiyo na tayari ratiba ya kesi hiyo imeishaanza kutolewa kwa mawakili wa pande zote,” kilisema chanzo chetu.

Kutokana na kupangwa kesi hiyo Juni 15, upande wa mashitaka unatarajiwa kuwasilisha majumuisho ya ushahidi wa kesi hiyo mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati baada ya kikao kilichopita kushindwa kuwasilisha kwa madai ya kutokuwa na muda wa kutosha.

Mbali na upande wa mashitaka, pia wazee wa baraza katika kesi hiyo, nao watapata fursa ya kuwasilisha majumuisho yao.

Mei 7, mwaka huu, mawakili wa utetezi waliwasilisha majumuisho ya ushahidi wa kesi hiyo baada ya washitakiwa kumaliza kutoa ushahidi wao katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, na ikafunga rasmi kupokea ushahidi upande wa utetezi.

Mawakili wa utetezi, Jerome Msemwa, Majura Magafu, Denis Msafiri na Ishengoma, waliiomba mahakama hiyo kuwaachia huru wateja wao kwa kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, umejaa mkanganyiko mkubwa na pia ni wa kuungaunga.

Pia walisema mashahidi katika kesi hiyo, wameshindwa kuthibitisha kama washitakiwa hao walihusika kufanya tukio hilo la mauaji, Januari 14, mwaka 2006.

Wakili Jerome Msemwa ambaye anamwakilisha Zombe, alidai kitendo cha mteja wake kutoa taarifa za mauaji ya watu hao kwenye vyombo vya habari, si kosa, kwani alifanya hivyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa askari wake wa chini.

Mbali ya Zombe na ASP Christopher Bageni, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi.

Washitakiwa hao wanadaiwa Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, waliwaua Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi, mkazi wa Manzese, jijini Dar es Salaam.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Juni 4,2009

No comments:

Powered by Blogger.