Header Ads

KESI YA MAHALU NGOMA NZITO

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya kuisababishia hasara serikali, ya zaidi ya sh bilioni 2, inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Meneja Utawala na Fedha, Grace Martin, umedai kuwa upande wa mashitaka ulikosea kufungua kesi hiyo kabla ya kuwaondolea kinga ya kidiplomasia washitakiwa hao.


Hoja hiyo ni miongoni mwa hoja nne ziliozowasilishwa jana katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, mbele ya Jaji Juxston Mlayi na kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Mabere Marando aliyekuwa akisaidiwa na Alex Mgongolwa, Bob Makani na Cuthbert Tenga.

Jana, Mahalu na mwenzake, waliwasilisha ombi namba 2/2009, dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), la kuomba mahakama hiyo ipitie mwenendo wa kesi ya msingi inayowakabili, ambayo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Marando aliiambia mahakama hiyo jana kuwa, walifikia uamuzi wa kuwasilisha ombi hilo la mapitio mahakamani hapo baada ya kubaini dosari kubwa tatu za kisheria licha ya kumweleza Hakimu Mkazi, Sivangilwa Mwangesi, anayesikiliza kesi hiyo ambaye hajazipatia ufumbuzi.

Kwa mujibu wa Marando, dosari ya kwanza ni kwamba washitakiwa wote ni wanadiplomasia, hivyo wana kinga ya kidiplomasia kwa mujibu wa sheria.

Alidai kuwa, mtu mwenye kinga ya aina hiyo, ataendelea kuwa nayo, na itaendelea kumlinda kwa mambo aliyoyafanya akiwa nayo, hadi pale mamlaka husika itakapomuondolea.

‘Sasa cha kushangaza, upande wa mashitaka ulikurupuka na kuwafungulia kesi washitakiwa hawa, ambao hadi sasa wana kinga ya kibalozi, kwa sababu mamlaka husika haijawaondolea kinga, hivyo kitendo cha serikali kuwashitaki, huku ikijua fika haijawaondolea kinga, ni makosa na hawakupaswa kushitakiwa,” alidai Marando.

Alitaja dosari ya pili kuwa, washitakiwa walifunguliwa kesi bila ya kibali cha DPP.

Marando alifafanua kuwa, washitakiwa walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Januari 22 mwaka 2007 na wakati wote huo, hati ya mashitaka haikuwa na kibali cha DPP hadi Aprili 25, mwaka huo, DPP Eliezer Feleshi, alitoa kibali.

Marando alitumia kifungu cha 26(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambayo inatamka bayana kuwa, shauri lolote linaloangukia kwenye makosa ya uhujumu uchumi, alipaswi kufunguliwa mahakamani bila kibali cha DPP.

“Mheshimiwa Jaji Mlayi, kifungu hicho kinakataza makosa kama haya yanayowakabili washitakiwa, yasifunguliwe bila kibali cha DPP, lakini upande wa mashitaka walifungua kesi hii bila kibali cha DPP. Na hili lipo wazi kabisa, kwani kesi ilifunguliwa Januari 22 mwaka 2007 na kibali cha DPP kikaja kuwasilishwa mahakamani Aprili 25, mwaka huu, hii ni ni kosa kisheria,” alidai Marando.

Wakili Alex Mgongolwa alidai kuwa, dosari ya tatu ni kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, haikuwa na mamlaka ya kuendesha kesi inayowakabili washitakiwa hao, kwa madai kuwa makosa yanayowakabili, yalifanyika nchini Italia na kwamba Italia haijumuishi mahakama hiyo.

“Na kwa mujibu wa kifungu cha 59(3) cha Sheria ya Mahakimu inayoainisha mipaka ya mahakama za hakimu mkazi nchini kuendesha kesi, kwa hiyo kabla ya kesi ya msingi kufunguliwa, walipaswa kuomba kibali toka kwa Jaji Mkuu ili Mahakama ya Kisutu iongezewe mipaka ya kuendesha kesi hiyo, pia uamuzi ule wa Mahakama ya Kisutu kupokea ushahidi wa shahidi wa upande wa mashitaka, anayeishi Italia kwa njia ya video, ni wazi kabisa Mahakama ya Kisutu ilivuka mipaka yake bila kupata kibali cha kuongezewa mipaka na Jaji Mkuu,” alidai Mgongolwa.

Akijibu pingamizi la upande wa mashitaka la kutaka mahakama hiyo isisikilize ombi la Mahalu, kwa sababu hakukuwa na ulazima wa kusikiliza, Mgongolwa alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu 43(1),44(1),(a) cha Sheria ya Mahakimu na kifungu cha 372 na 373(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, zinatoa nguvu kwa Mahakama Kuu kusikiliza ombi la mapitio ya jalada la kesi, ambalo kesi ya msingi imefunguliwa katika mahakama ya chini.

“Kwa sababu hiyo, tunaomba mahakama hii itupilie mbali mwenendo mzima wa kesi, kwa sababu umejaa dosari za kisheria ambazo zipo wazi na kisha iwaachilie huru washitakiwa,” alidai Mgongolwa.

Wakati mawakili wa utetezi wakibainisha dosari hizo kwa vielelezo, upande wa mashitaka ulionekana kukumbwa na wakati mgumu wa kupangua hoja hizo kwa vielelezo.
Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, akijibu hoja hizo alidai kuwa, hakukuwa na umuhimu wa mahakama hiyo kufanya mapitio.

Kuhusu hoja kwamba Mahakama ya Kisutu haikuwa na mamlaka ya kuendesha kesi hiyo, wakili huyo alidai kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ni Tanzania.

Hoja hiyo ilisababisha Jaji Mlayi kumtaka Boniface ampatie ushahidi unaoonyesha kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ni Tanzania, ambapo Boniface alimweleza jaji kuwa anamtuma Mwanasheria wa Takukuru, Ponsian Lukosi ambaye alikuwa akisaidiana naye, kwenda maktaba ya mahakamani hapo kwa muda ili akachukue ushahidi huo, lakini hadi ombi lilipomalizwa kusikilizwa jana saa saba mchana mahakamani hapo, Lukosi alirudi bila kuwa na ushahidi huo.

“Upande wa Mashitaka sijasahahu, nipatie huo ushahidi, mlioenda kuusaka unaonyesha Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ni Tanzania,” alisema Jaji Mlayi na kusababisha mawakili wa upande wa mashitaka kujiumauma bila kutoa maelezo yanayoeleweka, hali iliyosababisha watu kuangua vicheko.

Akijibu hoja ya washitakiwa hao kwamba hawakupaswa kushitakiwa kwa sababu hawajaondolewa kinga ya kidiplomasia, Boniface alijibu kwa kifupi bila kuonyesha vielelezo vyovyote, kwa kudai wana haki ya kushitakiwa.

Mgongolwa akijibu hoja hizo, alidai yote yaliyowasilishwa na upande wa mashitaka hayana msingi, na kwamba hakuna kitu muhimu katika sheria kama mamlaka na kusisitiza kuwa jambo likifanyika nje ya mamlaka husika ni batili.

Kuhusu hoja kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ni Tanzania, Marando alidai kuwa, hoja hiyo si sahihi kwa kuwa ubalozi wetu kuwa Italia ni upendeleo na kutolea mfano kuwa mwaka 1998 Ubalozi wa Marekani ulivyolipuliwa hapa nchini Tanzania, iliamua kuipatia Marekani eneo jingine la Msasani na kujenga tena ubalozi wake na kuhoji kwamba ina maana sehemu zote hizo ni nchi ya Marekani, jambo liloibua vicheko tena mahakamani hapo.

Kutokana na malumbano hayo ya hoja za kisheria, Jaji Mlayi alisema atatoa uamuzi kuhusu wa hoja hizo Juni 8.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Juni 4, 2009

No comments:

Powered by Blogger.