Header Ads

WAKILI ATAKA WASHITAKIWA EPA WAACHIWE HURU

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwaachia huru washitakiwa wa kesi hiyo, kwa madai kuwa ushahidi ulitolewa na upande wa mashitaka ni dhahifu na umeshindwa kuonyesha kiasi cha fedha walichoiba.


Washitakiwa katika kesi hiyo ni Mweka hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda na mpwa wake, Farijala Hussein ambaye ni mfanyabiashara na wote ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Wakili wa utetezi, Majura Magafu alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Cypriana William, ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, ambaye anasaidiana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Phocus Bambikya na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela, kusikiliza kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, jana, upande wa utetezi ulikuwa ukiwasilisha majumuisho ya ushahidi, ikiwa ni siku chache baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi wake.
Magafu alieleza kuwa, kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa ya kula njama, kughushi, wizi na kujipatia ingizo kwenye akaunti isivyo halali. Upande wa mashitaka ulileta jumla ya mashahidi tisa.

Alidai kuwa, mashahidi walioletwa na upande wa mashitaka, wameshindwa kuithibitishia mahakama kuwa washitakiwa hao na wengine ambao hawapo mahakamani, walipanga njama ya kuiibia BoT.

Akitolea mfano shahidi wa sita ambaye ni Ofisa wa Jeshi la Polisi, Salum Kisai, alidai kuwa licha ya kuwa ni mpelelezi, haukueleza wakati gani, mahali washitakiwa walipanga njama za kuibia Benki Kuu.

Akizungumzia hati ya kuhamisha deni lililotumiwa na washitakiwa kuonyesha MS/BC Cars Export Limited imewapatia idhini ya kukusanya deni la Kampuni ya Kiloloma & Brother inayomilikiwa na washitakiwa, kuwa hati hiyo ilighushiwa, alidai hakuna ushahidi uliothibitisha hilo.

Aidha alieleza kuwa, kosa la kula njama linaambatana na makosa mengine ya kujipatia usajili kwa njia ya udanganyifu na kughushi, kwa hiyo hakuna shahidi aliyekuja kuithibishia mahakama kwamba hati ya kuhamisha deni ‘deed of assignment’ ilighushiwa.

Magafu akifafanua kuwa, katika shitaka la wizi, hadi sasa hakuna mtu yeyote, awe Gavana, Naibu Gavana au Mkurugenzi wa Fedha toka BoT, aliyefika mahakamani hapo kueleza fedha za benki hiyo zilivyoibwa na kuongeza kuwa, waliokuja kutoa ushahidi walionyesha utaratibu wa kutoka kwa fedha ambao si shida ya mahakama.

Kuhusu shitaka la kujipatia ingizo la fedha kwa njia ya udanganyifu, Magafu alidai hakuna shahidi toka BoT au MS/BC Cars Exports Limited, aliyekuja kusema fedha zilizoingizwa kwenye kampuni ya washitakiwa ya Kiloloma & Brothers na hazikuingizwa kihalali.

Novemba mwaka jana, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka sita, kwamba mwezi Mei mwaka 2005 waliiba zaidi ya sh bilioni 1.8, mali ya BoT.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Juni 5, 2009

No comments:

Powered by Blogger.