Header Ads

VIGOGO DECI KIZIMBANI

*Wanadaiwa kuendesha shughuli za upatu bila leseni
*Watupwa rumande, ndugu zao waangua kilio kortini
*Kamati ya dharura DECI sasa wapanga kuandamana

Na Happiness Katabazi

BAADA ya vuta nikuvute kati ya viongozi na wanachama wa Kampuni Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), inayojihusisha na shughuli za kuvuna na kupanda pesa, hatimaye jana viongozi watano wa kampuni hiyo, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijni Dar es Salaam.

Viongozi hao walifikishwa mahakamani hapo, majira ya saa nane mchana, chini ya ulinzi wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao waliambatana na makachero wa polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Makao Makuu ya Upelelezi ya jeshi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika toka ndani ya jeshi hilo, watuhumiwa hao walikamatwa tangu juzi na kuchukuliwa maelezo na hatimaye jana kufikishwa mahakamani.

Wakili Kiongozi wa Serikali, Justus Mlokozi, akisaidiana na Prosper Mwangamila, mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Addy Lyamuya, alidai kuwa washitakiwa wote ni wachungaji wa Kanisa la Pentekoste.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saigaran ole Loitginye, Samwel Sifael Mtares, Arbogast Francis Kipilimba na Samwel Mtalis.

Washitakiwa hao ambao walirudishwa rumande, wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Simon Kitululu, Onesmo Michael, Shambwee Shitambala na Hudson Ndusyepo.

Kwa mujibu wa Mwangamila, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1,3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.

Alidai kuwa, kati ya mwaka 2007 na Machi 2009, katika makao makuu ya DECI, yaliyopo Mabibo Mwisho, jijini Dar es Salaam, washitakiwa waliendesha na kusimamia mradi wa upatu katika sehemu tofauti nchini kwa ahadi ya kuwapa wanachama wake fedha zaidi ambazo katika mazingira ya kibiashara ni kubwa kuliko mradi waliokuwa wakiufanya.

Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kupokea amana za umma bila kuwa na leseni kinyume na kifungu cha 6(1,2) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha Na.5 ya mwaka 2006 na kwamba, washitakiwa wote katika kipindi hicho, wakiwa kwenye ofisi zao za DECI, walipokea amana kutoka kwa umma bila leseni.

Washitakiwa wote walikana mashitaka hayo na wakili huyo wa serikali alidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa kesi hiyo.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, aliomba wateja wake wapewe dhamana kwa kuwa ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na ni wachungaji wa dhehebu la Pentekoste.

Ombi hilo lilipingwa na wakili kiongozi wa serikali, Mulokozi na kutoa hati ya kiapo cha mpelelezi mkuu wa kesi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Essack Mugassa ambacho kinataka washitakiwa wasipewe dhamana.

Alidai kuwa, endapo washitakiwa hao watapewa dhamana, wanaweza kuvuruga upelelezi na kuongeza kwamba tayari wameshawapatia upande wa utetezi hati hiyo ya kiapo.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, imeahirishwa hadi Juni 17 na washitakiwa wote walirejeshwa rumande.

Wakati washitakiwa hao wakipandishwa kwenye karandinga tayari kwa ajili ya kupelekwa rumande, baadhi ya ndugu na jamaa zao waliokuwa kwenye viunga vya mahakama hiyo, walishindwa kuvumilia na kuanza kuangua kilio, huku ndugu wengine pamoja na baadhi ya wanachama, wakiwa wamekaa vikundi wakitafakari hali hiyo.

Mapema mwaka huu, Kampuni ya DECI iliyowanufaisha watu wengi hasa wale waliojiunga mwanzoni, iliibua malumbano kati ya serikali, viongozi wa kampuni hiyo na wanachama wao, waliopinga hatua ya serikali kusitisha shughuli zake kwa madai kuwa haiko kihalali.

Kusimamishwa kwa shughuli za kampuni hiyo, kulitokana na uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutoa taarifa ya kuwataadharisha Watanzania waliojiunga na upatu huo kuwa, taasisi hiyo haiko kisheria na wanaweza kupoteza fedha zao walizopanda.

Shughuli za kupanda na kuvuna mbegu DECI, zilisitishwa baada ya serikali kusimamisha akaunti za kampuni hiyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika, hali ambayo baadaye ilisababisha uvunjifu wa amani katika ofisi za kampuni hiyo, baada ya wanachama wake kuamua kuchukua sheria mkononi kwa kuvunja vioo vya magari ya viongozi, wakitaka warejeshwe fedha zao.

Katika hatua nyingine, kamatai ya dharura ya wanachama wa DECI, wamefanya kikao cha ghafla jana mara baada ya viongozi wao kutupwa rumande, wakipinga hatua hiyo.
Kamati hiyo inayoongozwa na Isack Kalenge, inawataka wanachama wa DECI nchi nzima kuandamana Jumatano ijayo ili kuishinikiza serikali kuwaachia huru viongozi wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Juni 13, 2009

No comments:

Powered by Blogger.