SOS:SHIRIKA LILILOJENGA KIJIJI CHA WATOTO YATIMA
*NIA NI KUWALEA KATIKA FAMILIA ZENYE UPENDO
TATIZO la watoto wa mitaani wanaoishi katika mazingira hatari hapa nchini kadri siku zinavyozidi kusonga mbele linaanza kukua. Katika makala hii Mwandishi Wetu HAPPINES KATABAZI, amezungumza na Mkurugenzi wa Kijiji cha Watoto cha SOS Dar es Salaam, Dk. Alex Lenguju,(Pichani) na anatuelezea zaidi jinsi kijiji hicho kilivyojipanga kuwaokoa watoto wanaoishi katika mazingira mahumu.
Swali: Tueleze kwa mapana SOS Children Villages International nini?
Jibu: Shirika la SOS Children’s Villages International ni Shirika huru la Maendeleo ya Jamii lisilo la Kiserikali wala la Kidini, shirika hili linalenga hasa matunzo ya muda mrefu ya watoto yatima na waliotelekezwa katika mfumo wa familia mbadala. Katika mfumo huu, watoto wanalelewa kwa muda mrefu katika nyumba za familia zinazojitegemea ambazo kwa pamoja zinaunda Kijiji cha SOS.
Swali: Shirika lilianzishwa lini?
Jibu: Shirika hili lilianzishwa na Herman Gmeiner wakati alipojenga kijiji cha kwanza cha Watoto cha SOS mwaka 1949 katika mji wa Imst huko Austria. Katika vijiji vya SOS vya watoto tumejitolea kabisa katika ustawi wa watoto. Lakini pia tumejitolea kwa dhati kabisa kuimarisha familia na jamii kwa ujumla kama njia madhubuti ya kuzuia utelekezaji wa Watoto.
Shirika hili shirika la kwanza kuanzisha huduma kabambe ya malezi muda mrefu ya watoto yatima na waliotelekezwa katika mfumo wa familia mbadala ambapo hadi sasa linaongoza duniani katika utekelezaji wa mfumo huu. Mfumo wetu wa malezi ya watoto umejengwa juu ya kanuni kuu nne za msingi za Muundo wa Malezi wa SOS:
Kila mtoto anapata mzazi mmoja anayemjali, kumtunza na aliyekaribu naye kabisa wakati wote. Katika Kijiji cha Watoto cha SOS, watoto wanaishi katika nyumba za familia kila na kila nyumba inaongozwa na mama. Mama wa SOS anajenga uhusiano wa karibu na kila mtoto aliyekabidhiwa kwake akimpatia kila mtoto usalama, upendo na uthabiti ambao kila mtoto anahitaji ili aweze kukua vyema. Mahusiano ya kifamilia yanajengeka yenyewe kama kaka na dada. Katika nyumba za familia chini ya uangalizi wa mama, watoto wanakuwa pamoja kama kaka na dada wa familia moja, kwa namna hii wanajenga muunganiko wa kudumu kati yao.
Kila nyumba inatengeneza nyumbani kwao wenyewe, hapo ndipo wanapotoka na hapo ndipo wanaporudi. Chini ya paa la nyumba hii watoto wakiwa na mama yao wanapata kujisikia salama na kuwa wako kwao kweli kweli.
Famila ya SOS ni sehemu ya jamii. Familia imo ndani ya Kijiji ambacho ndicho kinachoipa familia mazingira ya jamii pana ambamo watoto wanapata fursa ya kufurahia utoto kwa furaha na wakati huo huo wanajifunza kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijumuiya. Mkurugenzi wa Kijiji ndiye pia Baba wa Kijiji, watoto wanamtambua kuwa ni baba yao. Baba wa kijiji pamoja na wafanyakazi wenza wa kiume wanawapatia watoto mambo muhimu wanayohitaji.
Swali: Matarajio yenu ya baadaye ni yapi?
Jibu: Matarajio ya SOS kwa ajili ya watoto wote duniani ni kufika hatua ambapo kila mtoto yumo ndani ya familia na anapata fursa ya kukua kwa upendo, heshima na usalama. Katika SOS tumepania mambo matatu makuu ikiwemo kujenga familia mbadala kwa watoto ambao hawana familia ili waweze kutengeneza mustakabali wao na kushiriki katika maendeleo ya jamii ambako watoto hawa wanatoka. Tunataka kila mtoto anayeingia katika malezi yetu afike hatua ya kuwa mtu mwenye mafanikio na mwanajamii anayeweza kutoa mchango wa maana katika jamii anamoishi. Sisi katika SOS tunaheshimu dini na tamaduni mbalimbali na tunafanya kazi kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa Juu ya Haki za Mtoto.
Swali: SOS ina fanyakazi katika nchi zipi?
Jibu: Kwa sasa SOS inafanya kazi katika nchi zaidi ya 132 duniani kote; ikiwa na Vijiji vya Watoto zaidi ya 470 na pia vituo mbalimbali vya huduma vya SOS kama vile Shule, Vituo vya Kijamii, Vituo vya Afya na Shule za Ufundi. Hivyo, kwa miaka zaidi ya 50 sasa wale wanofuata nyayo za mwanzilishi wa SOS wamesambaza wazo la SOS hadi kufika katika nchi mbalimbali, tamaduni, dini na mitindo ya maisha. Hapa Tanzania kijiji cha kwanza cha SOS kilifunguliwa Zanzibar mwaka 1991 katika eneo la Mombasa. Mei 2000, kijiji cha pili hapa nchini ambacho ni cha kwanza Tanzania bara kilifunguliwa huko Arusha katika eneo la Ngaramtoni.
Swali: Tueleze kijiji cha SOS Dar es Salaam kina jumla ya watoto wangapi?
Jibu: Kijiji cha SOS cha Dar es Salaam tunachokitambulisha sasa ni cha tatu katika nchi yetu. Kijiji hiki kinapokea watoto wachanga hadi wa miaka 6, ambao wanatunzwa hadi kufikia utu uzima ili nao wajitegemea wenyewe. Kijiji hiki kina jumla ya nyumba za familia 13, zenye uwezo wa kutunza watoto 130 kikiwa kimejaa. Kwa sasa tuna watoto 122 katika kijiji hiki, lakini tunatarajia kufikia watoto 120 hadi mwisho wa mwezi huu na kutimiza idadi kamili ya watoto 130 kabla ya mwisho wa mwaka 2010. Pamoja na mpango wa malezi ya watoto ya muda mrefu katika mfumo wa familia, shirika pia lina mpango wa kuimarisha familia hapa Dar es Salaam.
Mpango huu unalenga kuwasaidia watoto wenye uhitaji ambao hawakuweza kupata nafasi katika Kijiji na ni sehemu muhimu sana ya mkakati wa SOS wa kuzuia utelekezaji wa watoto.
Kwa wakati huu mpango wa kuimarisha familia unahudumia familia 52 zenye jumla ya watoto 202 na walezi wao, wengi wakiwa kutoka Manispaa ya Temeke, Kinondoni, Ilala na Bagamoyo. Hawa wanapewa huduma za chakula, matibabu, mahitaji ya shule na mafunzo mbalimbali kwa walezi.
Aidha SOS inasaidia familia kuandaa maendeleo ya mpango miaka 3-5 ili baada ya miaka hiyo ziweze kujitegemea. Na tumekuwa zikipatiwa misaada ya chakula, tiba, elimu na mafunzo ya ujasiriamali, malezi na afya.
Lengo kuu la mpango huu ni kuzuia utelekezwaji watoto kwani watu wengine wanatelekeza watoto kwasababu ya kushindwa kuwahudumia na mpango huo unapofanikiwa, idadi ya watoto wa mitaani na wanaolelewa kwenye vituo itapungua.
Lengo jingine la mpango huo wa kuimarisha familia ni kutetea haki za wa watoto. SOS pia inashirikiana na mashirika mengine ili kuhakikisha watoto kwenye jamii wanapata haki stahili kama vile chakula, mahali pa kulala na ulinzi salama. Hili halijaanza hapa Tanzania, lakini SOS inataka kuwa sauti ya watoto katika jamii ili familia ifahamu katika kulinda, kusimamia na kutetea haki za watoto.
Swali: Serikali inaisaidiaje SOS?
Jibu: Mchango mkubwa wa serikali ni pale ilipotoa idhini ya shirika la SOS lifanye kazi hapa nchini. Pia ilitoa ardhi kwetu hadi vijiji vikajengwa hapa Sinza C, inatupatia msamaha wa kodi wa vifaa vya watoto na kadri ya uwezo wake inatoa ruzuku. SOS inategemea michango kutoka kwa jamii kwa asilimia 100 kwaajili ya kuendelea kujenga na kuendesha kijiji hicho. Kila kitu kinatoka kwa watu wenye mapenzi mema katika jamii.
Hadi sasa sehemu kubwa ya misaada inakuwa ikitoka kwa wanajamii nje ya nchi lakini hivi karibuni Watanzania wameanza kupata mwamko wa kujitokeza, kusaidia watoto wetu kwa aina ya kuchangia fedha au mali na mashirika machache yameonyesha nia ya kutaka kusaidia kama vile Commercial Bank of Afrika, Zain, Vodacom, Kibo Trade na Hoteli ya Kempiskin Kilimanjaro inayotusaidia kwa kukusanya michango toka kwa wateja wake na kisha kutuletea hapa kijijini.
0716-774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Juni 6, 2009
No comments:
Post a Comment