Header Ads

SERIKALI YASISITIZA ZOMBE ANA HATIA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa serikali katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane, umejigamba kuwa umethibitisha kesi hiyo pasipo shaka, hivyo kuiomba mahakama kuwatia hatiani washitakiwa hao kwa makosa waliyoshitakiwa.


Akiwasilisha majumuisho ya kesi hiyo jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Wakili wa Serikali, Mugaya Mtaki aliyekuwa akisaidiana na Angaza Mwipopo, Alexander Msikila na Justus Kaishozi, alidai katika kuthibitisha kesi hiyo, walileta mashahidi 37 na kutoa vielelezo 23.

Akichambua ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, Mtaki, alidai ushahidi uliotolewa na daktari umethibitisha kuwa marehemu hao walikuwa wamepigwa risasi na kuitaka mahakama kuondokana na dhana kwamba walipambana na polisi.

“Wakili wa utetezi, Majura Magafu, alitoa hoja ya kuwa hakukuwa na ubishi marehemu wote walikamatwa wakiwa hai. Sisi tunakubaliana na ukweli huo kwani umethibitishwa na shahidi wa 2, 6 na 7 wa upande wa mashitaka.

“Jambo jingine ambalo tunaomba mahakama yako ikubaliane na sisi kuwa halina ubishi, ni washitakiwa Zombe, Christopher Makele na Hemed Makele walikwenda Kituo cha Polisi Urafiki kushughulikia kielelezo cha fedha,” wakili wa serikali alimweleza Jaji Salum Massati.

Pamoja na hayo, wakili huyo aliiomba mahakama kuzingatia ushahidi wa mshitakiwa Makale uliodai Zombe ni muongo kwa kusema kuwa alikuwa hajui kilichokuwa kikitendeka, na kwamba yeye (Makele) aliandika taarifa za uongo kwa Tume ya Jaji Mussa Kipenka na ACP-Mgawe kwa maelekezo yake.

“Kwa muhtasari ushahidi huo ndiyo unamuhusisha Zombe kwa sababu alikuwa anajua tukio japo hakuwepo msitu wa Pande. Ni rai yetu Zombe aonekane na hatia kama washitakiwa wengine.

“Na hatua ya Msemwa (Wakili wa Zombe) kumfananisha Zombe na Yesu, kwamba anasulubiwa bila hatia, sisi tunasema mshitakiwa huyo hastahili kufananishwa na Yesu, kwani katika kesi ya Yesu, yule jaji wa Kirumi alikuwa na roho ya kikatili, ndiyo maana hakamtia Yesu hatiani licha ya Pilato aliuliza kuna ushahidi gani wa Yesu kutiwa hatiani.

“Katika kesi hii upande wa mashitaka tumethibitisha kesi yetu na wewe ni jaji unayesimamia haki, hivyo usifananishwe na jaji aliyemsulubu Yesu,” alidai Mtaki na kusababisha watu kuangua kicheko mahakamani.

Aliendelea kueleza kuwa, ushahidi wa utetezi unaonyesha kuwa Zombe hakuwapo msitu wa Pande, lakini alihoji ni kwa nini upande huo unashindwa kueleza wakati huo Zombe alikuwa wapi.

“Mtukufu Jaji, common intention siyo lazima washitakiwa wakae pamoja kupanga kabla ya kutenda kosa, kwa hiyo mahakama hii iuzingatie ushahidi uliotolewa kuwa washtakiwa wana hatia.

“Endapo Zombe na Gwasabi hawataonekana na hatia katika kesi ya mauaji, basi tunaomba washitakiwa hawa waonekane na hatia kwamba walishiriki kuficha kosa wakati likitendeka,” alieleza.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Salum Massati, aliwaasa wazee wa baraza, Magreth Mossi na Nicolas Kimolo, kutoa maoni yao kuhusu kesi hiyo kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.

Pia aliwataka kutozingatia yale yaliyoripotiwa na vyombo vya habari, kwani yameandikwa mengi kuhusu kesi hiyo. Leo wazee hao wa baraza wanatarajiwa kutoa maoni yao ya mwisho katika kesi hiyo.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi.

Zombe na wenzake, wanadaiwa kufanya mauaji hayo Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, ambapo waliwaua Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, Juni 26,2009

No comments:

Powered by Blogger.