Header Ads

MAHAKAMA KUU YAMNG'ANG'ANIA PROFESA MAHALU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeyatupa maombi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Meneja Utawala wa Fedha, Grace Martin, wanaokabiliwa na kesi ya kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh bilioni 2.
Katika maombi hayo, washitakiwa hao walitaka mahakama hiyo iwaachilie huru kwa sababu mwenendo mzima wa kesi yao ya msingi, una dosari za kisheria.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Juxon Mlayi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili wiki iliyopita.

Katika uamuzi huo, Jaji Mlayi alisema ombi la Mahalu kuwa upande wa mashitaka ulikosea kufungua kesi hiyo kabla ya kuwaondolea kinga ya kidiplomasia, haina msingi kwa kuwa katiba ya nchi inatamka wazi kwamba mwenye kinga ya kutokushtakiwa ni rais pekee.

Alisema washitakiwa hao kweli wana kinga, lakini inatumika kuwakinga wanapokuwa Italia na kwamba serikali ile isingekuwa na mamlaka ya kuwashitaki hadi hapo Serikali ya Tanzania ingewaondolea kinga, lakini kwa kuwa washitakiwa hao ni watumishi wa umma, serikali ina mamlaka ya kuwashitaki bila hata ya kuwaondolea kinga.

Kuhusu hoja kuwa walifunguliwa kesi bila ya kuwapo kibali cha Mkrugenzi wa Mashitaka (DPP), Jaji Mlayi alisema baada ya kupitia jalada la kesi hiyo, ameona vibali viwili vya DPP, kimoja kikionyesha kesi hiyo ilikuwa ikiwakabili washitakiwa watatu na kibali cha pili, kinaonyesha washitakiwa wawili.

Alisema kibali hicho cha pili, kiliwasilishwa baada ya mshitakiwa mmoja ambaye alikuwa akishitakiwa pamoja na washitakiw hao, kufutiwa mashitaka na DDP.

Aidha, akichambua ombi kuwa Mahakama ya Kisutu, haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa sababu makosa ya washitakiwa yalitendeka nchini Italia na si hapa nchini, Jaji Mlayi alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inatoa mamlaka ya kumshitaki mtu aliyefanya makosa hata nje ya Tanzania.

Kuhusu ombi la waombaji waliokuwa wakipinga uamuzi wa Hakimu Mkazi, Sivangilwa Mwangesi wa kuchukua ushahidi kwa njia ya video, Jaji Mlayi alisema hawezi kulitolea uamuzi kwa sababu lilikwishatolewa uamuzi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hata hivyo, alitupa ombi la pingamizi la upande wa mashitaka, lililotaka mahakama hiyo isikubali kusilikiza maombi hayo.

Baada ya uamuzi huo kutolewa, wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, hawajaridhishwa na uamuzi huo, na wanakwenda kujiandaa kwa ajili ya kukataa rufaa katika Mahakama ya Rufani.

Juni 3, mwaka huu, mawakili wa utetezi, Mabere Marando aliyekuwa akisaidiwa na Mgongolwa, Bob Makani na Cuthbert Tenga wanaowatetea waombaji, waliomba Mahakama Kuu iwaachie washitakiwa hao kwa madai kuwa kesi hiyo ilifunguliwa bila kibali cha DPP.

Marando alifafanua kuwa, washitakiwa walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Januari 22 mwaka 2007 na wakati wote huo, hati ya mashitaka haikuwa na kibali cha DPP hadi Aprili 25, mwaka huo, DPP Eliezer Feleshi, alitoa kibali.

Marando alitumia kifungu cha 26(1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambayo inatamka bayana kuwa, shauri lolote linaloangukia kwenye makosa ya uhujumu uchumi, alipaswi kufunguliwa mahakamani bila kibali cha DPP.

Wakili Mgongolwa alidai kuwa, dosari ya tatu ni kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, haikuwa na mamlaka ya kuendesha kesi inayowakabili washitakiwa hao, kwa madai kuwa makosa yanayowakabili, yalifanyika nchini Italia na kwamba Italia haijumuishi mahakama hiyo.

Akijibu pingamizi la upande wa mashitaka la kutaka mahakama hiyo isisikilize ombi la Mahalu, kwa sababu hakukuwa na ulazima wa kusikiliza, Mgongolwa alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu 43(1),44(1),(a) cha Sheria ya Mahakimu na kifungu cha 372 na 373(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, zinatoa nguvu kwa Mahakama Kuu kusikiliza ombi la mapitio ya jalada la kesi, ambalo kesi ya msingi imefunguliwa katika mahakama ya chini.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 9,2009

No comments:

Powered by Blogger.