Header Ads

WAKILI WA LIYUMBA ACHARUKA

Na Happiness Katabazi

WAKILI wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, Majura Magafu, amecharuka mahakamani na kudai kuwa upande wa mashitaka una hila, na unafurahia kuona mshitakiwa huyo anaendelea kusota mahabusu.


Wakati wakili huyo akicharuka, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeitisha jalada la kesi hiyo namba 105/2009, inayomkabili Liyumba, ili iweze kupitia uamuzi wa kulegeza masharti ya dhamana, uliotolewa na Mahakama ya Kisutu, Ijumaa iliyopita.

Hatua hiyo ya Mahakama Kuu, imetokana na upande wa mashitaka kuwasilisha ombi hilo la mapitio katika mahakama hiyo ya juu.

Wakili wa utetezi, Magafu anayesaidiana na Hudson Ndusyepo na Profesa Gamalieli Mgongo Fimbo, aliikumbusha mahakama hiyo kuwa shauri hilo jana lilikuwa limekuja kwa ajili ya mahakama kuhakiki hati za masharti ya dhamana ili mshitakiwa aweze kudhaminiwa.

Magafu alidai kuna wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi wa BoT watakaosaini bondi ya sh milioni 50 kila mmoja, na kivuli cha hati ya nyumba iliyopo kitalu 2232 na 3233 Mtaa H, Mbezi Beach, yenye thamani ya sh milioni 882, mali ya mshitakiwa na kivuli cha hati ya kusafiria.

Alisema wamefikia kuwasilisha vivuli hivyo na si nyaraka halisi kwa kuwa bado zinahifadhiwa mahakamani hapo kwani zilitumika katika kesi Na 27/2009, iliyofutwa Jumatano iliyopita, na kwamba licha kuwasilisha maombi ya kutaka warejeshewe hati hizo, bado hawajarejeshewa.

“Tumefikia uamuzi wa kuwasilisha vivuli vya hati hizo kwa kuwa hati halisi bado zipo mikononi mwa mahakama hii na Ijumaa iliyopita tuliomba turejeshewe, lakini bado hatujarejeshewa.

“Pia Ijumaa tuliwawasilisha hati nyingine kwa upande wa mashitaka na pia leo asubuhi tuliwapatia hati nyingine ili wahakiki, lakini hadi tunaingia mahakamani hapa, hawajatupatia jibu, hivyo tunaomba mahakama hii ikubali kupokea hati hizo, huku tukisubiri kupata hati halisi ili mshitakiwa leo apate dhamana,” alisema Magafu.

Akijibu hoja hizo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Justus Mlokozi, ambaye alikuwa akisaidiana na Prosper Mwangamila na John Wabuhanga, alidai kuwa bado hawajathibitisha usafi wa hati hizo ambazo upande wa utetezi unataka zitumike kumdhamini mshitakiwa.

Mulokozi alidai kuwa, hati waliyopewa Ijumaa, inaonyesha ilifanyiwa tathimini Agosti mwaka 2008 na kuongeza kuwa, kuanzia wakati huo hadi jana, ni kipindi kirefu na chochote kinaweza kutokea kuhusu hati hiyo, hivyo aliomba wapewe muda kujiridhisha.

“Mheshimiwa hakimu, kilichosemwa na Mulokozi kimeonyesha wazi serikali ina hila, na inafurahia Liyumba anavyoendelea kusota mahabusu,” alidai Magafu.

Kauli hiyo ilisababisha Mulokozi kuinuka na kuiomba mahakama imwamuru Magafu atoe tuhuma hizo chini ya kiapo na aache kuikashifu serikali.

Hali hiyo ilimfanya Magafu ainuke tena kwenye kiti chake, na kuendelea kudai kuwa jukumu la kuhakiki masharti ya dhamana ni la mahakama, si upande wa mashitaka, na limetamkwa wazi katika kifungu cha 148(6,7) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyofanyiwa marekebisho 2002.

“Kama nyumba ya mshitakiwa ambayo hati yake bado inashikiliwa na mahakama, kwanini upande wa mashitaka una wasiwasi? Mei 28 mwaka huu, mshitakiwa kaachiliwa huru akakamatwa tena, akapelekwa huko wanapojua serikali, na nyaraka zote zilizotumika kumdhamini awali bado zipo mahakamani, sasa anataka kusema mahakama imeiba hizo nyaraka?

“Sisi tunaamini kitu kikihifadhiwa mahakamani, kinakuwa katika mikono salama, na kama upande wa mashitaka una wasiwasi, ulete ushahidi kama nyumba hiyo imeuzwa na ndiyo maana leo tumeomba hizo nyaraka zitumike kumdhamini mshitakiwa,” alidai Magafu.

Alidai kuwa, kama kweli serikali haina nia mbaya dhidi ya mashitakiwa, nyaraka hizo zitumike kumdhamini mteja wake na mambo mengine yatafuatia, na wapo tayari kwenda kujibu ombi la mapitio Mahakama Kuu.

Magafu alidai kuwa, anachokiona kwenye kesi hii ni upande wa mashitaka kutumia mbinu za kuchelewesha kesi ili mshitakiwa aendelee kusota rumande.

“Sasa tunaanza kuhisi kuna kitu kwenye hii kesi…mbona hila zote zinafanywa na upande wa mashitaka katika kesi hii hii tu?” alihoji Magafu.

Akitoa uamuzi wake baada ya malumbano makali ya hoja za kisheria, Hakimu Mkazi Mwaseba alisema kuwa, mahakama inatakiwa ajiridhishe na nyaraka hizo ambazo zimewasilishwa na upande wa utetezi.

“Ili niweze kutoa dhamana kwa mshitakiwa, lazima nijiridhishe na hizi barua za wadhamini mlizoleta leo, hakuna polisi wa kuzihakiki, hivyo siwezi kutoa dhamana,” alisema na kuamuru mshitakiwa arudi rumande hadi Juni 15.

Uamuzi huo wa Mwaseba wa kumnyima dhamana Liyumba, ulisababisha ndugu na jamaa wa mshitakiwa waliokuwa wamekuja kuhudhuria kesi hiyo, kushikwa na simanzi na kuondoka kwenye chumba cha mahakama wakiwa wamejiinamia.

Ijumaa iliyopita, Mwaseba alilegeza masharti ya dhamana kwa Liyumba, ambapo sasa atatakiwa atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 300, wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh milioni 50 kila mmoja, kutotoka nje ya Dar es Salaam hadi kwa kibali maalum na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 2, 2009

No comments:

Powered by Blogger.