Header Ads

MAHAKAMA:MARANDA ANA KESI YA KUJIBU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imesema Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma Rajabu Maranda na mpwawe, Farijala Hussein, wanaokabiliwa na kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania, (BoT), wana kesi ya kujibu.


Uamuzi huo ambao ni wa kwanza kutolewa katika kesi za EPA zaidi ya saba zilizofunguliwa mahakamani hapo, ulitolewa jana na jopo la mahakimu wakazi watatu, Cypriana William, Saul Kinemela na Phocus Bampikya wa mahakama hiyo.

Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo hilo, Bampikya ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, alianza kusoma majumuisho ya ushahidi uliotolewa wiki iliyopita na kumalizia majumuisho ya ushahidi uliowasilishwa na Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface.

“Jopo hili baada ya kupitia kwa makini majumuisho ya pande hizo mbili katika kesi hii namba 1161/2008, kwa kauli moja limekubaliana na majumuisho ya ushahidi yaliyotolewa Ijumaa iliyopita na upande wa mashitaka, kwamba washitakiwa wana kesi ya kujibu,” alisema.

Baada ya kumaliza kusoma uamuzi huo, wakili wa utetezi, Majura Magafu, aliiomba mahakama itoe amri ya kupatiwa nakala ya uamuzi huo ili ajue hoja zilizotumiwa na mawakili wa upande wa mashitaka na kujipanga kwa utetezi.

Alidai kuwa, wanatarajia kuleta mashahidi kumi na washitakiwa wenyewe watatoa ushahidi, hivyo kufanya idadi ya mashahidi katika upande wa utetezi kuwa 12. Hata hivyo, alikataa kutaja majina ya mashahidi hao.

Mahakama ilikubali ombi la Magafu na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 24, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Juni 11,2009

No comments:

Powered by Blogger.