Header Ads

LIYUMBA KIZUNGUMKUTI

*Mahakama Kuu yatengua kumlegezea masharti
*Yatoa masharti mapya ya dhamana ya bil 110/-

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetengua uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wa kulegeza masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba.

Aidha, mahakama hiyo imetoa masharti mapya ya dhamana kwa Liyumba na kuutaka uongozi wa Mahakama ya Kisutu usimamie utekelezwaji wake badala ya jukumu hilo kuachiwa Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba kwa madai kuwa amepotosha matakwa ya kifungu 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Uamuzi huo ulitolewa jana saa tatu asubuhi na Jaji Geofrey Shaidi baada ya kusikiliza hoja za upande wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi uliowakilishwa na wakili kiongozi wa serikali, Justus Mulokozi na John Rwabuhanga pamoja na upande wa mjibu rufaa (Liyumba) uliowakilishwa na mawakili wa kujitegemea; Majura Magafu, Hudson Ndyusepo na Onesmo Kyauke.

Jaji Shaidi alisema ametengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu uliotolewa na hakimu mkazi Mwaseba ambaye alilegeza masharti ya dhamana dhidi ya Liyumba kwani uamuzi wa mahakama hiyo umepotosha matakwa ya kifungu hicho cha 148(5)(e) ya CPA mwaka 2002.

Alisema kifungu hicho kipo wazi na kinamtaka mshitakiwa kutoa fedha au nusu ya mali anayotuhumiwa kuiba.

“Mengi yamesemwa kuhusu kifungu hicho, pande zote mbili katika shauri hili wamekubaliana, na lugha iliyotumika katika kifungu hicho haina utata wowote, hivyo sina tatizo na tafsiri ya neno fedha.

“Nakubaliana na tafsiri ya neno fedha iliyotolewa na Mulokozi, ambaye tafsiri yake aliinukuu kutoka kwenye kifungu Na.5 cha Kanuni ya Adhabu inayosema fedha maana yake ni ‘warrants’, ‘funds’, ‘bank cheque’, ‘current notes or request of payment’.

“Naomba ieleweke wazi kwamba kifungu hicho hakijataja kosa lolote moja kwa moja, kwani kinatamka kuwa mtu anayeshitakiwa kwa kosa lililohusisha fedha au mali ambayo inazidi sh milioni 10, atalazimika kutoa fedha au nusu ya mali anayotuhumiwa kuiba.

Hivyo kifungu hiki kinapaswa kitumike kwenye kesi inayomkabili Liyumba,” alisema Jaji Shaidi.

Kuhusu hoja ya mawakili wa utetezi iliyokuwa ikiomba mahakama hiyo isikubaliane na matumuzi ya kifungu hicho, kwani kinatumika kwenye makosa ya wizi na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu, alisema:

“Kwa heshima na taadhima kabisa, sikubaliani na ombi hilo la mawakili wa utetezi, kwani halina msingi wowote kwenye macho ya sheria na endapo ningekubaliana nalo, nami ningekuwa natafsiri vibaya, na katika uelewa wangu shitaka linalomkabili Liyumba ni kusababisha hasara baada ya kuongeza kiwango cha fedha katika mradi wa ujenzi wa minara pacha bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa BoT, hivyo kusababisha hasara ya sh bilioni 221 mali ya BoT.”

Alisema kwa sababu hiyo kiwango kilichoipatia BoT hasara ni fedha na wala siyo makisio ya kifedha kama ilivyodaiwa na mawakili wa utetezi.

“Mwaseba alikosea kusema kifungu hicho cha 148(5)(e) cha CPA, hakiendani na makosa anayokabiliwa nayo mshitakiwa, na kwamba usemi huo kamwe haukubaliki kwenye macho ya sheria…na kifungu hiki bado ni kifungu halali cha sheria na kitaendelea kutumika kama kilivyo,” alisema Jaji Shaidi huku akionyesha kukerwa na uamuzi huo.

Akijibu hoja ya utetezi iliyodai kuwa kifungu hicho kinakwenda kinyume na katiba ya nchi inayotoa uhuru wa mtu binafsi kuwa huru, jaji huyo aliwataka mawakili hao wafuate utaratibu wa kuhoji sheria na kwamba katika rufaa hiyo si mahali pake.

“Nasisitiza kifungu hicho kipo wazi na ninaamuru kitumike ipasavyo kama nilivyotoa sababu hapo juu, hivyo nakubaliana na rufaa ya DPP na ninatengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kwani ulitafsiri vibaya matumizi na matakwa ya kifungu hicho.

“Ninaelekeza Mahakama ya Kisutu impatie dhamana Liyumba kwa kuzingatia masharti ya kifungu hicho, yaani atoe fedha taslimu au hati ya mali inayolingana na nusu anayotuhumiwa kusababisha hasara ambapo nusu itakuwa sh bilioni 110.

“Liyumba asalimishe hati ya kusafiria kwa Mkuu wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, asisafiri nje ya mkoa huu bila kibali cha mahakama. Utekelezaji huu ufanywe na Mahakama ya Kisutu na si Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba ambaye mahakama imemwona alitafsiri vibaya kifungu hicho,” alisema Jaji Shaidi.

Baada ya umuzi huo kutolewa, Magafu aliwasilisha ombi la kutaka kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, lakini jaji huyo alimjibu kwa mkato kwa kumtaka apeleke maombi hayo kwa njia ya maandishi.

“Mheshimiwa Jaji sisi tutakata rufaa haraka iwezekanavyo na tunaomba utusikilize maombi yetu haya kwa njia ya mdomo, kwani sheria inakutaka wewe jaji utusikilize kwa njia ya mdomo na tunaomba ombi hili uliweke kwenye rekodi zako,” alizungumza kwa jazba wakili Magafu.

Akijibu, Jaji Shaidi alisema: “Nipo tayari nendeni mkakate rufaa, lakini Magafu nimekwambia nendeni kisha mlete ombi lenu hilo kwa maandishi na si vinginevyo.”

Wiki iliyopita, Wakili Kiongozi wa Serikali, Mulokozi, aliiambia mahakama hiyo kuwa, DPP hakuridhishwa na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu na ndiyo maana wameamua kukata rufaa.

Aliongeza kuwa, rufaa yao ipo katika sehemu kuu mbili. Mosi, wanaamini Mwaseba alikosea kutoa dhamana bila kuzingatia kifungu hicho; pili hakimu huyo alipotosha matakwa ya kifungu hicho.

Huku akionyesha kujiamini, Mulokozi alianza kwa kuichambua sababu ya pili, kuwa shitaka linalomkabili mjibu rufaa ni kusababisha hasara na kwa mujibu wa maelezo ya kosa yanaonyesha kuwa makosa hayo aliyafanya akiwa ni mtumishi wa umma kwani alizidisha kiwango cha fedha za ujenzi wa minara pacha (Twin Towers) bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa BoT.

“Mtukufu Jaji, mradi wa ujenzi wa minara pacha, kiwango cha fedha kiliainishwa rasmi, lakini Liyumba akiwa mtumishi wa benki hiyo alikizidisha kiwango kingine cha fedha na kwa kitendo chake hicho mwenye mali ambaye ni BoT aliingia hasara ambayo ni fedha halisi, hivyo tunaomba kifungu hicho kitumike kuamua dhamana ya Liyumba,” alidai Mulokozi.

Aidha, alidai kuwa maana halisi ya kifungu cha 284(a)(6) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, inatamka wazi endapo mahakama inapomtia hatiani mshitakiwa, kwa kuanzia, mahakama hiyo itachukua fedha taslimu au hati ya nusu ya mali iliyowekwa na mshitakiwa kama dhamana.

“Kwa hiyo, kwa kifungu hicho cha 284(a)(6) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sisi tunasema kinasaidia utekelezaji wa masharti yanayotamkwa katika kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002.

“Hivyo, tunaomba Mahakama Kuu iingilie kati kutafsiri kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Makosa ya Jinai kisha itengue uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kwa sababu kifungu hicho ndicho kinapaswa kitumike kwenye dhamana ya mshitakiwa,” alidai Mulokozi.

Mei 28 mwaka huu, Mwaseba alitangaza kumwachia Liyumba kwa dhamana ya sh milioni 300 badala ya sh bilioni 110 kama ilivyotakiwa na kifungu hicho cha sheria, wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh milioni 50 kila mmoja, zuio la kutoka nje ya Dar es Salaam hadi kwa kibali maalum na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani.

Masharti hayo ni tofauti na yale ya awali, alipotakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao wangesaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya nusu ya kiasi cha sh bilioni 221, anachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara.

Hata hivyo, uamuzi wa kulegezewa masharti ya dhamana, ulimfanya Liyumba apumue, hasa pale Hakimu Mwaseba aliposema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kulazimika kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kwamba, ni kweli kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka mapya yanayomkabili mshitakiwa huyo.

Liyumba anakabiliwa na makosa mawili ya jinai katika kesi namba 105/2009 kwa matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006 akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Aidha, anadaiwa kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha kosa linaloangukia kwenye shitaka la kwanza.

Liyumba alisomewa mashitaka mapya baada ya Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, kuwaachia huru baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa ina makosa kisheria.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, walikamatwa tena na Liyumba kusomewa mashitaka mapya, na Kweka kuachiliwa huru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 16,2009

No comments:

Powered by Blogger.