Header Ads

SERIKALI YAWEWESEKA MGOMBEA BINAFSI

Na Happiness Katabazi

KWA mara ya pili, serikali imekata rufaa dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Democrat (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, katika Mahakama ya Rufani nchini, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ulioruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu.


Kwa mujibu wa rufaa hiyo namba 45 ya mwaka huu, inaonyesha serikali iliwasilisha rufaa hiyo, Ijumaa iliyopita mahakamani hapo ikipinga hukumu ya iliyotolewa na waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu, ambao ni Jaji Mstaafu Amir Manento, Salum Massati, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Thomas Mihayo (Mstaafu), ambao walikubaliana na ombi na Mtikila na kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi nchini.

Katika rufaa hiyo, serikali imetoa sababu sita za kukata rufaa hiyo zikiwemo; Mahakama Kuu ilikosea kujipa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ilikosea kutengua vifungu vya Katiba ya nchi, na kukosea kisheria kwa kupunguza matakwa ya lazima ya Ibara 30(5) na 13(2) ya Katiba ya nchi.

Sababu nyingine ni kujipachika mamlaka ya kibunge ya kutunga sheria, kukosea kisheria kwa kuiweka Katiba ya nchi katika vyombo vya kimataifa na pia ilikosea kuitolea maamuzi kesi hiyo bila kuweka suala hilo bayana.

Mara ya kwanza, serikali ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika Mahakama hiyo ya Rufaa mwaka 2007, ambapo ilidai mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kutafsiri Ibara ya 21(1)(c), 39(1)(c) (b) na 69(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupwa na Mahakama ya Rufaa baada ya kukubalina na ombi la wakili wa Mtikila, Richard Rweyongeza kwamba, rufaa hiyo haina msingi na kwamba imejaa dosari za kisheria.

Awali katika hukumu ya Mahakama Kuu uliotolewa Mei 2006, ililiruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, kwa sababu Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.

Mahakama Kuu ilibainisha kuwa Katiba inatamka wazi kuwa, kila mwananchi ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi na haiweki masharti kuwa hilo lifanyike kwa mtu kujiunga na chama fulani.

Mwaka 1993, Mtikila alishinda kesi kama hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, lakini licha ya uamuzi huo wa mahakama, Bunge lilishindwa kutunga sheria ya kuruhusu mgombea binafsi hivyo alifungua kesi hiyo ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kushinda tena.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Julai mosi, 2009

No comments:

Powered by Blogger.