Header Ads

TUWE MAKINI MBINU CHAFU ZA UCHAGUZI MKUU ZIMEISHAANZA

Na Happiness Katabazi

WATANZANIA wenzangu kaeni mkao wa kula, msimu wa uchaguzi (mavuno) umewadia, hilo ndilo ambalo naweza kulisema kuhusu pilikapilika na hekaheka za maandalizi ya wagombea uenyekiti wa serikali za mitaa na vijiji, udiwani, ubunge na urais.

Mara nyingi, wananchi tumekuwa hatupo makini katika kuchagua viongozi kwa kuwa tunauona uchaguzi kama sehemu ya kuvuna fedha kutoka kwa wagombea.

Lakini tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameshabainisha kuwa, serikali imeandaa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ili kuondoa vifungu vinavyohalalisha takrima (rushwa).

Kauli hiyo ya Pinda inaonekana kukosa mashiko wa wagiga kura na wagombea kwa kuwa kila mmoja anajiona ana haki ya kutoa au kupokea takrima.

Tayari huku mitaani hivi sasa zimeshaanza pilikapilika kabambe kwa wagombea watarajiwa kutoa hongo kwa namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufadhili timu za mipira ya miguu, kuanzisha mashindano na kutoa vikombe vinavyopachikwa majina yao, kutoa misaada kwa vikundi vya waathirika vya ukimwi na SACCOS.

Walengwa wakuu wa takrima hizo ni vijana na wanawake kwa kuwa wao ndio wanaonekana kuwa ni rahisi kurubuniwa na kupokea rushwa.

Si jambo la kushangaza hivi sasa wapanbe wa wagombea hao kuanza kubisha hodi misikitini na makanisani kwa lengo la kutoa misaada mbalimbali pamoja na kujenga nyumba hizo za ibada.

Katika kipindi hiki, wagombea watakuwa wacha-mungu zaidi pamoja na kutembelea maeneo mbalimbali ilimradi wawe karibu na wananchi kwa lengo la kuwapumbaza.

Tunatakiwa tujiulize maswali magumu, fedha hizi wanazozigawa wapambe wa wagombea hao watarajiwa wamezipata wapi? Au kuna EPA mpya ambayo hatujaigundua?

Sina shaka kuwa kuna uhusiano wa karibu wa wingi huo wa fedha hizo zinazoanza kutapanywa na kupungua kwa mapato ya serikali yanayokusanywa na TRA.

Sababu zinazotolewa za kuyumba kwa uchumi kuwa ndiyo kiini cha kupungua kwa mapato ya nchi, yaweza kuwa kiini macho. Wakati ukifika tutabaini hilo.

Lakini pia tutupie macho yetu kwenye eneo ambalo limekuwa likilindwa na serikali kwa usiri mkubwa, yaani mikataba ya uwekezaji na tenda za manunuzi ya umma.

Naamini kwamba ufisadi katika maeneo haya haujaguswa kana kwamba haupo, lakini najua mabilioni ya serikali hulipwa kila mara kwa mikataba isiyo na tija kwa taifa, kuna kandarasi na tenda za manunuzi ya umma zinazosukwa kwa madhumuni ya kuiba mabilioni ya fedha za umma.

Miradi mingi inayofanywa hivi sasa na serikali inakuwa na mazingira ya watu kunufaika zaidi (ufisadi), ujenzi wa barabara, utengenezaji wa vitambulisho vya uraia vimetengewa fedha nyingi, lakini ukija kuangalia gharama halisi unaweza kuzimia.

Wakati mwingine ufisadi huu wa kuibia umma ufanyika mchana kweupe, kwani barabara zinazojengwa huharibika kabla ya kipindi kifupi tu baada ya kuanza kutumika.

Kwa nini jamii isiamini kwamba baadhi ya wanasiasa na watendaji serikalini wameshajichotea mabilioni ya fedha kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwakani?

Kuna tatizo gani katika kufuatilia mambo hayo? Mbona tuna vyombo vya usalama vingi? Idara ya Usalama wa Taifa inayoongozwa na kiongozi shupavu, Rashid Othman ipo, TAKUKURU chini ya Dk. Edward Hosea ipo. Je, hawajatambua maovu hayo?

Nina uhakika itakapofika mwaka 2011 zitaibuliwa kashfa za watu waliojichotea fedha za wananchi na kuzitumia katika uchaguzi.

Binafsi sijaona tija yoyote ya fedha zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, maarufu kama ‘mabilioni ya JK’, kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali. Pia nina shaka hata hizo sh trilioni 1.5 zilizotengwa kwa ajili ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi, zinaweza ziende ninakotarajia.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo, walishawahi kuliambia taifa kuwa nchi yetu haitaathirika na mtikisiko wa uchumi, lakini sasa ni tofauti je, nani aaminike?

Najua hakuna atakayeweza kuzuia fedha zilizotengwa na Rais Kikwete kwa ajili ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi zisitumike vibaya, wadadisi wa mambo wanaona fedha hizo zimewekwa kwa ajili ya uchaguzi, hasa kwa chama tawala ili waseme wameshinda kwa kishindo.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Julai 28,2009

No comments:

Powered by Blogger.