Header Ads

NANI MWEKEZAJI HALALI TRL?

Na Happiness Katabazi

NADHARIA ya kubinafsisha ni pana.Inajumuisha dhana ya kuuza mali ya walipa kodi kwa mtu binafsi ili mtu huyo aendeshe huduma hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na umma kwa ubora na ufanisi zaidi.


Mauzo kama hayo yanatakiwa yazingatie uwezo wa mtu kununua rasilimali inayouzwa kwa bei ya hali ya soko kwa mtindo ama wa shindani kitenda au kwa mtindo wa upendeleo kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo ya umma.

Ama kwa mtindo wa upendeleo wa wazawa kwa vile siyo halali kumshindanisha mzawa na mgeni katika mazingira ya kitenda.

Nadharia hii ya ubinafsishaji inahusu pia ukodishaji wa rasilimali za umma kwa mwendeshaji binafsi pale ambapo rasilimali husika haifai kuuzwa kwa mtu binafsi kwa maslahi ya taifa ama rasilimali hiyo ni kubwa mno kiasi kwamba mwekezaji hawezi kupata mtaji wa kutosha kununua rasilimali hiyo.

Kwa ujumla nadharia ya ubinafsishaji inaiondoa dola katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi ili dola izingatie wajibu wake wa utawala, ulinzi na usalama wa taifa.

Tulipoamua kubinafsisha miundombinu yetu na hasa shirika la ndege ilitubidi kuzingatia misingi hiyo niliyoitaja.

Kwa kuwa Kampuni yetu ya reli(TRL) ndiyo chombo mwafaka cha uchukuzi wa bidhaa na abiria chenye usalama na chenye uwezo wa kusafirisha binadamu na bidhaa kwa wingi, mataifa yaliyomengi hayapendelei kubinafsisha muundombinu huo.

Hivyo mtindo wa kukodisha reli kwa waendeshaji binafsi umekuwa ukitumika nchini Ujerumani,Swedeni,Uingereza,Marekani.Mtindo huo umetumika kwa ufanisi mkubwa.

Lakini ieleweke kwamba bado dola katika nchi hizo halijajiondoa kwenye wajibu wa kufanya reli za kisasa zinazotumia umeme na kuvipa nguvu viwanda vikubwa vinavyotengeneza Injini na mabehewa ya kisasa ya uchukuzi wa bidhaa na abiria.

Hivyo siku hadi siku raia katika mataifa hayo wanakuwa wakitegemea zaidi reli kama chombo kikuu cha usafirishaji wa mizigo na binadamu.Treni za kisasa zenye mabehewa ya kisasa yanayompatia abiria burudani,starehe zinazofanya usafiri huu kushindana na usafiri wa anga yaani ndege.

Spidi ya treni hizi zinazoendeshwa kwa spidi ya ya umeme ni kati ya km 250 hadi 650 kwa saa.Hizo ndizo treni tunazoziona katika nchi hizo kupitia mitandao au Televisheni katika kila nchi ambayo ni makini katika sekta ya uchukuzi.

Tanzania haina sababu ya kugundua taili katika eneo hili la Sayansi na Teknolojia kwani tayari dunia imeshapiga hatua hizo za kimaendeleo.

Tunapo binafsisha mfumo wetu wa reli lazima tuzingatie kukabidhi mfumo kwa kampuni yenye uwezo wa Kisayansi,Teknolojia na mtaji ili kuweza kuendesha reli zetu kwa viwango vya juu.

Ni ajabu! badala ya hayo tuliyoyataja nchi yetu imechagua kampuni RITES ambayo kisayansi na teknolojia bado ipo kwenye enzi za ujima na kimtaji ni sifuri.

Tuambiwe kama Rais Jakaya Kikwete aliamua kujitengea sekta hiyo ya reli ndiyo chaguo lake la uwekezaji binafsi, atuambie kwani tunaona sasa mlipa kodi ametishwa mzigo wa kumlipia mishahara mwendeshaji maelezo yoyote na rais yupo kimya.

Sasa kama rais hana hisa katika mradi huu atueleze ni kwanini anamkumbatia mwekezaji wa sasa TRL?

Na hizo fedha serikali inazomkopesha kila mwezi anamkopesha kwa idhini ya nani na kwa maslahi ya nani?

Ni serikali hii hii inashindwa kuboresha mishahara watumishi wa umma hususani sekta ya afya , walimu na hata kuwapa mikopo ya uhakika wanafunzi wa elimu ya juu, kuweka dawa katika mahospitali yake lakini ina fedha za kumjaza huyu mwekezaji wa TRL.

Hivi tunajikomba nini kwa huyu mwekezaji au ni shemeji yetu kutoka India?

Tumechoka, serikali isijaribu kutulazimisha tuitukane.Serikali isitulazimishe tuwe wakorofi na waaasi. Serikali itekeleze wajibu wake wa kuongoza kwa kuzingatia misingi ya Utawala bora kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni.Katika hili la mwekezaji wa TRL tunaona kunanuka ufisadi mkubwa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Juni 7,2009

No comments:

Powered by Blogger.