Header Ads

TUHARAKISHE KUTENGANISHA BIASHARA NA SIASA

Na Happiness Katabazi

HIVI karibuni kundi la wananchi wa Kijiji cha Sing’isi, wilayani Arumeru walivamia shamba la Mbunge wa Vunjo mkoani Kilimanjaro, Aloyce Kimaro (CCM), na kuchoma moto nyumba 20 na mazao mbalimbali yaliyokuwamo.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Basilio Matei, uharibifu huo mpaka hivi sasa unakadiriwa kusababisha hasara ya kiasi cha sh milioni 500.

Kamanda Matei ameahidi kuwa uchunguzi wa kujua thamani halisi ya mali zilizoteketea unaendelea na kuna uwezekano wa hasara kuongezeka.

Wakati uchunguzi huo ukiendelea tayari watu 86 wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo na 38 wameshafikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka.

Naamini kuwa matukio ya namna hiyo yanayozidi kushamiri siku hadi siku ni matokeo ya mfumo wa kisiasa ulioparaganyika kiitikadi na kimaadili hapa nchini.

Kujinasibu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani na nje ya nchi kuwa ni watetezi wa wanyonge, wakati hawatendi hicho wanachokisema, ni moja ya mambo yanayowafanya watu wachoshwe na kuamua kufanya mambo ambayo ni kinyume cha sheria.

Kuwapo kwa sera nzuri na mipango ya serikali isiyo na utekelezaji pamoja na viongozi kuhubiri kile wasichokitenda, hubomoa daraja la mawasiliano baina yao na wananchi.

Wananchi huona viongozi wao kama wasaliti na wanyonyaji wa rasilimali zao kwa kujilimbikizia mali nyingi ilhali maisha ya wananchi yakizidi kuwa magumu kadiri siku zinavyosonga mbele.

Tujiulize, viongozi wa kujilimbikizia mali wameingia kwa utashi wa kuwahudumia wananchi au wajinufaishe kibiashara kupitia mwamvuli wa siasa?

Kuchanganya biashara na siasa ni mtego unaotakiwa kuteguliwa kwa uangalifu zaidi, kwa kuwa hata ikulu hivi sasa imekuwa ikitumika kwa manufaa ya viongozi, fulani wasiozingatia maadili ya viongozi wa umma.

Tunaweza kuendelea kama viongozi wataweza kujiepusha na mgongano wa kimasilahi kama ambavyo tunaona kila kukicha.

Inawezekana vipi rais mfanyabiashara akubali muswada wa kuibana biashara anayoifanya yeye au familia yake?

Tukifanikiwa kutofautisha na kutenganisha biashara na siasa tutaweza kuwadhibiti viongozi mbalimbali, kuanzia ngazi za chini mpaka juu kujihusisha na biashara na hapo tunaweza kurejesha angalau maadili ya viongozi wa umma.

Nimefarijika baada ya kumsikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani sheria hiyo itakuwa imeshaanza kufanya kazi.

Mifumo ya kiutendaji ndiyo inayowafanya wananchi kujiona ni wakimbizi katika ardhi yao, hatuna sababu za kuzidisha pengo kati ya walionacho na wasionacho ambalo mwisho wa siku ni vurugu miongoni mwa jamii.

Wananchi wanapenda viongozi wao washiriki katika shughuli za kilimo au nyingine za uzalishaji mali, lakini wasingependa kuona viongozi hao wanatumia madaraka yao kujineemesha.

Tusingependa nchi ikumbane na matatizo ya ardhi kama yale tunayoyaona Zimbabwe, Sudan na kwingineko.

Sina haja kuuhisha uvamizi wa Kimaro na itikadi za kisiasa, lakini ni vizuri dola ikaendesha jambo hilo bila kuingiza utashi wa kisiasa ili haki ipatikane.

Kimaro na kiongozi mwingine yeyote kwa hivi sasa hawazuiwi kufanya biashara, hivyo ni vema kwa wakati huu wakapatiwa ulinzi wa kisheria.

Mwisho, nimalizie kwa kuitaka serikali iliyo madarakani chini ya Chama Cha Mapinduzi iachane na utawala wa kiimla na mfumo wa kuwindana kama ule wa paka na panya.

Kama wataendelea na utaratibu huu, basi mbele ya safari hali itakuwa mbaya zaidi na tutabaini yupi ni panya na yupi ni paka.


Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Juni 21, 2009

No comments:

Powered by Blogger.