Header Ads

SERIKALI:MARANDA ANA KESI YA KUJIBU

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayomkabili Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma na wenzake, umejigamba kuwa wameweza kuthibitisha kesi hiyo, hivyo kuiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam iwaone wana kesi ya kujibu.


Akiwasilisha majumuisho ya ushahidi katika kesi hiyo jana, Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface ambaye alikuwa akisaidiana na Timon Vitalis, Frederick Manyanda, Ephery Cedrick na Michael Lwena, alidai upande wa mashitaka umedhibitisha kesi hiyo, hivyo washitakiwa wa na kila sababu kujibu kesi inayowakali.

Aidha, Bonifacena alieleza kusikitishwa na wakili wa utetezi, Majura Magafu aliyedai kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kudhibitisha kesi hiyo licha ya kutoa vielelezo 17.

Mbele ya Mahakimu Wakazi, Cypriana William, Saul Kinemela na Phocus Bampikya, Wakili huyo wa serikali alidai miongoni mwa vielelezo hivyo kuna vielezo vya washitakiwa wawili katika kesi hiyo (Maranda na Farijala Hussin) ambavyo vinaonyesha walitoa maelezo ya ungamo kwenye Kikosi kazi kilichoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza wizi huo.

“Maungamo hayo ni maneno yalitoka kwenye vinywa vya washitakiwa wenyewe na wala si kwenye vinywa vyetu wala vyenu…licha ya juzi Magafu kuyapinga maungamo hayo, lakini sisi tunasema hayo ni maungamo ya washitakiwa na yamekidhi kifungu cha 3 cha sheria ya ushahidi ya mwaka 2002,” alidai Wakili huyo.

Akichambua ungamo la Maranda, alidai ingawa mshitakiwa huyo alikana kutofahamu Farijala alitoa wqapi fomu hizo, hapo panahitajika kutumika ushahidi wa mazingira na kusema kuwa upande wa mashitaka unaamini nyaraka hizo zilitengenezwa na washitakiwa hao.

Akijibu hoja ya Wakili Magafu kwanini hakueleta shahidi toka kampuni ya MS/BC Cars Eport ya Mumbai India, ili idhibishe kuibiwa, alidai wakili huyo analiangalia suala hilo juu juu.

“Ukiangalia hati ya kuhamisha mali inaonyesha BC Cars Eport imeridhia kampuni ya Kiloloma & Brothers idai deni lake na ukiangalia chini ya hati hiyo umewekwa muhuri wa Kiloloma & Bro’s Enterprises na saini imewekwa na mtu wa kufirika (Chares Kissa), sasa huu ni mkorogo wa kughushi na tukumbuke tunapoitaja Kiloloma & Bros tunaona sura ya Farijala Hussein,” alidai na kusababisha watu kuangua vicheko.

Aidha, alidai kama washitakiwa walikuwa wameingia makubaliano na kampuni hiyo iweje Farijara atumie jina la kufikirika na kueleza kwa sababu hiyo hawakuona umuhimu wa kumuita mtu kutoka kampuni hiyo kutoa ushahidi mahakamani.

Akichambua shitaka la tano, la kuwasilisha hati za uongo, alidai wa shahidi toka BoT unaonyesha Maranda ndiye aliyekuwa akifika katika benki hiyo na kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa ambazo ni kilelezo cha 12 zilizokuwa zikionyesha anatakiwa alipwe deni kwaniaba ya kampuni hiyo ya nje.

Akipangua hoja ya Magafu kuwa hakuna mtu aliyetoka BoT kuja kulalamika kwamba waliibiwa fedha, alidai dosari ya majumuisho ya wakili huyo ni kwamba hakuangalia upande wa pili, kwani kuna nyaraka toka Benki Kuu ambazo zinaonyesha zilituma fedha kwenye kampuni ya washitakiwa na kwamba upande wa mashitaka haukuona haja ya kumleta Gavana kuja kudhibitisha wizi kwani nyaraka walizozitumia kujipatia fedha, kusajili jina la biashara ni za kughushi.

“Kwa hiyo tunaomba mahakama hii tukufu iwaone washitakiwa wanakesi ya kujibu kwani tunataka wapande kizimbani na kuleza bila kificho sh bilioni 1.8 waliipataje” alidai Boniface.

Aidha, alidai ungamo la Farijala linaonyesha yeye ndiye aliyejaza fomu ya kuomba kupatiwa jina la biashara la Kiloloma & Bro’s Enterprises na kwamba ndiye aliyepeleka fomu hiyo BRELA na kulipia ada ya usajili sh 6,000.

Wakili huyo wa Serikali alidai pia mshitakiwa huyo wakati anasajili kampuni hiyop alikiri kutumia jina la kufikirika la Chares Issac Kissa.

Akichambua shitaka la kwanza la kujipatia usajili kwa njia ya udanganyifu, Boniface alidai Farijara alipata usajili wa kampuni hiyo kwa udanganyifu, kwani alitumia jina la kufikirika.
Pia alieleza udanganyifu mwingine aliokiri kuufanya mshitakiwa huyo ni kudanyanya kuwa ofisi ya kampuni hiyo ipo nyumba Na. 7 Mtaa wa Iramba, Magomeni.

Sambamba na hayo, alieleza kuwa ushahidi wa mtaalam wa maandishi umebainisha kuwa fomu hiyo ilikuwa imejazwa na Farijala.

Baada ya kumaliza kuwalisha majumuisho hayo, Hakimu Cypiriana William alisema atatoa uamuzi wa suala hilo Jumatano ijayo iwapo washitakiwa wanakesi ya kujibu au la.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumamosi, Juni 6,2009

No comments:

Powered by Blogger.