Header Ads

SHAHIDI AUGUA GHAFLA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa kwanza Mary Kiwia ,katika kesi ya wizi wa Sh bilioni 6.3 wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania, inayowakabili mtu na mdogo wake Johnson Lukaza na Mwesigwa Lukaza jana alishindwa kupanda kizimbani kuanza kutoa ushahidi wake baada ya hali ya afya kubadilika ghafla akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.


Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface mbele ya Mahakimu wa Kazi wanaosilikiza kesi hiyo Prophir Lyimo,Emilius Mchauru na Edson Mkasimongwa alieleza mahakama kuwa kesi hiyo ya jinai namba 1156/2008, jana ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa na kuwa walileta shahidi mmoja ili aweze kuanza kutoa ushahidi wake.

“Lakini kwa bahati mbaya shahidi huyo ambaye amefika leo(jana) mahakamani hapa presha imepanda hivyo tunaomba tupewe muda ili tuweze kuwatafuta mashahidi wengine” alidai Boniface.

Hata hivyo Tanzania Daima katika uchunguzi wake imebaini shahidi huyo aliyepandisha presha wakati akisubiri kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake anaitwa Maria Kiwia mbaye ni Mwanasheria Kitaaluma.

Hata hivyo kiongozi wa jopo la mahakimu hao wakazi, Lyimo alisema wanakubalina na hoja ya wakili utetezi Alex Mgongolwa na Richard Rweyongeza kuwa jarada la kesi hiyo linadosari na kwamba dosari hizo haziwezi kufanyiwa marekebisho na mahakama ya Kisutu isipokuwa Mahakama Kuu hoja ambayo iliingwa mkono na Wakili Boniface ambaye aliiongeza kuwa jarada hilo lipelekwe mahakama hiyo ya juu lipewe maelekezo.

“Kwa hiyo kimsingi sisi jopo limebaini jarada lina dosari zinazotakiwa kutolewa maelekezo hivyo tunaamuru jarada la kesi hii lipelekwe Mahakama Kuu kwaajili ya maelekezo na naninaairisha kesi hii hadi Julai 8 mwaka huu.” alisema Prophir Lyimo.

Novemba mwaka jana , ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Novemba –Desemba 2007 washitakiwa hao walikula njama,kughushi hati ya kuamisha deni na kuibia sh 6,300,402,224.64 mali ya BoT, ambapo walighushi hati ya kuamishia mali iliyoonyesha kampuni yao ya Kernel Limited imepewa idhini ya kukusanya deni la kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Juni 9,2009

No comments:

Powered by Blogger.