Header Ads

DAWA ZA KULEVYA ZA SH.BIL 6.2/-ZAWAFIKISHA KORTINI

Na Happiness Katabazi

WATU wanne wakiwamo rai wawili wa Pakstan wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama na kusafirisha kilo 179 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.2.


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Biswalo Mganga, mbele ya Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Freddy Chonde na Kambi Zubery ambao ni Watanzania na Abdul Ghan Peer Bux na Shahbaz Malik ambao ni raia wa Pakstan.

Wakili Mganga alidai kuwa kwa wakati tofauti kati ya Januari mosi na Februari 21 mwaka huu, katika maeneo tofauti hapa Tanzania na nchini Pakistan, washitakiwa kwa pamoja walikula njama kutenda kosa la kuleta na kusafirisha dawa za kulevya nchini Tanzania.

Mganga alidai kuwa Februari 21, mwaka huu, maeneo ya Mtaa wa Jogoo, Mbezi Beach kwa pamoja washitakiwa wote waliingiza nchini dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 179,000 sawa na kilo 179 aina ya heroin zenye thamani hiyo.

Hakimu Augustina alisema kuwa washitakiwa hao hawapaswi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Mganga alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika. Hata hivyo, mawakili wanaowatetea washitakiwa hao wakiongozwa na Yassin Member, uliomba upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi haraka kwa kuwa watuhumiwa wamekamatwa hapa nchini.

Akijibu hoja hiyo, Mganga alidai kwamba watuhumiwa hao wamekamatwa juzi na kwamba shauri hilo linawahusisha raia wa kigeni, hivyo inawapasa wafanye upelelezi wa kina na kwa nafasi.

Hata hivyo, Hakimu Mmbando aliutaka upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi haraka na akaliahirisha shauri hilo hadi Machi 9, mwaka huu na siku hiyo litakuja kwa ajili ya kutajwa na akaamuru washitakiwa wote warudishwe rumande.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 24 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.