Header Ads

JWTZ WATOA BOTI KIGAMBONI

Na Happiness Katabazi

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limetoa boti zake mbili kwa ajili ya kusaidia usafiri katika kivuko cha Kigamboni.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Jeshi hilo iliyosambazwa jana mchana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa boti hizo za Kamandi ya Wanamaji-Kigamboni zinatoa msaada huo wa kuvusha abiria kutokana na kusitishwa kwa kivuko kikubwa (pantoni) kiitwacho MV Magogoni baada ya kupata hitilafu ambayo isingewezekana kuendelea na shughuli zake.

“Boti hizo mbili za JWTZ zimekuwa zikivusha abiria tangu Januari mosi mwaka huu kati ya Kigamboni na Magogoni na kutoka Magogoni kuelekea Kigamboni hadi pantoni ya mv Magogoni itakapokuwa tayari kwa kazi hiyo,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, ilisema kitendo cha JWTZ kutoa huduma au msaada kwa wananchi ni sehemu ya majukumu yake ya msingi ya kusaidia wananchi na mamlaka za kiraia pale yanapotokea matatizo au majanga yanayohusu jamii moja kwa moja.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa huduma hiyo ni moja ya huduma nyingi ambazo JWTZ lilishatoa na litaendelea kufanya hivyo wakati wote panapohitajika msaada wa dharura.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 3 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.