Header Ads

SHAHIDI AELEZA ALIVYOITILIA SHAKA DECI

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA meneja wa Benki ya Afrika(BOA) Tawi la Sinza, Godliving Maro ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa benki yake ilifikia uamuzi wa kuifunga ya akaunti ya washtakiwa ambao ndiyo walikuwa viongozi wa Taasisi ya Entrepreneurship for Community Initiative(DECI), kwasababu ilipokea amri ya kufanya hivyo toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Jackson Mtares, Dominic Kisendi, Timotheo ole Loitgimnye, Samuel Mtares, Arbogast Kipilimba na Samuel Mtalis, ambao wanadaiwa kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na sheria pamoja na kupokea amana za umma bila leseni.
Maro ambaye ni shahidi wa tano wa Jamhuri alikuwa akiongozwa na Wakili wa Serikali Prosper Mwangamila na Zuberi Mkakati kutoa ushahidi wake mbele ya hakimu Mkazi Stewart Sanga ambapo alidai kuwa majukumu yake katika benki hiyo ni kuakiki nyaraka za wateja walizozitumia kufungulia akaunti zinaendana na matakwa ya benki na pia kutazama nyendo za fedha zinazoingia na kutoka kwenye akaunti za wateja wao.

Maro alidai yeye akiwa na majukumu hayo mwaka 2009 alishiriki kuihakiki akaunti DECI na kubaini nyaraka walizozitumia kufungulia akaunti aziendani na ripoti ya fedha zilizokuwemo kwenye akaunti ya washtakiwa kwasababu awali washtakiwa waliwaeleza kuwa kampuni yao ya DECI ni Saccos na kuongeza kuwa anavyofahamu yeye SACCO inapaswa kuwa inatoa mikopo tu na si vinginevyo.

“Na hasa kilichoitufanya tuitilie shaka akaunti hiyo ni kuona dola 200,000 kuingizwa kwenye akaunti ya DECI ikabidi BOA iende kutembelea ofisi za taasisi hiyo ilipo Mabibo na tulipofika ofisini kwao kutaka kujua chanzo cha fedha hizo lakini washtakiwa hao hawakutueleza na benki haikuridhika ikabidi benki iwasilishe taarifa kwa Kitengo cha Usalama wa Fedha(FIU) ndani ya Wizara ya Fedha na Uchumi. ”alidai Maro.

Alieleza kuwa baada ya (FIU) kupokea taarifa hizo toka BOA, Wakurugenzi wa DECI, washatakiwa hao walifika katika benki yao kutaka wapatiwe fedha taslimu Sh bilioni moja na kwamba uongozi wa benki hiyo ulikataa kuwapatia licha fedha hizo zilikuwa ni mali ya washtakiwa.

Aidha baada ya muda siku chache kupitia benki ilipokea barua toka kwa kampuni ya uwakili ya Azania Law Chamber ambayo iliitaka benki hiyo iwapatie washtakiwa kiasi hicho cha fedha na kwamba benki ilikataa tena kutoa fedha taslimu na kuwataka washtakiwa iwapatie namba ya akaunti ili waweze kuwatumia fedha hizo.

“Washtakiwa hao hatimaye wakaleta namba ya akaunti inayomilikiwa na kanisa la Jesus Christ Delivers la Magomeni iliyopo kwenye Benki ya Dar es Salaam, na BOA ikawatumia zaidi ya Sh bilioni moja na zaidi ya Sh.milioni mia moja zilizokuwa zimesalia kwenye akaunti washtakiwa ,benki hiyo ilizipeleka kwenye akaunti inayoshukiwa na nia ya kufanya hivyo ni BOA kutaka kuifunga hiyo akaunti kwenye yetu na kusubiri maelekezo toka serikalini;

“Aprili 2009 nikiwa ofisini ilikuja barua toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa BOA na kuitaka benki yetu iifunge akaunti ya DECI ambayo ilikuwa na salio la zaidi ya sh.milioni 100” .alidai Maro.

Aidha alieleza mahakama kuwa anamfahamu mshtakiwa Tomotheo ole Olitiginye na Samwel Mtares kwasababu washtakiwa hao walifungua akaunti ya pamoja kwenye benki hiyo na katika upekuzi wake alibaini nayo ilikuwa na shaka katika nyaraka walizozitumia kufungulia akaunti na mtiriko wa fedha unaoingia kwenye akaunti hiyo na hivyo akalamizika kutoa taarifa kwenye Kitengo cha Usalama wa Fedha na mwisho wa siku Mwanasheria Mkuu pia alitoa amri kwa benki yao kuifunga pia akaunti hiyo.

Kuhusu mshtakiwa wa kwanza na wa pili Jackson Mtares na Domic Kigendi nao alidai kuwa aliwafahamu pia kwasababu walifungua akaunti ya pamoja katika benki hiyo na kwamba upekuzi wake ulibaini akaunti na nyaraka zilizotumiwa na washtakiwa kufungulia akaunti hiyo hazikuwa na matatizo yoyote ila kwasababu washtakiwa hao wote walikuwa wakihusika kwenye akaunti ya DECI ambayo ilishafungwa kwa maelekezo ya AG , Benki yao ikaamua kusitisha biashara na washtakiwa haoi na pia akaunti ikafungwa kwa amri ya mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Shahidi huyo akijibu swali aliloulizwa na mawakili wa utetezi Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo kwamba ni kwanini shahidi alivyokwenda kuikagua ofisi ya DECI na kukuta umati mkubwa nje ya ofisi ya DECI asitambue kuwa watu wale ndiyo waliokuwa chanzo cha fedha cha taasisi hiyo, Maro alijibu kuwa uwingi wa watu siyo kigezo cha fedha na kwamba wateja walipaswa wafungue mioyo yao na kuwaeleza kwa mapana chanzo cha fedha zao kuwa nyingi kwenye akaunti ile ya DECI.Shahidi wa sita anatarajiwa kupanda kizimbani leo kuanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 25 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.