Header Ads

MAWAKILI WA MINTANGA WAGEUKA MBOGO

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaji Shabani Mintanga, umeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuifuta kesi hiyo kwasababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta mashahidi.

Mawakili wa utetezi Majura Magafu, Jerome Msemwa na Yasin Memba mbele ya Jaji Agustino Mwarija jana waligeuka kuwa mbogo mahakamani hapo na kuomba kesi hiyo ifutwe kwani licha ya upande wa Jamhuri kushindwa kuleta mashahidi hao katika kesi hiyo ilianza rasmi kusikilizwa jana juzi pia imeonyesha aitilii umuhimu kesi hiyo.

“Jopo la mawakili wa utetezi kwa kauli moja tunaomba kesi hii ifutwe kwani upande wa Jamhuri haileti mashahidi licha ya mahakama hii imekuwa ikiwataka ifanye hivyo na miongoni mwa mashahidi wa Jamhuri ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olmpiki(TOC), Filbert Bayi na Mkurugenzi wa Michezo nchini, Leonard Thadeo wanaishi hapa jijini na tunawaona kila siku lakini cha ajabu upande wa Jamhuri unashindwa kuwaleta mashahidi hao kuja kutoa ushahidi mahakamani na matokeo yake mteja wetu anaendelea kusota rumande;

“Jumanne wiki hii kesi hii ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa rasmi lakini upande wa Jamhuri ukasema haujaja na shahidi na ukaomba upewe siku moja yaani Juzi ili waweze kuitumia siku hiyo kumpata shahidi ili waweze kumleta shahidi huyo leo(jana) aanza kutoa ushahidi lakini pia wanadai wameshindwa kumleta shahidi na hivyo mahakama hii haina budi kuairisha usikilizaji wa kesi hii na mteja wetu anarudi rumande kuendelea kusota…kwa sababu hizi sisi tunaomba kesi hii ifutwe” alidai wakili Jerome Msemwa.

Awali Wakili wa Serikali Zuberi Mkakati aliikumbusha mahakma kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya shahidi wa upande wao kuanza kutoa ushahidi lakini hilo halitaweza kufanyika kwasababu pia jana wameshindwa kuwapata mashahidi na kwamba hawana uhakika hati za wito wa mahakama wanazozitoa kama zinawafikia mashahidi hao na kuomba kesi hiyo iairishwe tena.

Kwa upande wake Jaji Mwarija alisema anatoa nafasi ya mwisho kwa upande wa Jamhuri kuleta mashahidi wao na akaiairisha kesi hiyo hadi kikao kijacho.

Mintanga alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, mwaka 2008 akikabiliwa na mashitaka ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi milioni 120 nchini Mauritius kupitia mabondia Emmilian Patrick, Petro Mtagwa na kocha Nasoro Michael na wengine watatu walipokwenda kushiriki mashindano ya ngumu ya pili ya Afrika nchini humo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 11 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.