NYARAKA ZA MENGI KUHUSU EPA,KAGODA ZAKATARIWA TENA KORTINI
Na Happiness Katabazi
KWA mara ya pili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi, lililotaka mahakama hiyo iwapatie nakala ya uamuzi iliyoutoa Ijumaa iliyopita ili aweze kwenda Mahakama Kuu kuomba ufanyiwe mapitio.
Mengi kupitia wakili wake Michael Ngaro, wanapinga kutupwa kwa nyaraka zinazohusu wizi wa fedha kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayoihusisha kampuni ya Kagoda ambazo Mengi anadai ina uhusiano na Manji.
Uamuzi wa kulitupa ombi hilo, ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana, ambaye alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili anakubaliana na hoja ya mawakili wa mlalamikaji (Manji), Mabere Marando, Dk. Ringo Tenga, Richard Rweyongeza na Beatus Malima, ambao walidai ombi lililowasilishwa na wakili wa mdaiwa Michael Ngaro na Deo Ringia, halina msingi wa kisheria.
Muda mfupi baada ya hakimu huyo kutoa uamuzi wa kukataa nyaraka za Mengi, zinazohusu EPA na Kagoda mawakili wake walieleza kutoridhishwa na uamuzi huo na kuomba wapatiwe nakala ya uamuzi ili waende kuiomba Mahakama Kuu iufanyie mapitio.
“Nataka ieleweke kwamba mahakama inaongozwa na kutenda kazi zake kwa mujibu wa sheria na hivyo basi mahakama hii inatupilia mbali ombi la mdaiwa (Mengi) lililotaka apatiwe nakala ya uamuzi wangu ili aweze kuomba upitiwe na Mahakama Kuu kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ambazo zimeandikwa Na. 25 ya mwaka 2002, inakataza upande wowote katika kesi yoyote kwenda mahakama ya juu kupinga amri za muda zinazotolewa na mahakama ya chini hadi kesi ya msingi itakapomalizika na kutolewa hukumu.
“Sababu hiyo ya kimsingi na kisheria niliyoitoa hapo juu ndiyo imenisukuma kulitupilia mbali ombi hilo la mdaiwa (Mengi) la kutaka kwenda kuiomba Mahakama Kuu iupitie uamuzi wangu nilioutoa Ijumaa iliyopita na kwa maana hiyo kesi hii itaendelea kusikilizwa katika mahakama hii ya Kisutu na hata sasa niko tayari kwa ajili ya kuanza kuisikiliza na imeamriwa hivyo na mahakama hii,” alisema Hakimu Mkazi Katemana kwa kujiamini.
Baada ya kumaliza kusoma uamuzi huo, Hakimu Katemana aliziuliza pande zote mbili kama ziko tayari kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo jana, lakini wakili wa Manji, Marando, alidai kuwa kwa jana hawakuwa tayari kwani mteja wao hakuwa amefika mahakamani na pia walikuwa wanafahamu kesi hiyo jana ingelikuja kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi huo, hivyo waliiomba ipangiwe tarehe nyingine.
Hakimu huyo aliahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo hadi Machi 14 na 15 mwaka huu.
Ijumaa iliyopita Hakimu Katemana alitoa uamuzi wa kuzikataa nyaraka 14 zikiwemo zinazoihusu kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd.
Mapema mwaka juzi, Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.
Ili kuthibitisha madai ya kumuita Manji Fisadi Papa, Mengi alitaka kuzitumia nyaraka za EPA na Kagoda, lakini mahakama ilikataa kuzitumia nyaraka hizo kutokana na madai yaliyotolewa na wakili Marando anayemtetea Manji.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Februali 16 mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment