Header Ads

WANAHABARI TUHESHIMU TAALUMA

Na Happiness Katabazi

BABA wa taifa Mwalimu Julias Nyerere aliwahi kusema kuwa “Ukweli una tabia moja nzuri sana ,achagui adui wala rafiki”.

Hivyo basi leo nimelazimika kutumia nukuu hiyo kwasababu mtazamo wangu utawahusu sana wanahabari wenzangu ambao naweza kusema ni familia moja na mimi na hivyo ni marafiki.
Februali 16 mwaka huu, Kambi ya 511 KJ ya Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam na kusababisha baadhi ya wananchi wenzetu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya na makazi yao kuharibika vibaya.

Binafsi natoa pole kwa wahanga waliokumbwa na janga hilo likiwemo Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi waTanzania (JWTZ), ambalo nalo nimiongoni mwa wahanga kwani wanapiganaji wetu wanne walijeruhiwa na nyumba mbili ziliabiwa.

Lakini kama ilivyoada kwa sisi watanzania wengi hasa baadhi ya wanahabari kupitia kalamu kila litokeapo jambo huwa hatukosi kuingiza hisia zetu badala ya kusubiri taarifa za wanataaluma husika wa matukio hayo.

Na hii ndiyo imeanza kuwa mila na desturi ya sisi wanahabari na baadhi ya wanasiasa wa hapa nchini kupenda kuhararisha vitu na kuwaaminisha wananchi baadhi ya taarifa huku tukijua wazi huku wakijua wazi hawana ushahidi wa jambo husika.

Ifike mahala sasa jamii ya watanzania tuje utamaduni wa kuheshimu taaluma za wanataaluma wengine naamini tukifanya hivyo tutakuwa tunaliondoa taifa kweny ugonjwa huu ambao uanaanza kulitafuna taifa la wananchi na wanahabari la kutoheshimu taarifa na kazi za wanataluma wengine.

Ijumaa iliyopita mimi nilikuwa ni miongoni mwa wanahabari tulioudhuria mkutano wa JWTZ ambao ndiyo ulikuwa mkutano wa kwanza wa jeshi hilo tangu milipuko hiyo .

Kwanza nikiri kwamba tangu nianze kazi hii ya uandishi wa habari kwa takribani miaka 12 sasa, sikuwahi kuudhulia mikutano inayohusisha wahariri na wakurugenzi wa vyombo vya habari lakini siku hiyo Mhariri wangu Mtendaji Absalom Kibanda alinituma nimwakirishe kwenye mkutano huo kwaniaba yake.

Kwanza napenda kumshukuru kwakunikabidhi majukumu hayo kwani ama kwa hakika fursa hiyo ilipa fursa ya kuthibitisha pasipo shaka kwamba kuna baadhi ya wahariri wanaotuongoza kwenye vyumba vya habari, uelewa wao wa kujua mambo ni mdogo wakati mwingine ukilinganisha na sisi waandishi wa habari wadogo.

Kwani kupitia baadhi ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa na mabosi wetu hao kuhusu tukio hilo yalikuwa yakidhiirisha wazi uwezo wetu wa kutanyambua na kufahamu majukumu yanayofanywa jeshi letu ni mdogo mno.Inasikitisha sana.

Kwani wakati mabosi wetu hao wakiuliza maswali hayo ambayo yalikuwa yakipanguliwa vyema kwa hoja za kutaaluma na Mkuu wa Usalama na Utambuzi Jeshi, Brigedia Jenerali Paul Meela na Mkuu wa Milipuko Jeshini,Brigedia Jenerali Leonard Mdeme hali iliyosababisha baadhi ya wanajeshi na wanausalama wa jeshi waliokuwa wamevalia nguo za kirai na mimi tukiwa tukiangua vicheko mara kwa mara.

Mfano mhariri anahoji ni kwanini JWTZ inapomaliza kufanya uchunguzi wake ni kwanini haitoi ripoti nzima kwa waandishi wa habari?Hivi katika akili ya kawaida tu na haitaji uwe ni mwanajeshi au wazazi wako ni wanajeshi, jeshi linaweza kutoa kutoa ripoti yake ya uchunguzi kwa ikaitapanya kwenye vyombo vya habari.

Ndiyo JWTZ yenye inasema uchunguzi ukikamilika utatoa taarifa.Sisi wanahabari tunaitaka hiyo ripoti ya uchunguzi tuipeleke wapi,Je kwa maadui wa nchi yetu kesho na kesho kutwa waje kutudhuru?

Mwanahabari anauliza swali kwamba ana taarifa kwamba wananchi tayari wamepoteza imani na jeshi lao kutokana na milipuko hiyo? Na wakati mwanahabari huyo anauliza swali hiyo mkononi hana hata ushahidi wa majina hata walau matano ya wananchi ambao wamekosa imani na jeshi hilo.
Na ndiyo maana nimeshindwa kuficha hisia zangu kwani makamanda wale wa JWTZ,Meela na Mdeme waliweza kuyapangua maswali ya wanahabari napia mara kwa mara Brigedia Mdeme alilazimika kuwaingiza katika darasa la milipuko na Meela kulazimika kuwaingiza kwenye darasa la sheria wahariri hao ambao aliwaambia JWZT huwa hawajiudhuru na kuwataka wakaisome Sheria ya Usalama na Ulinzi ya mwaka 1964.

Tumekuwa wepesi mno kutaka kupatiwa ripoti hiyo ya uchunguzi lakini mbona sisi wananchi tunakuwa wagumu sana kudai tupatie maamuzi yanayifikiwa kwenye baraza la mawaziri ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa ni siri?Na huko ndiko wakati mwingine yanapitishwa maamuzi ambayo yametekelezwa mwisho wa siku yamekuja kuligharimu taifa.

Inawezekana hili linasababishwa na sisi wanahabari kutotaka kubobea kwenye eneo Fulani la kuandika habari za aina fulani(specialization),makusudi, kutotaka kujifunza, ujinga,kununuliwa au ni umaamua wetu?

Na tatizo hilo la kukosekana kwa specialization ndiyo kunakosababisha sasa baadhi ya wahariri ambao hata mlango wa mahakama haujui au kesi zinaendeshwaje kuishia kuzipotosha habari za mahakama pindi wanapozihariri,hujikuta wanaweza hisia zao ambazo habari za mahakama ni mwiko kuweka hisia zao, kinachitakiwa kuandika kile kilichosemwa mahakamani.

Nafahamu kuwa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inatoa huru kwa wananchi wa kutoa maoni yao. Lakini Hata mwalimu Nyerere alishawahi kusema ‘uhuru bila mipaka ni sawa na wendawazimu”.Na msemo huu rafiki yangu kipenzi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam,(ACP), Abdallah Zombe ninpokutana naye katika mazungumzo yetu amekekuwa akinukuu nukuu hiyo ya Nyerere akisema kuwa hivi sasa huu uhuru wa kutoa maoni hivi sasa ambao inaonekana hauna mipaka sasa kwani unaingilia hadi taaluma za watu ni hatari kwa mustakabali kwa taifa.

Sote ni mashahidi kwa jinsi ya baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwa vikiripoti kesi ya Zombe na kabla ya kufikishwa mahakamani kwa hisia zao badala ya kuripoti kile kilichokuwa kikisemwa mahakamani.Na matokeo yake akaja kushinda kesi na yeye akafikia uamuzi wa kuyashtaki magazeti hayo ikiwemo gazeti letu.

Wanahabari hivi sasa ndiyo kimbilio kubwa la wananchi na hivi sasa wanahabari ndiyo wamekuwa wakipata habari nyingi sana tena kwa haraka ukilinganisha na miaka iliyopita.Kwahiyo nasisi wanahabari tubadilike.

Hivyo basi nimalizie kwa kuwaasa wanaandishi wenzangu,wanasiasa na wananchi wa kada nyingine tuheshimu taaluma za watu pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwani leo hii tunaenda maofisi na kurudi nyumbani salama na kukaa kwenye mabaa na kulewa pombe ni kwasababu kuna baadhi ya wanajeshi JWTZ, Idara ya USalama wa Taifa,Polisi wanakesha kwa kutumia mbinu walizofunzwa mafunzoni kuakikisha taifa letu na wananchi wake wanaishi salama.

Na ieleweke kwamba kulinda usalama wa taifa na mali zake ni taaluma za watu, serikali ilipeleka askari wetu JWTZ chini ya Jenerali Mwamunyange huko Mafinga ,Mafinga nayo Idara ya Usalama wa Taifa chini ya Rashid Othman inapeleka askari wake kuhenya kwenye chuo chake Mbweni na Jeshi la Polisi chini ya IGP-Said Mwema linapeleka askari wake kuhenya Kule CCP-Moshi.

Hivyo tunapaswa tuheshimu kazi zao na pindi wanapolitaka taifa liwe nasubira kwani bado wanafanyia uchunguzi jambo Fulani ,tusiwaharikishe kwani wengine ni maamuma katika fani hiyo ya uskari.

Ikumbukwe kwamba taifa la wananchi na viongozi wanaishi na kuaminishwa umbeya, chuki, na uongo ambao umekuwa ukiandikwa kwenye vyombo vyetu vya habari na baadhi ya waandishi wasiyo na maadili ,kamwe hilo siyo taifa thabiti.

Nalisema hili kwa uchungu sana kwani hivi sasa taifa letu ndiyo linaelekea huko kwani wananchi wengi huko mitaani na maofisini wamekuwa wakiamini sana habari ambazo tumekuwa tukiziandika kumbe wakati mwingine sisi waandishi tumekuwa tukiandika habari hizo bila kuwa na ushahidi wa kutosha, hisia zetu kuliko uhalisia wa jambo husika na mwisho wa siku aliyeandikwa hivyo kwa kupakaziwa uenekana ni mtu mchafu kwa jamii kumbe si kweli.

Sisi wanahabari tusilifikishe taifa huko,kwani mwisho wa siku hata watoto wetu watakuwa ni waathirika wa dhambi hiyo ya uzushi na umbeya.Tanzania ni nchi yetu na JWTZ itabaki kuwa ni chombo chetu ambaItaliccho kimeanzishwa kwamujibu wa Sheria Na. 24 ya Ulinzi na Usalama ya mwaka 1964.Tumekikabidhi jukumu la kulinda mipaka ya nchi yetu na ndiyo Jeshi la Tanzania.

Hivyo katika hili la milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto ni vyema na haki tukalipa nafasi ya kufanyakazi yake chini ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi hilo Jenerali Davis Mwamunyange.

Tuache hisia (speculation) katika jambo hili na katika masuala mengine ya taaluma za watu ambazo sisi hatujazisomea kama walivyotutaka Mabrigedia Jenerali Paul Meela na Leonard Mdeme kwani kufanya hivyo ni wazi tutapandikiza chuki mbaya kwa wananchi na jeshi lao pamoja serikali.Na sisitiza kwamba tuheshimuwa taaluma watu wengine na tuachane na maneno ya kusikia, tusimame kwenye maadili ya taaluma yetu ya uandishi naamini tutakuwa tulijenga taifa letu.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika.
0716-774494.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februali 22 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.