Header Ads

MHASIBU MAHAKAMA KUU KORTINI KWA WIZI

Na Happiness Katabazi

MHASIBU Msaidizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi, Raymond Mazale, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na kosa la wizi wa sh milioni 22 mali ya mwajiri wake.

Wakili wa Serikali Beatrice Mpangala mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam, Aloyce Katemana, alieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka manne ya wizi.

Alisema mshtakiwa anatuhumiwa kufanya udanganyifu wa stakabadhi za serikali na kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa nyakati tofauti.

Mpangala alidai kuwa kati ya Machi 4, 2009 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa ni mhasibu msaidizi wa mahakama hiyo kwa njia ya udanganyifu alitumia stakabadhi za malipo ya serikali Na.3359401 hadi 33659600.
Hata hivyo Mpangala alisema kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo na Hakimu Mkazi Katemana alisema makosa hayo kwa mujibu wa sheria yana dhaminika na kusema ili mshtakiwa apate dhamana atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 11.08, wadhamini wawili ambao kila mmoja atatoa hati ya mali yenye thamani ya sh milioni tano.

Hata hivyo mshtakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo na kupelekwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Februari 12.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februali 5 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.