Header Ads

TAKUKURU NI MAAMUMA WA SHERIA?

Na Happiness Katabazi

HUENDA ule utabiri ‘bubu’ uliokuwa ukitolewa na baadhi ya wananchi kwamba zile kesi za rushwa zilizokufunguliwa ‘chapuchapu’ kwa mbwembwe na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) dhidi ya baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM )katika kura za maoni mwaka 2010 ni kiini macho.


Sote bado tunakumbuka kwamba miongoni mwa Wana CCM walioburuzwa mahakamani na Takukuru kwa kudaiwa kutoa rushwa ili majina yao yapitishwe kwenye uchaguzi wa ndani ya chama chao ni aliyekuwa waziri na mbunge wa muda mrefu, Joseph Mungai na Katibu Mkuu wa (TFF), mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fredrick Mwakalebela.

Awali Wakili wa Takukuru, Imani Mizizi, mbele ya Hakimu Mkazi, Festo Lwiza wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, alidai Juni 20 mwaka jana, Mwakalebela alitoa hongo ya sh 100,000 kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoga, Hamis Luhanga, ili awagaie wajumbe 30 wa CCM, walioitwa kwenye kikao hicho cha kujipanga kupiga kura za maoni.

Mwanasheria alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa kinyume cha Sheria ya Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007, kifungu cha 15(1),(b),kinachosomeka pamoja na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010, kifungu cha 21(1),(a) na kifungu cha 24(8).

Hivi karibuni tumeisikia Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa kwa wakati tofauti ikitoa amri ya kuwafutia kesi washitakiwa kwa maelezo kwamba hati za mashitaka zimeonekana kuwa na dosari za kisheria. Hati hizo ziliandaliwa na mawakili wa taasisi hiyo.

Washitakiwa walishitakiwa kwa kutumia sheria mbili tofauti kwenye hati moja ya mashitaka, kitu ambacho ni kinyume cha sheria na kinaweza kusababisha washitakiwa washindwe kuandaa utetezi wao.

Kwa muktadha huo hapo juu, sasa tunaweza kuona ule utabiri umetimia, kwani hata wahenga walisema: “Lisemwalo lipo na kama halipo lina kuja.”

Na kwa washitakiwa hao wawili kuachiliwa na mahakama ni wazi msemo huo wa wahenga umetimia.

Takukuru ndiyo chombo chetu ambacho moja ya majukumu tuliyowakabidhi ni kuchunguza, kuzuia na kupambana na rushwa na hivi sasa kina mawakili wake ambao hufika mahakamani kuendesha kesi zinazohusiana na rushwa.

Na Watanzania ndio tumeridhia tuwe na chombo hicho kwa kuhakikisha taifa letu linamtokomeza mdudu rushwa kwasababu ni adui wa haki.

Hivyo, kitendo cha baadhi ya mawakili wa Takukuru walioshiriki kuandaa hati hizo mbili za mashitaka dhidi ya Mungai na Mwakalebela na kubainika hati hizo zimeandaliwa ovyo, ndiko kumenisukuma kuandika mtazamo huu na kuinyoshea kidole taasisi hiyo.

Kisheria upande wa Jamhuri wanaruhusiwa muda wowote kuzifanyia mabadiliko hati zao za mashitaka pindi inapobainika kisheria.

Watanzania tujiulize, hivi umakini wa wanasheria wa Takukuru katika mashauri hayo uko wapi?
Haiingii akilini kabisa, Rais Jakaya Kikwete ambaye alisaini kwa haraka Sheria ya Gharama za Uchaguzi 2010 na kuiagiza taasisi hiyo iwashughulikie bila aibu wanasiasa wote hata wa CCM wanaotoa rushwa kwenye uchaguzi, halafu hawa mawakili wa taasisi hiyo washindwe kuwa makini katika kuandaa hati za mashitaka na mwisho wa siku watuhumiwa wanaachiwa na mahakama!

Tujiulize, mawakili hao ni ‘maamuma’ na ‘mbumbumbu’ wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010?

Au taasisi hiyo iliamua kuwafungulia kesi hizo ili kumuhadaa Rais Kikwete kwamba ile sheria aliyoisaini pale Ikulu ndiyo imeanza kutumika, huku mawakili wa taasisi hiyo wakiwa wameandaa madudu katika hati hizo za mashitaka?

Kwa hiyo wananchi tumtegemee tena kumsikia Ofisa Uhusiano wa Takukuru, wiki hii kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kwamba licha mahakama kumwachia Mwakalebela, taasisi yake itamshitaki tena, kwani tungali tukikumbuka kwamba hata alipoachiwa Mungai ofisa habari huyo alisema maneno hayo ambayo kwa watu wenye akili timamu kama sisi na tunajua kinachoendelea, tunaishia kupata kichefuchefu na hasira.

Vyovyote iwavyo, ninapenda kuwaasa hasa mawakili wa serikali hususan nyie mawakili na wachunguzi wa Takukuru, tumieni taaluma zenu vizuri na kwa haki, kwa masilahi ya taifa letu na si kwa lengo la kuwafurahisha baadhi ya wanasiasa wenye hulka za kinyang’au au watu wenye nguvu ya fedha na madaraka kuwaumiza wananchi ambao wana ugomvi wao binafsi.

Kumbukeni vyeo na taaluma mlizonazo ni dhamana, kwa hiyo baadhi yenu kwa makusudi mnavyoamua kutumia vyeo au taaluma zenu kuwaumiza wananchi, ipo siku Mungu atawalipa mshahara wa dhambi.

Nasema haya kwa uchungu, kwani nina miaka 12 sasa ya kuripoti habari za mahakamani, nimeshuhudia na ninaendelea kujifunza mambo mengi, kwamba kuna baadhi ya wananchi wenzetu wanafikishwa mahakamani kwa kubambikiwa kesi, ingawa kuna wanaofikishwa kihalali.

Kwa mtazamo wangu, ni vema mawakili wa Takukuru kuwa makini katika uandaaji wa hati za mashitaka na uendeshaji wa kesi zake, kwani kubainika kwa hati hizo mbili kuwa na dosari ni wazi kunachangia kuporomosha heshima ya taasisi hiyo na ndugu wa washitakiwa wataanza kujenga chuki dhidi ya taasisi hiyo na serikali yetu. Hatutaki tufike huko.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.

0716- 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi Mosi mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.