Header Ads

KESI YA MPENDAZOE,MAHANGA HAKIELEWEKI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Machi 8 mwaka huu itatoa uamuzi wa kulikubali au kulikataa ombi la aliyekuwa mgombea Ubunge wa Segerea, Fred Mpendazoe (Chadema) la kutaka aruhusiwe kuweka sh milioni 15 mahakamani kama dhamana.

Dhamana hiyo ni sh milioni tano kwa kila mdaiwa ambapo wadaiwa katika kesi hiyo ni Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Dk. Makongoro Mahanga (CCM), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi anazotakiwa kuzitoa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2002.

Katika kesi ya msingi Mpendazoe anapinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 jimbo la Segerea yaliyomtangaza Dk. Mahanga kuwa mbunge.

Baada ya Jaji Profesa Ibrahimu Juma kusikiliza ombi la mlalamikaji na pingazimi la mawakili wa wadaiwa lililotaka ombi hilo litupwe, amesema atatoa uamuzi wa ama kukubali au kukataa ombi la Mpendazoe Machi 8.

Awali Wakili wa mlalamikaji Peter Kibatala aliiambia Mahakama kuwa wamekuja na ombi jipya la kuomba mteja wake aruhusiwe kuweka kiasi hicho cha fedha kwani tayari mteja amepata kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo wakili wa wadaiwa hao Jerome Msemwa alilipinga ombi hilo na kuiomba Mahakama isimruhusu hadi pale mlalamikaji atakapopeleka ombi rasmi mahakamani la kuiomba impangie kiwango cha kuweka mahakamani hapo.

Wakili Msemwa aliongeza kuwa kifungu cha 111(3) cha Sheria ya Uchaguzi kinamtaka mwombaji anayeiomba mahakama imsamehe kulipa dhamana hiyo au kumpunguzia kiwango cha kulipa, anatakiwa awasilishe ombi hilo ndani ya siku 14 tangu alipofungua kesi ya msingi ya kupinga matokeo ya Ubunge.

Akipangua hoja hiyo wakili wa Mpendazoe, Kibatala aliambia kuwa kifungu hicho kilichotumiwa na Msemwa hakiendani na ombi lao waliloliwasilisha kwa kuwa ombi lao ni Mahakama imruhusu aweke kiasi hicho cha fedha na si vinginevyo.

Februali 15 mwaka huu, Jaji Juma alitupilia mbali ombi la Mpendazoe la kuitaka Mahakama hiyo imsamehe kulipa fedha hizo kwa sababu hana uwezo wa kupata fedha hizo na kwamba amebaini hati ya kiapo cha maombi hayo kina dosari za kisheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi Mosi mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.