MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imevikataa  vielelezo vya utetezi vilivyowasilishwa na Mwenyekiti wa Makampuni ya  IPP Ltd, Reginald Mengi, katika kesi aliyofunguliwa na mfanyabiashara  Yusuf Manji.
   Uamuzi wa kuvikataa vielelezo hivyo vinavyojumuisha nyaraka 14  zikiwamo zinazoihusu kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd ulitolewa  mahakamani hapo jana na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana.
   Katika kesi hiyo, Manji anamlalamikia Mengi kwa madai ya kumkashfu akimdai fidia ya shilingi moja kwa kumuita fisadi papa.
   Hakimu Katemana alisema amefikia uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja  za kisheria zilizowasilishwa mbele yake na pande zote mbili  kwa siku  mbili tofauti.
   Akisoma uamuzi wake huo,  alisema anakubaliana na hoja za kisheria  zilizowasilishwa awali na jopo la  mawakili wa mlalamikaji  ambao  wanaongozwa na Mabere Marando, Richard Rweyongeza, Dk. Ringo Tenga na  Beatus Malima kwamba mahakama hiyo itupilie mbali maombi ya mdaiwa  (Mengi) ya kutaka nyaraka hizo zikiwemo nyaraka vivuli ambazo  zinaonyesha ni mali ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (TAKUKURU), ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mkataba baina  kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd na Quality Finance  Corporation Ltd.
   “Kwa kauli moja mahakama hii inatupilia mbali ombi la mdaiwa (Mengi)  kwa sababu nyaraka hizo anazotaka kuzitumia kutolea ushahidi hazihusiani   na kesi hii kabisa, na pia nyaraka hizo ni vivuli.”
   Baada ya Hakimu Katemana kumaliza kusoma uamuzi wake, Wakili wa mdaiwa  Michael Ngaro anayesaidiwa na Deo Lingia aliinuka kwenye kiti  alichokuwa ameketi na kuieleza mahakama kuwa uamuzi wa hakimu huyo  haukuwa wa kushtukiza.
   Wakili Ngaro alidai kuwa  kitendo cha hakimu huyo kuzikataa nyaraka  hizo ni wazi sasa kimesababisha mteja wake asizitumie nyaraka hizo kama  ushahidi wakati siku atakapoitwa na mahakama hiyo kujitetea na kwamba  wanaomba nakala ya uamuzi huo na ili kwenda kuupinga Mahakama Kuu  Kanda  ya Dar es Salaam.
   Hata hivyo hoja hiyo ya wakili Ngaro ya kutaka kwenda Mahakama Kuu  kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, ulipingwa vikali na mawakili wa  mlalamikaji ambao walimwomba Ngaro asiipotezee muda mahakama hiyo kwani  katika mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Bunge mwaka 2002 yanakataza  kuyakatia rufaa maamuzi madogo (ruling) yanayotolewa na mahakama za  chini kabla kesi ya msingi haijamalizika.
   Hata hivyo hoja hiyo ya mawakili wa Manji, ilimfanya wakili wa Mengi  kuwasilisha ombi jipya la kuiomba mahakama itumie busara zake kwani siku  itakapofika mteja wake kuja kujitetea atakosa nyaraka.
   Baada ya ombi hilo, Katemana aliahirisha shauri hilo hadi Februari 15 mwaka huu ambapo atatoa uamuzi.
   Mapema asubuhi jana wakili wa Mengi, alianza kujibu hoja za mawakili  wa mlalamikaji zilizowasilishwa mahakamani hapo Februali 4, mwaka huu,   aliomba nyaraka za mteja wake zipokelewe na pingamizi la Manji kutaka  nyaraka hizo zisipokelewe litupwe.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Februali 12 mwaka 2011.
 
No comments:
Post a Comment