Header Ads

MANJI,MENGI WAVUTANA MAHAKAMANI

• Kisa ni nyaraka za Kagoda
Na Happiness Katabazi

JOPO la mawakili wa kujitegemea wanaomtetea mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji (35), jana walipambana kwa kutumia hoja za kisheria ili kuishawishi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ikubaliane na pingamizi lao la kutaka nyaraka zilizowasilishwa na mdaiwa Reginald Mengi zisitumike katika kesi hiyo.

Jopo hilo lililosheheni mawakili wa kujitegemea maarufu linaloongozwa na Mabere Marando, Dk. Ringo Tenga, Sam Mapande, Richard Rweyongeza na Beatus Malima mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katema waliiambia mahakama kuwa juzi mawakili wa mdaiwa Mengi ambao ni Michael Ngaro na Deo Ringia, waliwapatia nyaraka hizo ambazo walidai Mengi atazitumia kujitetea wakati ukifika.

Sababu zilizotolewa na Marando kutaka nyaraka hizo zisitumike ni kwamba hazihusiani na kesi hiyo ambayo mteja wake Manji anataka Mengi amlipe fidia ya shilingi moja. Kwa mara nyingine tena jana Manji alifika mahakamani hapo.

Marando alisema sababu nyingine ambayo wanataka nyaraka hizo zilizoletwa na mawakili wa Mengi zitupwe na mahakama ni kwa sababu nyaraka hizo ni kivuli.

Kadhalika zinaonyesha ni mali ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ofisi ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (takukuru) na kwamba nyaraka hizo licha ya kuwa ni vivuli lakini pia hazionyeshi kama zimethibitishwa kisheria (certified copy).

“Sheria ya ushahidi ya mwaka 2002, inamtaka mtu alete nyaraka halisi mahakamani kama ushahidi na kama hana nyaraka halisi mdai au mdaiwa anaruhusiwa kuomba upande wa pili wa kesi hiyo umpatie nyaraka halisi ili aweze kuzitoa mahakamani kama ushahidi.
“Lakini hawa mawakili wa Mengi hawajatuomba nyaraka halisi hadi sasa na pia walitakiwa hizo nyaraka wazilete mapema mahakamani kabla ya kesi haijaanza kusikilizwa.

Marando pia alishangazwa na nyaraka hizo zinazoonyesha zimetolewa na ofisi ya AG na TAKUKURU kufikishwa mahakamani bila kibali cha mamlaka hizo wala kuonyesha kama alilipia ada ya kupata nyaraka hizo.

Akisoma moja ya nyaraka hizo ambayo ni mkataba ulioingiwa baina ya Kagoda Agriculture Ltd na Quality Group Finance Ltd, Marando alieleza kuwa mkataba huo uliiingiwa na makampuni hayo na si mteja wao (Manji) na kwamba wao ni mawakili wanaomtetea mlalamikaji binafsi na wala si mawakili wa makampuni yanayomilikiwa na mteja wao.

Katika hilo, wakili huyo wa Manji alimshauri Mengi kama anataka kutumia nyaraka ni vyema akafungua kesi nyingine dhidi ya makampuni ya Manji.

Hata hivyo ilipofika upande wa wakili wa Mengi, Ngaro, kujibu hoja hizo aliieleza mahakama kuwa hayuko kwenye nafasi nzuri ya kujibu hizo hoja hivyo kuomba muda wa kwenda kuwasiliana kwanza na mteja wake (Mengi) ambaye yuko safarini mkoani Arusha.

Ombi hilo la Ngaro lilikubaliwa na Hakimu Mkazi Katemana ambaye aliahirisha usikilizaji wa kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengu hadi Februali 11 mwaka huu.

Mapema mwaka juzi, Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashifu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februali 5 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.