Header Ads

MSHTAKIWA KESI YA SAMAKI ALIDANGANYA MAHAKAMA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imesema kwamba mshtakiwa 19 Jakson Sirytoya katika kesi ya Uvuvi haramu kwenye Ukanda wa Bahari ya Hindi maarufu ‘Kesi ya Samaki wa Magufuli’ ni muongo na ameidanganya mahakama hiyo.

Hayo yalisemwa na Jaji Radhia Sheikh jana wakati akitoa uamuzi wake katika kesi ndani ya kesi(Trial within a Trial) ambapo alisema anakubaliana na hoja za Wakili wa Serikali Mwandamizi Biswalo Mganga zilizoiomba mahakama hii itupilie mbali hoja za mawakili wa mshtakiwa huyo kwasababu ni za uongo.

Jaji Sheikh alisema amefikia uamuzi huo wa kutupilia mbali pingamizi la mawakili wa mshtakiwa huyo Ibrahimu Bendera na John Mapinduzi lilotaka mahakama hiyo isipokee ungamo la mshtakiwa huyo(Sirytoya) ambaye ni raia wa Kenya kwasababu mshtakiwa huyo tangu akamatwe hakuwahi kuchukuliwa maelezo ya ungamo na kwamba maelezo hayo ya ungamo yaliyotolewa na upande wa Jamhuri na kupokelewa kama utambulisho namba moja hakuyatoa kwa ridhaa yake kwani alitishwa na Inspekta Antony Mwita.

Alisema mahakama hiyo baada ya kuendesha kesi ndani ya kesi ilipata fursa ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande mbili na kusikiliza ushahidi wa Jamhuri, Inspekta Mwita ambaye ndiye aliyeandaa ungamo la mshtakiwa na pia ilisikiliza ushahidi wa shahidi wa utetezi ambaye ni mshtakiwa mwenyewe na mahakama hii ikabaini yafuatayo:

“Shahidi wa utetezi ambaye ndiye mshtakiwa wa kwanza Sirytoya alitoa maelezo ya uongo kwani wakati akitoa ushahidi wake alisema hajawahi kuhojiwa na polisi na mara akasema maelezo hayo ya ungamo aliyatoa si kwa ridhaa yake kwani alitishwa na mara akasema kwamba Inspekta Mwita alikuwa akimhoji kirafiki, na kwamba alikuwa hafamu kusoma na kuandika hata jina lake;

‘Lakini wakati siku Jamhuri inawasomea maelezo ya awali washtakiwa hao mahakamani ambapo maelezo hayo yaliandikwa kwa lugha ya Kiingereza, mshtakiwa huyo alipewa maelezo hayo ili aweze kusaini maelezo anayoyakubali na anayoyakataa na mshtakiwa huyo aliweza kulisoma jina lake na akaweka saini ;

“Pia mahakama ilitafakari sababu hizo mbili za mshtakiwa zilizotaka tusipokee ungamo hilo kama kielelezo kwasababu eti hajawahi kuungama na ungamo hilo hakulitoa kwa ridhaa yake……Nilijiuliza kama mshtakiwa huyu anadai hakuwa kuungama polisi hii hoja yake nyingine ya kwamba ungamo hilo hakulitoa kwa ridhaa yake kwani alitishwa na polisi inatoka wapi?

“Hivyo basi kwa maelezo hayo juu mahakama hii inatamka wazi kwamba mshtakiwa huyo alitoa ushahidi wa uongo katika kesi ndani ya kesi mbele ya mahakama hii, na mahakama hii imejiridhisha kwamba mshtakiwa alipewa haki zote wakati anachukuliwa ungamo na Inspekta Mwita na kwamba ni kweli ungamo lile ni lake na wala hakutishwa hakutishwa kama anavyodai na kwamba ungamo hilo limezingatia matakwa yote ya kisheria na kwamba pingamizi hilo la mshtakiwa la kutaka ungamo hilo lisipokelewe nalitupilia mbali na ninalipokea ungamo hilo kama utambulisho namba moja katika kesi hii”alisema Jaji Sheikh.

Wakati huo huo Jaji Sheikh amesema Machi 3 mwaka huu, atatoa uamuzi wa kujitoa au kutojitoa kusikiliza kesi hiyo.

Uamuzi huo unafuatia ombi la washatkiwa 34 ambao ni raia wa kigeni katika kesi hiyo kupitia mawakili wao ,Ijumaa iliyopita kuomba Jaji huyo ajitoe kwasababu hawana imani na yeye.

Ombi hilo la kumtaka jaji Sheikh ajitoe ulikuja saa chache baada ya jaji huyo kutoa uamuzi wa kuwanyima dhamana licha ya kifungu cha 148 (6) na (7) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, makosa yanayowakabili washtakiwa kuwa na dhamana ambapo alisema mahakama hiyo imetumia mamlaka yake kuwanyima dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi Mosi mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.