Header Ads

KIKWETE AITAKA MAHAKAMA IJISAFISHE

Na Happiness Katabazi

RAIS Jakaya Kikwete ameomba uongozi wa Mhimili wa Mahakama nchini kuondoa hisia za ukosefu wa uhadilifu zinazowakabili baadhi ya watendaji wa mahakama nchini.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana katika sherehe ya siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo maudhui ya siku ya sheria mwaka huu ni “ Umuhimu wa elimu kuhusu mahakama kama hatua ya msingi ya utatuzi wa migogoro katika jamii”.

“Leo katika kusherekea siku hii ya sheria minauomba mhimili wa mahakama mambo mawili .Mosi; uadilifu katika utoaji haki…bado kuna hisia ya ukosefu wa uhadilifu kwa watoaji haki ambao ni mahakama kwamba wenye fedha ndiyo wanapata haki na wasiyo na fedha hawapati haki:

“….Uwezo wa kuondoa hisia hizo mbaya upo mikononi mwenu na ninatambua sifa za uadilifu mlizokuwa nazo majaji na mahakimu licha miongoni mwenu wamekuwa na sifa za ukosefu wa uhadilifu na kwa taarifa nilizonazo uongozi umekuwa ukiwashughulikia kiutawala”alisema Rais Kikwete.

Aidha Rais Kikwete alisema ombi lake la pili kwa mhimili wa mahakama linahusu maboresho katika sekta ya sheria, kwamba anaomba maboresho yafanywe kwa kasi kwani kasi ya sasa ya ufanywaji wa maboresho ya sheria ni ndogo na kwamba wabia wa nchi katika sekta hiyo wameishaanza kulalamikia utendaji wa programu hiyo ya maboresho kwamba inasuasua hali inayosababisha wabia wetu kurudisha fedha ambazo awali zilitengwa kwaajili ya maboresho ya sheria na kuongeza kuwa changamoto nyingine zinazoikabili mahakama hivi sasa kwa asilimia fulani zinachangiwa na kasi hiyo ya kusuasua ya sekta ya maboresho ya sheria.

Hata hivyo Rais Kikwete aliutaka mhimili wa mahakama kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu kwa umma kuhusu tendaji kazi, na muundo wa mahakama ukoje kwani kwakufanya hivyo pia kutamuondolea adha anayoipata hivi sasa kwani baadhi ya wananchi ambao kesi zao mahakamani zimekwisha amriwa na wakashindwa katika kesi hizo ,kila kukicha wamekuwa wakifika ofisini kwake Ikulu wakimuomba atengue hukumu hizo kwakuwa yeye ni rais wa nchi na kwamba ana mamlaka ya kutengua.

“Ndiyo maana leo hii nasisitiza mahakama ione umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya habari kikamilifu kutoa elimu kwa umma kuhusu utendaji na muundo wa mahakama kwani kuna wananchi wamekuwa wakijazana pale ofisini wakitaka nitengue hukumu zilizokwishatolewa na mahakama na mimi nimekuwa nikiwaambia sina mamlaka ya kufanya hivyo… wananchi hao wamekuwa wakinijibu kama siwezi kufanya hivyo watamchagua rais anayeweza kufanya hivyo na kwamba ndiyo maana wanataka Katiba mpya…lakini yote hii inasababishwa na umma kuwa na uelewa finyu wa sheria na muundo wa mahakama.’alisema Kikwete nakusababisha watu kuangua vicheko.

Aidha kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alisema bado mahakama inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha, majengo na rasilimali watu na hivyo kumuomba rais aongezee bajeti mhimili huo.

“Mahakama itaendelea na mikakati maalum ya kuongeza kasi ya usikilizaji na umalizikaji wa kesi, tutakumbushana, tutawajibishana,tutarekebisha kanuni zenye mafumbo, tutarahisha taratibu,tutabadilisha zile za kale,tutawaelimisha zaidi na kuwasimamia mahakimu.Tutawaandika majaji wastaafu”alisema Jaji Mkuu Othman.

Awali mshereheshaji wa sherehe hiyo ambaye ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Francis Mutungi alisema sherehe hizo ni kiashiria cha kuanza kwa mwaka mpya wa mahakama na kwamba sherehe hiyo kwa mwaka huu itakuwa ni tofauti na miaka iliyopita kwani itaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na siyo Kiingereza nakwamba huko ni kukukuza lugha ya Kiswahili na hotuba zote jana ziliandika na kusomwa kwa lugha ya Kiswahili hali iliyopokelewa kwa furaha na waudhuliaji wengi ambao katika sherehe za miaka iliyopita walikuwa wakipata wakati mgumu kuelewa baadhi ya maneno ya kisheria yaliyokuwa yakisomwa kwenye hotuba za wanasheria.

Wakati huo huo katika hali isiyotarajiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Freeman Mbowe aligeuka kivutio wakati akiinuka kwenye kiti alichokaa kuelekea kwenye ngazi za mahakama kuu kwaajili ya kushiriki na viongozi mbalimbali wa serikali na mahakama kupiga picha, ambao watumishi wa mahakama, mawakili na wananchi mbalimbali walioudhulia sherehe hiyo walioanza kumshangilia kwa sauti ya juu ‘Mbowe Mbowe,Mbowe’ na kiongozi huyo kulazimika kuwapungia mkono na kutabasamu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 3 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.