Header Ads

KESI YA SAMAKI WA MAGUFULI:WASHTAKIWA WAMKATAA JAJI

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE raia 34 wa kigeni wanaokabiliwa na kesi ya uvuvi haramu kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi maarufu “Kesi ya Samaki wa Magufuli’ jana waligeuka mbogo na kumuomba Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Radhia Sheikh, ajitoe kusikiliza kesi hiyo kwa sababu hawana imani naye.

Ombi hilo liliwasilishwa na mawakili wa washtakiwa hao, John Mapinduzi na Ibrahimu Bendera, mahakamani hapo ikiwa ni saa chache baada ya jaji huyo kutoa uamuzi wa kuwanyima dhamana licha ya kifungu cha 148 (6) na (7) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, makosa yanayowakabili washtakiwa kuwa na dhamana.

Sababu ya jaji huyo kuwanyima dhamana ni kwamba mazingira ya kesi hiyo washtakiwa wakipewa dhamana wanaweza wakaruka.

“Wateja wangu wamenieleza kuwa hawana kabisa imani na wewe na wanaomba ujitoe uongozi wa mahakama umpange jaji mwingine kwa sababu wanaamini dhamana ni haki yao.

“Wateja wangu wamenieleza kwamba kilichowashtua zaidi ni kwamba mapema mwaka jana jaji wa mahakama hii, Njegafibili Mwaikugile, alishatoa masharti ya dhamana kwa wateja wangu na ambapo wateja wangu walikimbilia Mahakama ya Rufani na jopo la majaji wa rufani watatu waliokuwa wakiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Agustino Ramadhan liliamuru ombi hilo la washtakiwa la kutaka wapatiwe waliwasilishe Mahakama Kuu na mahakama hiyo isikilize ombi hilo.

“Mimi pamoja na wateja wangu tulitekeleza amri ya Mahakama ya Rufani na ndipo tukaleta upya ombi la dhamana mbele yako na Januari 17 mwaka huu, ukalisikiliza…lakini cha ajabu leo umetoa uamuzi wa kuwanyima dhamana wateja wangu wakati Jaji Mwaikugile wa mahakama hii alishatoa masharti ya dhamana …,” alidai Mapinduzi.

Alieleza kuwa sababu nyingine iliyowashangaza wateja wake na kufikia hatua ya kumkataa jaji huyo ni kwamba katika uamuzi wake huo wa maombi ya dhamana amewataja washtakiwa ni wahamiaji haramu na kwamba hawana hati za kusafiria.

Wakili Mapinduzi alidai kuwa maneno hayo ya jaji, wateja wake wamesema hayana ukweli wowote kwani kuna baadhi ya washtakiwa wana hati za kusafiria na zimegongwa mhuri wa serikali ya Tanzania na kwamba wao hawakuwa na mpango wa kuja kuishi hapa nchini isipokuwa walikuwa wakipita njia na ndipo walipokamatwa na katika Bahari ya Hindi eneo la Tanzania.

Aidha Mapinduzi alidai wateja wake wamesema katika hati ya kiapo iliyowasilishwa hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kwamba wakipewa dhamana wanaweza kuruka dhamana na kwamba kesi hiyo imechukua muda mrefu kumalizika na kwamba jaji huyo amekuwa akiichelewesha kwa makusudi.

Alisema kuchelewesha huko kwa kesi kumesababisha wateja wake kuendelea kusota rumande kwa muda mrefu tangu Machi 8, 2009.

Mapema jana asubuhi Jaji Shekhe akitoa uamuzi wake kuhusu ombi la kupatiwa dhamana washtakiwa hao ambalo liliwasilishwa mahakamani hapo na washtakiwa, alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili katika ombi hilo Januari 17 mwaka huu, alisema kwa mujibu wa sheria ya Makosa ya Jinai ,washtakiwa wana haki ya kupata dhamana ila tu kwa mazingira ya kesi hiyo mahakama hiyo imetumia mamlaka yake kuwanyima dhamana washtakiwa hao kwa sababu ilifikiria mambo yafuatayo:

Jaji Sheikhe alisema kabla ya kufikia uamuzi huo mahakama ilijiuliza kuwa washtakiwa wanakabiliwa na makosa ambayo yana adhabu kali, alisema kosa la kwanza ni la uvuvi haramu ambalo adhabu yake ni jela miaka 20 au faini ya sh bilioni tano.

Alisema kosa la pili ni uharibifu wa mazingira katika Bahari ya Hindi na endapo watapatikana na hatia watatumikia kifungo cha miaka 10 au kulipa faini ya sh bilioni tano na kosa la tatu ni kusaidia kutendeka kwa kosa ambalo kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi katika Kina kirefu cha Bahari ni miaka saba jela.

“Pia mahakama hii kabla ya kufikia kutoa uamuzi huo ilijiuliza kuwa washtakiwa wote ni wahamiaji haramu, hawana vibali vya kuishi hivyo endapo watapewa dhamana je hawawezi kuruka dhamana? Pia mahakama hii haikuona haja ya kutoa amri kwa Idara ya Uhamiaji ya hapa nchini itoe vibali kwa kuishi kwa washtakiwa hao ….kwa hiyo basi mahakama kwa kutumia mamlaka yake licha makosa yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria ila kwa mazingira ya kesi mahakama inakataa kuwapatia dhamana washtakiwa,” alisema Jaji Shekhe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi Februali 26 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.