Header Ads

11 KORTINI KWA MAUAJI YA KUANGUKA KWA GHOROFA


Na  Happiness Katabazi

HATIMAYE Mfanyabiashara Razah Hussein Razah na wenzake 10 jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wakikabiliwa na jumla ya makosa 24 ya kuua bila kukusudia.

Mbali na Razah washitakiwa wengine ni Godluck Mbaga,Wilbroad Mugabisyo,Ibrahim Kisoki,Mohamed Abdubakari,Charles Salu, Zonazea anage,Vedasto Ferand,Michael Hemed  Hemed,Albert  Jones na Joseph  Ringo ambao waliletwa jana saa  nane mchana chini ya ulinzi mkali wa wanausalama ambao walikuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Ilala(RCO), Duwani Nyanda.

Mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka mawakili waandamizi wa serikali waliokuwa wakiongozwa na Bernad Kongora, Tumaini Kweka, Lasdlaus Komanya, Peter  Mahugo, Kinyeshi waliwasomea mashitaka hayo kwa kupokezana.

Wakili Kongora alidai mashitaka yote hayo 24 yanayowakabili washitakiwa wote yanafanana na kwamba wanakabiliwa na makosa ya kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , kuwa   mnano Machi 29 mwaka huu huko katika eneo la Mtaa wa Indragand waliwaua watu 24 bila kukusudia.

Hata hivyo wakili Kongora aliwataka washitakiwa hao wajibu chochote kwakuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ni Mahakama Kuu na kwamba upepelezi bado haujakamilika na kwamba wanaomba mahakama isiwapatie dhamana kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuwapatia dhamana.
Hata hivyo mawakili wa utetezi zaidi ya saba ambao Jerome Msemwa, Adronicus Byamungu,John Mhozya waliomba mahakama hiyo iwapatie dhamana na washitakiwa wanao wadhamini wakuaminika kwasababu tayari kuna maamuzi mbalimbali yalishatolewa na mahakama ya Rufaa na mahakama Kuu katika kesi za makosa ya kujaribu kuua ,mahakama hizo zilisema mahakama za chini zina mamlaka ya kutoa dhamana kwa kesi ambazo zinafunguliwa kwanza mahakama ya chini na kisha zinakuja kuamishiwa mahakama kuu kwaajili ya usikilizwaji.

Hata hivyo mawakili wa serikali walipinga maombi hayo kwa maelezo kuwa maamuzi hayo ya mahakama rufaa yalitolewa kwenye kesi ya kujaribu kuua wakati kesi inayowakabili washitakiwa hao ni kuua bila kukusudia na kusisitiza kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na hivyo haina mamlaka ya kuwapatia dhamana.

“Mheshimiwa hakimu  sisi upande wa Jamhuri tunawasii mawakili wa washitakiwa wawe watulivu na wavumilivu kwani kesi hii ndiyo kwanza imefunguliwa leo, na upelelezi bado haujakamilika na sheria zilizotungwa na bunge zipo wazi kabisa zinasema ni Mahakama Kuu peke yake ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hii na si mahakama hii hivyo tunasisitiza kuwa mahakama hii haina mamlaka ya kutoa dhamana’alidai wakili Kongora.

Itakumbukwa kuwa Machi 29 mwaka huu, ghorofa mmoja lililokuwa linajengwa katika mtaa wa Indragand lilianguka na kusababisha watu  idadi hiyo ya watu 24 kupoteza maisha.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Aprili 4 mwaka 2013.
  

No comments:

Powered by Blogger.