Header Ads

KORTINI KWA KUUZA MAENEO YA WAZI

Na Happiness Katabazi

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), jana ilimfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu aliyekuwa  Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Steven Kongwa na mwenzake Revecotus Wachawendera, kwa makosa ya kuuza eneo la wazi lililopo eneo la  Mbezi.

Mbele ya Hakimu  Mkazi Agustina Mbando, Mwendesha Mashtaka toka Takukuru,Husein Mussa alidai washitakiwa walitenda kosa hilo kati ya Januari 2000 na Desemba 2001.

 Mussa alidai  washtakiwa hao walitenda kosa hilo wakati Kongwa alipokuwa na wadhifa wa Ofisa Mpimaji Ardhi wa Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam na Wachawendera akiwa mpimaji wa ardhi katika Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Alidai kati ya kipindi hicho waligawa bila kufuata taratibu za sheria ya mipango miji Kitalu namba 1/851 na kitalu namba 1/597 Block “L” eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya bustani.

Alilitaja kosa jingine ni la  kushindwa kutimiza wajibu wao kinyume na sheria, hivyo kama wapimaji ardhi kwa pamoja walikiuka sheria ya mipango miji kwa kugawa eneo hilo.

Hata hivyo washitakiwa hao walikana mashitaka na hakimu aliwapatia masharti ya adhamana ambayo waliyatimiza na akaairisha kesi hiyo Mei 20 mwaka huu itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com; Aprili 24 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.