Header Ads

DOSARI ZA KWAMISHA RUFAA YA DPP DHIDI YA ZOMBE




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Rufaa nchini, jana ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP)-Dk.Eliezer Feleshi dhidi ya Aliyekuwa Mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Dar es Salaam(ACP)-Abdallah Zombe na wenzake baada ya mahakama hiyo kubaini dosari katika hati ya kukata rufaa.

Rufaa hiyo Na.254/2009 inayosikilizwa na jopo la majaji watatu Edward Rutakangwa,Mbarouk Mbarouk na  Bethek aMila, ambayo jana ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa kwa siku mbili mfululizo , jaji Mbarouk kabla ya kuanza kusikiliza hoja za rufaa hiyo aliutaka upande wa mwomba rufaa(DPP), wameiweke sawa mahakama kuwa katika hati ya kukata rufaa ya ya kupinga hukumu ya mahakama kuu ya kesi ya mauji Na.26/2006 ya Zombe na wenzake inasomeka kuwa hukumu ya mahakama kuu iliyotolewa na Jaji wa mahakama ya rufaa   Salum Massati.

“Hebu mawakili wa mwomba rufaa ebu mtufafanulie hili, hati  yenu ya kukata rufaa inasema hukumu ya mahakama kuu ilitolewa na jaji wa mahakama ya rufaa (Massati)…sasa kama hukumu hii ilitolewa na jaji wa mahakama ya rufaa ebu tuwalize sasa nyie waomba rufaa, michokileta hapa mbele yetu ni ombi la mapitio, marejeo au?Maana majaji wa mahakama ya rufaa hawawezi kusikiliza rufaa inayotokana na hukumu iliyotolewa na jaji mwenzao wa mahakama ya rufaa, tunachokifanya ni kufanya marejo au mapitio;

“Jicho la mahakama limeona ni kama   hakuna rufaa mbele yake kwani  rufaa ya kesi ya jinai ni lazima iwe na hati ya kukata rufaa kwa mujibu wa Kanuni ya 68(1) cha Mahakama ya Rufaa’ nakuongeza kuwa kwa dosari hiyo mahakama inaona nikama hakuna rufaa iliyokatwa dhidi ya zombe na wenzake”alisema Jaji Mbarouk.

Jaji Rutakangwa aliwataka mawakili wanaomwakili DPP wajipe muda na wasome vizuri Ibara ya 119 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inasomeka kama ifuatavyo:
“Jaji yoyote  wa Mahahakama ya Rufani hatakuwa na mamlaka  ya kusikiliza shauri lolote katika Mahakama Kuu  au katika mahakama ya hakimu  ya ngazi yoyote.:

“Isipokuwa kwamba iwapo jaji yeyote wa mahakama kuu atateuliwa  kuwa Jaji Mahakama ya rufaa, basi hata baaa ya kuteuliwa kwake kuwa jaji wa mahakama ya rufani,jaji huyo  aweza kuendelea kufanyakazi kazi zake katika mahakama kuu mpaka amalize  kutayarisha  na kutoa hukumu  au mpaka akamilishe shughuli nyingine yoyote  inayohusika na mashauri  ambayo yalikwisha anza kuyasikiliza kabla kabla  hajateuliwa  kuwa jaji  wa mahakama rufani, na kwamba ajili hivyo itakuwa  halali kwake  kutoa hukumu  au uamuzi  mwingine wowote unaohusika kwa kutumia  kutumia au  kutaja madaraka  aliyoshika kabla  ya kutueliwa  kuwa jaji wa mahakama ya rufani,  lakini endapo hatimaye hukumu hiyo au uamuzi  mwingine utapingwa kwa njia  ya rufaa itayofikishwa mbele ya  mahakama ya rufani,basi katika hali  hiyo jaji  huyo  wa mahakama ya rufani,hatakuwa  na mamlakaya kusikiliza  rufaa hiyo:inasomeka ibara hiyo.

Alisema mawakili wa mwomba rufaa walipaswa katika hati yao ya kukata rufaa waandike jaji Jaji Masati ambaye zamani alikuwa ni jaji wa mahakama kuu na sikuandika jaji wa mahakama ya rufaa.

Akijitetea mawakili wakuu wa serikali wanaomwakilisha DPP, Vitalis Timon, Prudence Rweyongeza, Mgaya Mtaki, Alexander Mzikila, Edwin Kakoraki alikiri dosari hiyo na akaomba mahakama hiyo iwapatie ruhusa ya kwenda kufanyia marekebisho dosari hiyo chini ya Kanuni ya 4(2),(2),(b) ya Sheria ya Mahakama ya Rufaa na kwamba hata jana walikuwa wapo tayari kufanyia marekebisho hati hiyo ya kukata rufaa ambayo jicho la mahakama limeona ina dosari na kisha  jana hiyo hiyo kuirejesha upya mahakamani.

Hata hivyo mawakili wa wajibu rufaa Richard Rweyongeza, Majura Magafu, Denis Msafiri  walianza kwa kuishukuru mahakama kuwa jicho mahakama limeweza kubaini dosari hiyo na kwamba kwa dosari hiyo ni kwamba hakuna hati ya rufaa mbele ya mahakama hiyo na kwamba akaiomba mahakama ikatae kuwapa muda wa kufanyia marekebisho kwani tayari muda wa kukata rufaa umeishapita na kwamba kama wanataka kukata rufaa watalazimika kuwasilisha ombi la kuongezewa muda ambao ni siku 30 chini ya kanuni ya 68(1) ya Mahakama ya Rufaa.

‘Kwa sababu jicho la mahakama limeona dosari hiyo  sisi wajibu rufaa tunaomba mahakama iitupilie mbali rufaa hiyo kwani katika kesi za jinai kama hakuna hati ya kiapo ni wazi hakuna rufaa mahakamani iliyowasilishwa na DPP’alidai wakili Magafu.


Akijibu hoja hiyo wakili Vitalis alidai Kanuni ya 4(2),(a),(b) ya Mahakama ya Rufaa inaipa mamlaka kutoa amri ya kuwaruhusu kwenda kufanyia marekebisho hati hiyo ila wanakiri ni kweli hati yao yao waliyoitumia kukata rufaa ina mapungufu hayo.

Kwa upande wake jaji Rutakangwa alisema amezikilza hoja za pande zote mbili ni nzito na zina mvuto na kwamba jopo linaomba lipewe muda wa kwenda kuandaa uamuzi wake na kwamba uamuzi wao utakapokuwa tayari watazijulisha.  

Agosti 17  mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kihistoria ya kesi ya mauji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili Zombe na wenzake ambapo jaji Salum Massati ambaye hivi sasa ni jaji wa mahakama ya rufani aliwaachilia huru Zombe na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi hiyo kwa maelezo kuwa upande wa jamhuri ulishindwa kuleta ushahidi mzuri ambao ungewea kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana hatia.


Baada ya hukumu hiyo ya mahakama kuu, DPP hakulidhishwa na hukumu hiyo Oktoba 7 mwaka 2009 akakata rufaa Mahakama ya Rufaa ,  kupinga hukumu hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama ya rufaa,rufaa hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa jana lakini ikashindikana.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi na jana washtakiwa wote walifika mahakamani hapo.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 23 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.