Header Ads

KESI YA LWAKATARE YAPIGWA KALENDA


Na Happiness Katabazi

KESI ya tuhuma za ugaidi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph jana ilitajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.

Mbele ya Hakimu Mkazi Alocye Katemana, wakili Mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka alieleza kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba jalada la kesi hiyo limeitwa Mahakama Kuu hivyo hakimu Katemana aliarisha kesi hiyo hadi Aprili 17 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kuamuru washitakiwa warejeshwe gerezani.

Hata hivyo jana hali ilikuwa ni tofauti na siku ya kwanza kesi hiyo ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo ambapo jana wafuasi wa chama hicho hawakutokea mahakamani kama zamani na jana waliojitokeza mahakamani hapo ni ndugu wa washitakiwa hao.

Lwakatare alirudishwa katika gereza la Segerea anapoishi chini ya ulinzi mkali wa askari wa Jeshi la Magereza ambao walikuwa amefika nae mahakamani hapo kwaajili ya kuakikisha ulinzi unaimarishwa.

Wakati kesi hiyo ya msingi iliyoailishwa jana, tayari uongozi wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, imesema Aprili 15 mwaka huu, Jaji Lawrence Kaduri atasikiliza ombi la Lwakatare.

Machi 22 mwaka huu,  mawakili wanaomtetea Lwakatare,Peter Kibatara na Tundu Lissu  waliwasilisha  Mahakama Kuu Dar es Salaam, ombi namba 14 la mwaka huu, la kuomba mahakama hiyo iitije majadala ya kesi tuhuma za ugaidi zilizofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwaajili ya kuzifanyia marejeo.


Kwa mujibu wa kiapo kilichoapwa na wakili Kibatara, mawakili hao wanaomba mahakama hiyo ifanyie marejeo wa majadala ya kesi ya ugaidi Na.37/2013 iliyofunguliwa wa Machi 18 mwaka huu na Mkurugenzi wa Mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya Lwakatare na Ludovick Joseph mbele ya hakimu Emilius Mchauru  ambapo siku hiyo alisikiliza maombi  ya pande mbili.

Maombi ya mawakili wa utetezi yaliomba washitakiwa wapewe dhamana wakati mawakili wakuu wa serikali Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo waliomba mahakama isitoe dhamana kwasababu kesi makosa yanaoyoangukia katika sheria za ugaidi ya mwaka 2002 hayana dhamana.

Ambapo siku hiyo hakimu Mchauru aliairisha kesi hiyo hadi Machi 20  kwaajili ya kuja kutolea uamuzi wa maombi hayo pamoja na maombi mengine lakini  hakimu huyo alijkuta akishindwa kutoa uamuzi wake kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer  Feleshi amewasilisha  hati ya kuwafutia kesi washitakiwa hao chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwasababu hana  haja ya kuendelea kuwashitaki.

Lakini dakika chache baada ya hakimu Mchauru kuwafutia kesi hiyo, wanausalama waliwakamata tena washitakiwa hao na kisha kuwapandisha mahakamani mbele ya Hakimu mwingine Alocye Katemana na wakili wa serikali  Rweyongeza alianza kuwasomea mashitaka manne mapya katika kesi mpya iliyopewa Na.6/2013 ambayo mashitaka ni yale yale  yaliyokuwa kwenye hati ya mashitaka ya awali  iliyofutwa na DPP,ambapo Katemana aliwataka washitakiwa wasijibu chochote na akaamuru waende gerezani hadi Aprili tatu.

Kwa mujibu wa madai yao mawakili wa Lwakatare wanaomba Mahakama Kuu ipitie uamuzi wa  DPP wa kuifuta hati ya awali ya mashitaka na kisha kuwafungulia kesi upya washitakiwa hao wakati kesi hiyo ilikuwa imekuja kwaajili ya mahakama kuitolea uamuzi lakini mahakama ikashindwa kutoa uamuzi wake kwasababu DPP aliwasilisha hati ya kuifuta kesi hiyo.

Kosa la kwanza ambalo linawakabili washitakiwa wote kuwa ni la kula njama kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , na kwamba mnamo Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o  Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia  sumu kwa lengo la kumdhuru  Denis Msaki  ambaye ni Mhariri wa habari wa Gazeti la Mwananchi ambalo ni kinyume na kifungu cha 227 cha sheria hiyo.

Wakili Rweyongeza alilitaja  kosa la pili kuwa ni la kula njama  ambalo pia ni kwaajili ya washitakiwa wote  ambalo ni kinyume na kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na.21 ya mwaka 2002, ambapo washitakiwa hao walitenda kosa la ugaidi la  kutaka kumteka Msaki  kinyume na kifungu  cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Shitaka la tatu ni la washitakiwa wote ambapo wanashitakiwa kwa kosa la  kupanga kufanya makosa ya ugaidi  kinyume na kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi kwamba Desemba 28 mwaka jana,walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyaraka Msaki  kinyume na kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Shitaka la nne, Rweyongeza alidai linamkabili Lwakatare peke yake  ni aliwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi , kwamba Desemba 28 mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki nyumba hiyo ilipo Kimaraka King’ong’o  kwa makusudi  aliliruhusu  kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick  cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msaki hata hivyo walikanusha mashitaka hayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi Aprili 4 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.