MHASIBU WA OFISI YA MKEMIA MKUU WA SERIKLI KORTINI KWA WIZI
Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA Muhasibu wa Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali, Godfrey Mbuilo jana amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na makosa ya wizi wa Sh.milioni 153.8 mali ya serikali.
Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Tumaini Kweka alidai kuwa mshtakiwa anatuhumiwa kwa mashtaka manne ya wizi wa
fedha akiwa mtumishi wa Umma.
Kweka alidai kuwa Agosti 2,
2011, Mbuilo akiwa katika Ofisi za wakala wa Mkemia Mkuu wa
Serikali aliiba sh. milioni 40 zikiwa ni mali ya Serikali.
Hata hivyo alidai kuwa fedha hizo,
ziliingia katika miliki yake akiwa mtumishi wa umma.Katika shtaka la pili
mshtakiwa anatuhumiwa Septemba 5, 2011 akiwa katika ofisi hiyo hiyo
aliiba sh. milioni 45 mali ya Serikali.
Shtaka la tatu anatuhumiwa, Oktoba
5, 2011 aliiba sh. milioni 40 mali ya Serikali, ambazo aliiba akiwa mtumishi wa
umma.
Pia katika shtaka la nne Mbuilo
anatuhumiwa kati ya Januari 31 mwaka jana na Aprili 10 mwaka huo huo,
akiwa katika ofisi hizo, aliiba Dola za Kimarekani 18,000, ambazo ni takribani
sh. milioni 28.8 za Kitanzania.
Wakili huyo alidai kuwa jumla ya
fedha anazotuhumiwa Mbuilo kuiba ni sh. milioni 153.8, baada ya kumsomea
mashtaka hayo alikana kuhusika na makosa hayo.
Hata hivyo wakili huyo alidai
upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine ili
waendelee na upelelezi.
Wakili wa mshtakiwa Deinol Msemwa
alidai kuwa mashtaka anayoshtakiwa mteja wake yanadhamana, pia mashtaka hayo
hayaangukii katika kifungu namba 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa
ya Jinai ya mwaka 2002.
Pia alidai hakuna sheria yoyote
inayozuia dhamana, na mshtakiwa hajawahi kushtakiwa na kosa lolote wala
hawakuwahi kuruka dhamana yoyote, kwa hiyo anaomba dhamana kwa mteja wake.
Kweka alidai sheria namba 148 (5)
(e) cha CPA, kinaeleza wazi kuwa,mtu yoyote anayeshtakiwa kama kiasi cha fedha
kinazidi sh. milioni 10, mshtakiwa atatakiwa atoe nusu ya fedha taslimu au hati
mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hiyo.
Hata hivyo alidai nusu ya fedha ya
Mbuilo ni sh. milioni 76.9, ambazo atatakiwa atoe au awasilishe hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Mmbando alisema masharti ya dhama
mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh. milioni
100 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya sh. milioni 76.9, na
hati hiyo itatakiwa ikaguliwe kama kweli inafikia kiasi hicho.ili
Mbuilo amerudishwa rumande kwa
kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, kesi yake itatajwa Aprili 24 mwaka huu.
Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com ; Aprili 12 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment