Header Ads

ASKARI JWTZ KORTINI KWA MAUJI


 Na Happiness Katabazi

ASKARI wawili wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), kikosi cha 501 Lugalo Hospitali, na mlinzi mmoja jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wakikabiliwa na kosa mmoja la kuua kwa kukusudia.

Mbele ya Hakimu Bingi Mashabara wakili wa serikali Leonard  Challo aliwataja washitakiwa hao kuwa ni askari mwenye namba MP 95753 Noah Losidui(25)  na MT. 99170 Laphael Macha (29) na mlinzi mmoja ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach, Ravelian Paulo(40).

Wakili Challo alidai kuwa Aprili 3 mwaka huu,  huko eneo la Kawe washitakiwa walimuua kwa makusudi mtu mmoja aitwaye  Yohana Mbelewa.

Hata hivyo Hakimu Katema aliwataka washitakiwa wasijibu chochote kwasababu mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba ni mahakama kuu ndiyo yenye mmamlaka ya kuisikiliza na akaiarisha kesi hiyo hadi Aprili 29 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kuamuru washitakiwa wote wapelekwe gerezani.

Wakati huo huo, askari wa Jeshi la Magereza  mwenye Na. EXB 7947 WDR ,Briton Sikaya (23), alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Alocye Katemana kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya  zenye uzito wa gramu 20.23 aina ya Heroine zenye thamani ya Sh. 910,350 katika Gereza la Keko.

Wakili wa serikali Hellen Moshi alidai kuwa mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7 mwaka huu,  ambapo alikamatwa na askari  katika eneo hilo la gereza Keko akiwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya, lakini hata hivyo alikanusha shitaka hilo na wakili wa serikali ukadai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Hakimu Katemana alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wa wawili ambao wanatoka ofisi zinazotambuliwa na serikali na yeye mshitakiwa atasaini bondi ya Sh.milioni moja na nusu.

Lakini hata hivyo mshitakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana na hakimu Katemana akaamuru apelekwe gerezani na akaiarisha kesi hiyo hadi Aprili 26 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Aprili 13 mwaka 2013. 


No comments:

Powered by Blogger.