Header Ads

SHEIKH PONDA ANA HATIA- JAMHURI


Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi ya Sh.milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiisilamu Sheikh Ponda Issa Ponda wenzake 49 umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, iwaone wanatia kwa mujibu wa kesi inayowakabili na iwahukumu kwa mujibu wa sheria.

Upande wa jamhuri katika kesi hiyo unaowakilishwa na wakili Mwandamizi wa Serikali ,Tumaini Kweka na Jessy Peter waliwasilishwa ombi hilo kwa njia ya maandishi mahakamani hapo jana kama walivyoamriwa na hakimu mkazi Victoria Nongwa Machi 21 mwaka huu, ambpo alizitaka pande zote katika kesi hiyo jana ziwasilishe majumuisho yao ya mwisho yanayoomba mahakama iwaone washitakiwa wana hatia au la.

Wakili Kweka liliikumbusha mahakama kuwa washitwakiwa wanakabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa, kuingia kwa jinai,kujimilikisha ardhi la kiwanja cha Chang’ombe Markas kinyume na sheria, wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59, na kosa la uchochezi linalomkabili Ponda na mshitakiwa wa tano Mkadamu Swallehe.

Wakili Kweka alidai katika kuthibitisha kesi yao waliweza kuleta jumla ya mashahidi 16 ambapo shahidi wa kwanza,tatu na nne waliieleza mahakama  kuwa wao wanafanyakazi katika Baraza Kuu la Waislamu(Bakwata) ambao walieleza mahakama kuwa eneo la markas lilikuwa ni mali ya Bakwata lakini Bakwata ikaamua kubadilishana eneo hilo la kampuni ya Agritanza Ltd hivyo kampuni ya Agritanza ndiyo mmiliki halali wa eneo hilo na siyo mali ya waislamu.

“Jamhuri imeweza kuleta ushahidi madhubuti ambao  unatosha kuishawishi mahakama hii iwaonyesha washitakiwa wote wana hatia katika makosa yanayowakabili”alidai wakili Kweka.

Alidai kuwa hakuna ubishi kwamba washitakiwa wote walikamatwa eneo la tukio (markas) na Ponda wakati akitoa utetezi wake alidai kuwa wakati kuna mgogoro wa umiliki wa eneo hilo na yeye kama kiongozi wa taasisi hiyo, alitoa agizo kwa viongozi wa misikiti kuwatangazia waislamu wote kuwa kutakuwa na ujenzi wa msikiti wa muda katika eneo hilo la Markas liloibwa ili waweze kurirejesha mikononi mwa waislamu kwani washitakiwa hao wanadai eneo hilo ni mali ya waislamu.

“Kwa utetezi huo wa Ponda, sisi upande wa jamhuri tunaona kisheria kuwa makosa yote yanayowakabili washitakiwa waliyatenda kwa makusudi na walikuwa wakijua wanavunja sheria za nchi hivyo tunaiomba mahakama hii iwaone washitakiwa wote wana hatia”aliadai wakili Kweka.

Akichambua hoja ya washitakiwa iliyokuwa inadai kuwa wao wana haki ya Kikatiba inayompa uhuru mwananchi wa kwenda sehemu yoyote anayoitaka bila kubughudhiwa ,ambapo wakili Kweka alitumia maamuzi yaliyotolew na Mahakama Kuu Katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo mahakama hiyo ilisema haki ya mtu isivunje haki ya mtu mwingine.

‘Sisi tunasema washitakiwa hawa walivunja haki za watu wengine kwa kuingia kwa jinai kwenye kiwanja cha Chang’ombe Markas na hivyo basi tunaiomba mahakama hii waone washitakiwa wote wana hatia na iwahukumu kwa mujibu wa sheria.”alidai Kweka.

Hakimu Nongwa alisema atatoa hukumu ya kesi hii inayosubiriwa kwa shahuku kubwa na watu oktoba 18 mwaka huu.

Oktoba 18 mwaka huu,kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi aliwasilisha hati ya kumfungia dhamana Ponda na Mkadamu , ambapo hadi hivi sasa washitakiwa wanaishi katika gereza la Segerea.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Aprili 4 mwaka 2013.  

No comments:

Powered by Blogger.