OMBI la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred
Lwakatare, la kuiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuifuta kesi
inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana lilisikilizwa
mafichoni, hivyo kuibua malalamiko makubwa kwa wafuatiliaji.
Kesi hiyo ambayo inafualitiliwa na wananchi wengi, iliendeshwa katika
chemba ya Jaji Lawrence Kaduri, hatua iliyowafanya hata waandishi wa
habari za mahakamani kuzuiwa na askari wa Jeshi la Magereza kuingia
ndani ya chumba hicho kidogo.
Badala yake waandishi hao walilazimika kufanya juhudi za ziada
kuwashawishi askari hao ili angalau wamruhusu mmoja wao, Faustine
Kapama, aingie ndani asikilize halafu baadaye awasimulie, ombi ambalo
hatimaye lilikubaliwa, hivyo wengine zaidi ya 15 kubaki nje.
Kadhia hiyo haikuwakuta waandishi pekee, bali hata wabunge wa CHADEMA
na wafuasi wao zaidi ya 70 waliofika mahakamani hapo tangu saa moja
asubuhi kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo, walijikuta wakiishia kwenye
korido za mahakama hiyo.
“Tunajua Lwakatare ameshtakiwa na serikali. Serikali hiyo hiyo leo hii
imeamua kesi hii iendeshewe kwenye chemba ili sisi wananchi na
waandishi wa habari tusisikie na kuona yanayozungumzwa katika kesi hiyo.
“Mahakama inafahamu fika kesi hii hivi sasa imezua mjadala mkubwa
sana, kwanini huyu Jaji Kaduri hakusoma alama za nyakati na akaamua
kuipeleka katika mahakama ya wazi?” walihoji wananchi hao.
Kitendo hicho kiliwakera waandishi wa habari za mahakamani wakidai
chemba iliyotumika ni chumba kidogo, hivyo wamenyimwa fursa ya
kuisikiliza kesi hiyo na kisha kwenda kuiripoti kwa umma.
Mawakili waumana
Mvutano mkubwa wa kisheria ulijitokeza wakati mawakili wa pande zote
mbili za serikali na Lwakatare wakichambua hoja zao mbele ya Jaji
Kaduri.
Awali, upande wa Serikali ukiongozwa na mawakili Prudence Rweyongeza,
Peter Mango na Ponsian Lukosi uliweka pingamizi mbili kuwa maombi
yaliyowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa utetezi, Mabere Marando,
Peter Kibatala na Tundu Lissu, vifungu vyake vilikosewa.
Hata hivyo, upande wa utetezi nao uliweka pingamizi kuwa upande wa
serikali ulikosea vifungu walivyonukuu katika kupeleka maombi yao
Mahakama Kuu, hoja ambayo mawakili wa Serikali walilazimika kuifuta
kabla haijaanza kujadiliwa.
Pingamizi la pili lilihusu hati ya kiapo ambapo mawakili wa serikali
walihoji uhalali wake, lakini hoja za kisheria zilizojibiwa na Kibatala
zilimaliza mjadala huo, hivyo kuanza kusikiliza kesi ya msingi.
Katika kesi hiyo, upande wa utetezi ulisema kitendo alichofanya
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hakikuwa cha lazima. Kwamba licha ya
mkurugenzi huyo kuwa na mamlaka ya kufuta kesi, lakini anapofanya hivyo
lazima aoneshe amefuta kwa masilahi ya umma, kutafuta haki au pengine
kuzuia mahakama isidhalilike na hukumu ambayo ingetolewa.
Mawakili hao walisema kuwa kesi iliyofutwa na kurejeshwa tena Kisutu
ilikuwa ni matumizi mabaya ya mamlaka ya DPP, hivyo kuiomba Mahakama Kuu
kupitia upya mwenendo wa kesi namba 37/2013 iliyofunguliwa Kisutu kwani
ilifunguliwa kwa nia ya kumdhalilisha mtuhumiwa.
Walihoji iliwezekanaje kufuta kesi na kuifungua ndani ya muda mfupi, kwamba walipata wapi ushahidi mwingine mpya.
Mawakili hao wa utetezi wanaiomba Mahakama Kuu ifanye yafuatayo:
Kwanza, ipitie mwenendo wa kesi zote mbili, namba 37/2013 na 6/2013 ili kujua kama zina hoja ya msingi, halali au la.
Pili, wanaomba mahakama iamrishe kuwa mwenendo wa kesi namba 6 urudi
katika kesi namba 37, ili Mahakama ya Kisutu iweze kutoa hukumu kutokana
na mambo yaliyokuwa yanabishaniwa kisheria.
Tatu, wanaiomba Mahakama Kuu kuingilia mchakato wa ‘nole’ (hawana
hatia) iliyotolewa na DPP kwa muda mfupi kisha kumtia mtuhumiwa hatiani,
ambavyo ni kinyume kabisa cha madaraka ya DPP.
Mmoja wa mawakili hao, Lissu alisema kuwa mashtaka hayo ni ya kutunga
na hayana uhai kisheria kwa kuwa Mahakama ya Kisutu tayari ilishaanza
kuisikiliza.
Lissu aliongeza kuwa hakuna haja ya kuibebesha lawama Mahakama ya
Kisutu kwa masuala hayo bali wanasheria wa serikali walioielekeza
mahakama vibaya kwa kuingilia mchakato wake ili waweze kutekeleza azima
yao.
Alidai kuwa kesi ilikuwa ni ya jinai inayosikilizwa wazi tena bila
kificho, hivyo hakukuwa na ulazima wa mawakili wa serikali kumvizia
Lwakatare kwa kuifuta na kuifungua upya.
Awali wakili Rweyongeza alipangua hoja za mawakili wa Lwakatare ambazo
zilidai DPP alitumia madaraka yake vibaya kuifuta kesi Na. 37/2013 na
akazitaja sababu zilizosababisha aifute kesi hiyo na kufungua kesi mpya
Na. 6/2013 Machi 20 mwaka huu, kwa kuwa mashitaka ni yale yale.
Aliitaja sababu ya kwanza iliyofanya DPP aifute kesi Na. 37 /2013
iliyofunguliwa Machi 18 mwaka huu, kuwa ni uongozi wa Mahakama ya Kisutu
kukosea na kuifungua kesi hiyo katika jalada la kesi zinazoendeshwa
katika mahakama za chini (Subordinate Court) badala ya kuisajili kesi
hiyo katika rejista ya kesi zinazopaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Pili, ni kwamba hakimu aliyeisikiliza kesi hiyo, Emilius Mchauru,
alikosea kuwaruhusu washtakiwa hao kujibu mashitaka wakati Mahakama ya
Kisutu haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo ya ugaidi.
“Hivyo basi upande wa Jamhuri tunasisitiza kuwa uamuzi wa DPP wa
kuifuta kesi ile ulikuwa wa haki ambao ulikidhi matakwa ya kifungu cha
nane cha Sheria ya Uendeshaji wa Mashitaka ya mwaka 2008,” alidai
Rweyongeza.
Akipangua hoja ya mawakili wa utetezi iliyokuwa ikiiomba Mahakama Kuu
iifute kesi ya msingi inayowakabili washitakiwa hao kwa sababu kosa la
pili, tatu na nne hayaoneshi nia ya washitakiwa hao kutenda makosa ya
ugaidi, alidai kuwa hoja hizo zimeletwa wakati usio sahihi kwani kesi ya
msingi ipo katika hatua za uchunguzi, upelelezi bado haujakamilika.
Alidai kuwa huenda siku za usoni DPP akaamua kubadilisha hati ya
mashtaka kwa hiyo ombi hilo halina msingi na kwamba hata hivyo Sheria ya
Kuzuia Ugaidi inasema kitendo cha kumteka nyara mtu ni kosa la
ugaidi, kwa hiyo kinachotakiwa kuzingatiwa katika hilo ni suala la
ushahidi tu.
Kwa upande wake, Jaji Kaduri alisema amesikiliza kwa makini hoja za
mawakili wa pande zote mbili na kwamba tarehe ya kuja kutoa uamuzi wa
malumbano hayo ya kisheria itatolewa kwa njia ya maandishi.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Aprili 16 mwaka 2013.
|
No comments:
Post a Comment