Header Ads

GODBLESS LEMA AIBWAGA TENA CCM

Na Happiness Katabazi

Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ameibuka kidedea baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya marejeo ya rufaa iliyomrejesha bungeni.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na makada watatu wa CCM mkoani Arusha, kupitia kwa Mawakili wao Alute Mughway na Modest Akida wakiiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya hukumu yake hiyo kwa madai kuwa hukumu hiyo haikuwa sahihi.
Hata hivyo, jana Mahakama ya Rufani ilisikiliza maombi hayo kutoka kwa waombaji pamoja na hoja za wajibu maombi na kisha kutupilia mbali maombi hayo ikisema kuwa hayana msingi.
Uamuzi huo wa kutupilia mbali maombi hayo ulisomwa na Jaji Bernard Luanda, kwa niaba ya jopo la majaji wenzake lililokuwa likiongozwa na Engela Kileo na Salum Massati.
Hata hivyo, jopo hilo halikutoa sababu za kutupilia mbali maombi hayo na badala yake lilisema litatoa maelezo ya kina baadaye.
Majaji hao isipokuwa Kileo ndiyo waliosikiliza na kutoa hukumu ya rufaa iliyomrejesha Lema bungeni, ambayo ilikuwa inapingwa na makada hao wa CCM.
Awali, kabla ya kutupilia maombi hayo ya marejeo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya waombaji hao kutaka suala hilo lisikilizwe na jopo la majaji saba.
Wakili Mughwai aliwasilisha maombi katika Mahakama ya Rufani akiomba marejeo ya rufaa yahamishwe katika jopo la majaji watatu na kupelekwa kusikilizwa na jopo la majaji saba kwa madai kuwa kuna jambo linatakiwa kushughulikiwa kutokana na mazingira yake.

Wakili wa Lema, Methods Kimomogoro alidai kuwa Wakili Mughwai amechanganya maombi hivyo kuleta utata na kwamba kama alikuwa akitaka yasikilizwe angeyapeleka katika utaratibu ulio sahihi.

“Kanuni ya Nne ya Mahakama ya Rufaa, inasema hakuna kanuni rasmi inayowezesha jopo hili kuhamisha maombi ya marejeo kwenda kwenye jopo la majaji saba kwa ajili ya mapitio,” alisema Kimomogoro na kuongeza:“Labda kama maombi ya mapitio yangekubaliwa, wangekwenda hatua ya pili ya kuomba jopo la majaji saba.

Maombi haya hayajafuata utaratibu hivyo naomba Mahakama iyatupilie mbali kwa kuwa sababu za kisheria hazikidhi na Mahakama haina uwezo wa kuyatolea uamuzi.”

Wakili wa Serikali, Vicent Tangoh alimuunga mkono Kimomogoro na kuongeza kuwa hiyo inaonyesha hakuna maombi yoyote mbele ya Mahakama wala kitu cha kupeleka katika jopo la majaji saba.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 23 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.