Header Ads

HONGERA JESHI LA POLISI KWA KUKAMILISHA HARAKA UPELELEZI KESI YA LWAKATARE






Na Happiness Katabazi

APRILI 13 mwaka huu, kupitia mitandao yangu ya kijamii ya www.katabazihappy.blogspot.com na Facebook; happy katabazi niliweka makala yangu iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Komeni kujadili mwenendo wa kesi ya Lwakatare nje ya mahakama’.

Kwa kifupi tu ndani ya makala hiyo nilikuwa nawakemea baadhi ya wanasiasa na waandishi wa habari ambao walikuwa wakiijadili mwenendo wa kesi hiyo nje ya mahakama ambayo mawakili wakuu wa serikali Ponsia Lukosi, 
Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo wanaoiendesha kesi hiyo tangu ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza Machi 18  mwaka huu, na kisha kesi hiyo ikafutwa ikajafunguliwa Machi 20 mwaka huu na ikapewa Na.P1,7/2013,  Machi 22 mwaka huu, kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Alocye Katemana walisema wazi kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kesi hiyo ikaarishwa hadi Aprili 30 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.



Nikiri wazi kuwa baada ya kuiweka makala hiyo kwenye mitandao hiyo ilisomwa na wengi na kuwa wengine walionikosoa kwa hoja zisizo na mashiko kwani walishindwa kujikita kwenye hoja yangu iliyokuwa ikikemea makundi hayo iache tabia ya kuingiria uhuru wa mahakama na iliwasisitiza waheshimuwa mgawanyo madaraka.

Lakini kundi jingine lilinipongeza kwa makala hiyo na ninashukuru pia kwani kwa njia moja au nyingine mawazo yangu hayo yaliyokuwa yamewekwa kwenye makala hayo  ambayo yalikuwa yakikataza baadhi ya wanasiasa na waandishi wa habari kaacha kuijadili kesi hiyo nje ya bunge kwani kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama.

Wiki iliyopita Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angella Kairuki , Mbunge wa Kigoma Mjini Peter Serukamba na baadhi ya wabunge wengine wakati wakiwa bunge wakichangia hotuba ya Ofisi ya Rais, ambazo hotuba zao ziliwasilishwa bunge na waziri Steve Wassira , George Mkuchika, baadhi ya wabunge walikuwa wakichangia maoni ya bajeti hizo na wengine na walipokuwa wakitaka kuijadili kesi ya Lwakatare , Waziri Kairuki na Serukamba na Wasira walimwomba Spika wa Bunge Anna Makinda na Naibu wake Job Ndugai wawazuie wabunge wasijadili kesi ya Lwakatare kwani ipo mahakamani, na endapo bunge likiruhusu hilo ,ni wazi bunge litakuwa linaingia uhuru wa mahakaman.

Nawapomgeza viongozi hao kwani mawazo yao hayo yalishabiana na mawazo yangu hayo niliyokuwa nimeyaandika katika makala hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “KOMENI KUJADILI KESI YA LWAKATARE NJE YA MAHAKAMA’.

Na siyo siri tangu bunge likataze jambo hilo lisijadiliwe nje ya mahakama naweza kusema katazo hilo limesaidia kwa kiasi fulani kwani wale wanasiasa na waandishi wa habari ambao walifikia mbali sana kwakusema kesi hiyo ni ya kubambika ,wamepunguza kasi ya kujadili kesi hiyo na watu tunajiuliza kasi ile ya kuijadili kesi hiyo ya kaka yangu Lwakatare nje ya mahakama imeishia wapi?

Itakumbukwa kuwa Aprili 22 mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Issa Mungulu aliwaeleza waandishi wa habari kuwa upelelezi wa kesi tuhuma za ugaidi inayomkabili  Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatale na mwenzake Joseph Ludovick umekamilika na kwamba jeshi la polisi litapelekea jalada hilo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP)-Dk.Eliezer Feleshi kwaajili ya hatua za kisheria kuhusu kesi hiyo.

Tamko hilo la Kaimu DCI-Mungulu kwa niaba ya jeshi la polisi ndiyo limenisukuma kuandika makala hii ya kulipongeza jeshi la polisi kwani  limeanza kukamilisha upelelezi wake haraka hasa ukizingatia kesi hiyo iliyozua mjadala mkubwa nchini ilifunguliwa Machi  20 mwaka huu. Na Aprili 22, Jeshi la Polisi linautangazia umma kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Hakika hatua hii ni ya kupongeza kwani imedhiirisha kuwa hivi sasa jeshi la polisi limeanza kuondokana na kusuasusa kwa kukamilisha haraka upelelezi wa kesi mbalimbali.

Naweza kusema kwa kipindi cha mwaka huu, tu katika kesi ambazo zinafuatiliwa na umma kwa karibu ,upelelezi wa kesi ya Lwakatare nao umechukua muda mfupi kukamilika kwani kesi ya kwanza ambayo nimeiripoti pale katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu ambapo upelelezi ulichukua siku mbili kukamilika ni kesi ya jinai Na.125/2013, Jamhuri dhidi ya wafuasi 53 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu,Sheikh Ponda Issa Ponda  ilidumu mahakamani hapo kwa siku 32 tu tangu ilipofunguliwa rasmi Februali 18 na kutolewa hukumu Machi 21 mwaka huu.Ambapo Hakimu Sundi Fimbo aliwatia hatiani washitakiwa kwa makosa matatu ya kufanya mkusanyiko haramu, kukaidi amri ya jeshi la polisi ambapo kila kosa aliwahukumu kwenda jela mwaka mmoja,Na hivyo wafungwa hao ambao hivi sasa wanaishi Magereza tofauti nchini wanatumikia adhabu ya mwaka mmoja tu gerezani.

Kwa kuwa mimi ni mwandishi wa habari za mahakamani kwa zaidi ya miaka 14 sasa, hupenda kuzilipoti kesi nyingi tangu zinapofunguliwa hadi zinapomalizika na kesi ikishatolewa uamuzi na mahakama nimejenga utaratibu wa kuandika makala inayohusu kesi husika, hivyo hata hukumu ya kesi hiyo ya wafuasi wa Ponda baada ya kutolewa hukumu, niliandika makala  ambayo niliiweka kwenye mitandao yangu ya kijamii yaani www.katabazihappy.blogspot.com na Facebook.happy katabazi ; ambayo ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho (HONGERA OFISI YA DPP,POLE WAFUASI WA SHEIKH PONDA).

Ambapo ndani ya makala hiyo nililipongeza jeshi la polisi kwa kukamilisha haraka tena kwa kasi ya ajabu upelelezi wa kesi hiyo ya wafuasi wa Ponda, ambapo wasitakiwa walitenda makosa Februali 15 mwaka huu,na Februali 18 wakafikishw a mahakamani, na baada ya kusomewa mashitaka mawakili waandamizi wa serikali   Bernad Kongora, Bernad Kongora,Peter Ndjike,na Joseph Mahugo,walieleza upelelezi umekamilika na kesho yake Februali 19, kesi hiyo ilikuja kwaajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali na walisomewa na siku iliyofuata mashahidi wa upande wa Jamhuri ambapo shahidi wa kwanza alikuwa Mkuu wa upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam(ZDCO), Hemed Msangi alitoa ushahidi wake.

Wafuasi hao walifanya maandamano haramu Februali 15 mwaka huu, wakitaka kwenda ofisi ya DPP, ili wamshikinikize ili aweze kuindoa hati yake ya kumfungia Ponda dhamana aliyowasilisha katika mahakama ya Kisutu siku ya kwanza Ponda na wenzake walipofikishwa mahakamani Oktoba 18 mwaka jana, kwa makosa ya uchochezi na wizi wa malighafi za Sh.milioni 59 .

Wakati kesi ya Ponda na wenzake 49 inakuja kutolewa hukumu Mei 9 mwaka huu. 

Kwa wasomi wa sheria tunafahamu faida ya upelelezi kukamilika kwa haraka kwani upelelezi wa kesi unapokamilika kwa haraka ,unaisadia pia kesi iliyopo mahakama kutochukua muda mrefu kumalizika na mshitakiwa kujua mapema hatima yake.

Kwani hakuna ubushi kuna kesi zinachukua zaidi ya mwaka mmoja upelelezi kukamilika na matokeo yake washitakiwa ambao wanakabiliwa na kesi zisizo dhamana kusota gerezani muda mrefu.

Na kwa mujibu wa makosa ya kesi inayomkabili Lwakatare, makosa hayo hayana dhamana hivyo Lwakatare tangu alipofunguliwa kesi anaishi katika Gereza la Segerea akisubiri hatima ya kesi yake. 

Hivyo basi kitendo cha jeshi la polisi kuutangazia umma kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika ni wazi sasa umefanya kesi hiyo kupiga hatua nyingine ya kisheria. Kwani kesi hiyo ambayo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza, mawakili wa serikali siku wakifika mahakamani na kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri umekamilika, hatua nyingine ya kisheria inayofuata ni kwa mujibu wa tarehe itakayopangwa na mahakama ni kwamba  upande wa jamhuri kuwasomea washitakiwa hao maelezo ya kina ya kesi hiyo inayowakabili (Committal Proceeding) .

Baada ya ya zoezi hilo la kuwasomea (Committal Proceeding) , mahakama itatangaza kuifunga kesi hiyo katika mahakama hiyo ya hakimu mkazi na kisha jadala la kesi hiyo litaamishiwa Mahakama Kuu kwaajili ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa rasmi,ambapo siku ya kwanza washitakiwa hao watasomea mashitaka yao na kisha wataruhusiwa kujibu (Plea).

Na hatua nyingine za kuletwa kwa mashahidi zitaendelea.Hadi hapo shauri hilo litapofikia tamati kwa mahakama kutoa maamuzi yake au DPP  akiona hana haja ya kuendelea na kesi hiyo anaweza kuifuta kesi hiyo chini kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.
Kwani fursa hiyo ya kujibu mashitaka hayo walinyimwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi,kwani mahakama ya hakimu mkazi haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kwa tamko hilo la jeshi la polisi kuwa upelelezi umekamilika ni wazi linaweza kuwa funzo pia kwa wale wote wakiwemo baadhi ya wanahabari wenzangu  waliokuwa waikijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama  kwa kuandika makala na habari zenye mawazo ya kijinga ambayo hayana msingi wowote wa kisheria na yaliyokuwa na lengo la kutaka kuiondoa kesi hiyo ambayo imefunguliwa kwa mujibu wa Sheria za nchi ianze kujadiliwa nje na watu ambao hawana mamlaka ya Kimahakama.

Ni rai yangu kwa wale waandishi wote ambao walikuwa wakiandika makala zao kujadili kesi hiyo na wengine kufikia hatua ya kusema kesi hiyo ni ya kubambika, na wakati wakiandika kuwa kesi hiyo ni ya kubambika utafikiri walikuwa na ushahidi na hilo kumbe hawana , kama ni kweli wanampenda kaka yangu Lwakatare na siyo wanafki na walikuwa na lengo la kuipotisha kesi hiyo , basi wakusanye vielezo vyao vya kuonyesha kesi hiyo ni ya kubambika ili siku kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa waje wawe mashahidi wa upande wa washitakiwa na waonyeshe vielelezo hivyo, maana kuzungumza jambo hilo kuwa mshitakiwa fulani amebambikiwa kesi wakati hufanyi jitihada zozote za kufika mahakamani siku ya kesi na kutoa vielelezo, hakutamsaidia mhusika na jamii itakuhesabu kuwa wewe ni mbumbumbu na mnfaki.

Napenda kuwaasa  baadhi ya  wanahabari wenzangu kuwa  tujenge utaratibu wa kuheshimu mgawanyo madaraka, majukumu ya wanataaluma wenye taaluma zingine na kwamba tusikubali kugeuzwa kuwa ‘Microphone Political Party’.  Tusimame kwenye maadili ya taaluma yetu kwaajili ya maslahi ya taifa letu.
Kwani hata nchi nyingi zilizoendelea ,waandishi wa nchi hizo walichangia mchango mkubwa wa taaluma yao katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Waandishi wa habari katika nchi hizo zilizoendelea ,baadhi yao wameamua kubobea katika eneo fulani la kuripoti habari fulani.Mfano mwandishi wa habari anayeandika habari za Kitabibu au mazingira, basi mwandishi huyo anakuwa amesomea pia fani za Kitabibu na mazingira, lakini hapa kwetu hali ni tofauti na ndiyo maana kila kukicha baadhi ya waandishi wamekuwa wakiripoti habari zilizopotoshwa.

Wakati ni huu, tuache majungu, kutumiwa na wanasiasa uchwara tena kwa bei rahisi tu na wazi wazi kwa kutupangia tuandike habari hii kwa maslahi yao vyama vyao,majimbo au nyadhifa zao,tujiendeleze kielimu na  tubobee katika kuandika habari ambazo moyo na akili zetu  zinakutuma ujikite huko kwa nia njema.Naamini tufanya hivyo tutakuwa tunalisaidia taifa letu na mungu atalipa dhawabu.

Mwisho nirudie kwa kulipongeza jeshi la polisi kwa kukamilisha upelelezi wa kesi ya Lwakatare haraka, na pia nilitie moyo jeshi la polisi kwa kuendelea kukamilisha upelelezi katika kesi nyingine haraka zinazowakabili washitakiwa wengine wenye kesi mbalimbali kwani nimekuwa nikishuhudia kwa macho yangu ninapokuwa mahakamani naripoti kesi mbalimbali, washitakiwa na mawakili kesi zao zimekuwa zikiarishwa kwa zaidi ya hata mwaka mmoja kwa kile kinachodaiwa na upande wa jamhuri kuwa jeshi la polisi bado halijakamilisha upelelezi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com
 Facebook; happy katabazi ; Jumatano ,Aprili 24 mwaka 2013.



No comments:

Powered by Blogger.