Header Ads

MWANZO,MWISHO KESI YA SHEIKH PONDA HUU HAPA




*HUKUMU YA PONDA NI LEO APRILI 18

Na Happiness Katabazi

FUATANA na mwandishi wa makala haya   Happiness Katabazi ambaye ni mwandishi wa habari za mahakamani hapa nchini, ili uweze kufahamu kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 48, ilipofunguliwa hadi  kesho (Aprili 18) inapofikia hatua ya mwisho kutolewa hukumu.

Mimi na miongoni mwa waandishi wenzangu wa chache ambao mungu alitujalia uzima na afya njema ambapo tuliweza kuifuatilia kesi hii tangu ilipofunguliwa rasmi mahakamani hapo Oktoba 18 mwaka jana hadi kesho inapomalizika ,tuliweza kujifunza mambo mengi  ambayo yametupa faida sisi binafsi ikiwemo faida ya kufahamu vyema jinsi ya aina ya kesi hii iliyohusisha washitakiwa wengi ilivyoweza kuendeshwa na mawakili wa serikali na utetezi na hakimu na wana usalama pia.

Kwani kesi hii ya Ponda tangu ilipofunguliwa hadi kesho inatolewa hukumu, imekuwa ikiendeshwa chini ya ulinzi mkali unaoratibiwa na wana usalama toka vyombo vya ulinzi na usalama kwa njia zinaonekana na sizoonekana kwa urahisi.

Tunawashukuru wana usalama wote walioendesha ulinzi siku ya kesi hii kwani walituwezesha hata sisi waandishi wa habari za mahakamani kufanyakazi yetu kwa amani na uhuru licha hapo mwanzo tulikuwa tukipokea vitisho kutoka kwa baadhi ya washitakiwa.

Aprili 18 mwaka huu; Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu, Victoria Nongwa ,anatarajiwa kuketi katika kiti cha enzi na kutoa hukumu ya kesi hiyo Na.245/2012 inayomkabili Ponda na wenzake.

Aprili 3 mwaka huu:Mawakili wa upande wa Jamhuri ,Tumaini Kweka na Jessy Peter na mawakili wa utetezi Juma Nassor na Njama waliwasilisha majumuisho yao mahakamani hapo kwa njia ya maandishi ambapo mawakili wa upande wa jamhuri waliiomba mahakama iwaone washitakiwa wote wana hatia na wapewe adhabu kwa mujibu wa sheria.

Wakati mawakili wa utetezi waliiomba mahakama iwaone washitakiwa hawana hatia na iwaachilie huru kwa sababu hawakutenda  makosa yanayowakabili na kwamba upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yao.

Machi 21 mwaka huu;Sheik Ponda, mshitakiwa wa tano Mukadamu Swaleh walijitetea.Na washitakiwa wenzake wa nne nao walijitetea siku hiyo na hivyo kufanya jumla ya washitakiwa 48 wa kesi hiyo kumaliza kutoa utetezi wao.Na siku hii ndipo upande wa utetezi walifunga utetezi wao.

Machi 4 mwaka huu:  Hakimu Nongwa atoa uamuzi wake ambapo aliwaona washitakiwa wote wana kesi ya kujibu na akatupilia mbali hoja ya mawakili wa utetezi iliyokuwa ikidai kesi hiyo ni ya madai na kwamba ifutwe.

Machi 6 mwaka huu:Washitakiwa kesi ya sheikh Ponda waanza kujitetea mfululizo.Ambapo siku hiyu jumla ya washitakiwa saba walijitetea.

Machi 7 mwaka huu: Jumla ya washitakiwa saba walijitetea.

Machi 11 mwaka huu:Jumla ya washitakiwa saba walijitetea.Hivyo hadi kufikia siku hiyo jumla ya washitakiwa saba walikuwa wameishajitetea.

Machi 12 mwaka huu: Washitakiwa watatu tu ndiyo walitoa utetezi siku hiyo na kufanya jumla ya washitakiwa waliotoa utetezi wao kufikia 27.

Februali 18 mwaka huu: Mawakili wa pande zote mbili wawasilisha kwa njia ya mdomo.Wakili wa upande wa Jamhuri Tumaini Kweka awasilisha aiomba mahakama iwaone washitakiwa wote wana kesi ya kujibu kwasababu upande wa jamhuri umeweza kuithibitisha kesi yake.

Na mawakili wa utetezi nao waliomba mahakama iwaone washitakiwa hawana kesi ya kujibu kwasababu jamhuri imeshindwa kuthibitisha kesi yao na kwamba kesi hiyo ni ya madai ambayo inahusisha mgogoro wa ardhi hivyo ifutwe.

Februali 25 mwaka huu: upande wa jamhuri uliifunga kesi yake baada ya mashahidi  wake wa tatu kumaliza kutoa ushahidi wao.Ambao ni shahidi wa 17,  D/C F8586 Ismail wa kituo cha Polisi Chang’ombe, shahidi wa 15 ambaye ni F3929 D/C ,Constebo Eliaeli (35) ,shahidi wa 16 ambaye ni Stationi Sajenti  Amos wa kituo cha Polisi Kati . Hivyo kufanya upande wa jamhuri kuwa umeleta jumla ya mashahidi 17 na wakatoa ushahidi na ulileta jumla ya vielelezo 13.

Februali 22 mwaka huu: shahidi 12,13 wa upande wa jamhuri watoa ushahidi wao. Shahidi wa  13, Koplo Masiku ambaye ni Askari kituo cha polisi Chang’ombe ,shahidi wa 14 wa upande wa Jamhuri D/C Koplo Zakayo.

Februali 21 mwaka huu; Shahidi wa 12 ambaye ni Mkuu wa  upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kipolisi Temeke(RCO), Ame Anange Anoqie alitoa ushahidi wake ambapo alisisitiza kuwa  Ponda na wenzake  siyo wamiliki halali wa kiwanja cha Chang’mbe Markas na kwamba waliingia kwa jinai katika kiwanja hicho.

Februali 20 mwaka huu: Shahidi wa 11 wa upande wa jamhuri amabye ni Mpelelezi Mkuu wa kesi hiyo, Inspekta Thobias Walelo (34), ambaye alitoa vielelezo vilivyopokelewa na mahakama kama kielelezo cha nane  ambapo ni mapanga, Jambia, mabango,vipaza sauti,masufulia ,majenereta  alieleza kuwa baada ya kuwakamata washitakiwa hao wakiwa na majambia, visu, vipaza sauti, viloba viwili vya unga wa sembe, mikeka,mabango, visu,sufulia ,ndoo za plastiki.

Walelo alidai kuwa yeye akiwa ni mpelelezi mkuu wa kesi hiyo yeye na askari wenzake walioenda kuwakamata washitakiwa hao   waliamua kuwabeba washtakiwa hao kwenye magari ya polisi kwa awamu mbili na kisha kuwapeleka katika kituo cha polisi Kijitonyama ambapo waliwafikisha saa 12 asubuhi na kuanza kuwahoji ambapo waliwahoji hadi Oktoba 18 mwaka jana , washitakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi.

Februali 19 mwaka huu: Mahakama ya imetupilia mbali pingamizi la mawakili wa upande wa utetezi lilokuwa linataka mahakama hiyo isipokee  kama kielelezo maelezo ya ungamo yaliyotolewa na mshitakiwa  wa tano katika kesi hiyo Mkadamu Swaleh Abdallah,polisi  kama kielelezo.Uamuzi huo ulitokana baada ya kufanyika kesi ndogo(Trial within a Trial),baada ya mawakili wa utetezi kutaka maelezo ya onyo ya Mukadamu yasipokelewe kama kielelezo kwasababu maelezo hayo si yake.

Februali 18: Shahidi wa  nane, D/c-Sajenti Mkombozi Mhando   alidai kuwa  Novemba 11 mwaka jana, alikuwa Kituo Kikuu cha Polisi Kati akiwa na timu ya wapelelezi wenzake toka Temeke yeye alipewa jukumu la kumhoji mshitakiwa wa tano, Mukadam abdallah Swaleh ambapo alimpa haki zake zote.

Na kuanzia leo hadi leo hukumu inamalizika ulinzi ulikuwa ni waina yake wakati kesi ilipokuja ikija mahakamani kwaajili ya kutajwa na kusikilizwa.Ulinzi wa kesi hii ulikuwa ni waina yake ukilinganisha na ulinzi unaotolewa wakati wa kesi nyingine kwani kesi hii wana usalama uweka vifaa maalum katika ofisi za mapokezi  ya mahakama kwaajili ya kuwakagua watu wanaoingia.

Februali 28 mwaka huu;shahidi wa sita ambaye ni fundi  mwashi Hamis Salum Mkangama(30), Shahidi wa saba,  William Milanzi(43) wa upande wa jamhuri walitoa ushahidi wao.
Januari 17 mwaka huu:  shahidi wa nne   Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la (BAKWATA),Masoud Ikome(72),  amedai kuwa kiwanja kilichopo Chang’ombe Markas  ni mali halali ya kampuni ya Agritanza Ltd na siyo mali waislamu(Bakwata).

Shahidi  wa tano ambaye ni miongoni mwa Wakurugenzi wa Kampuni ya Agritanza Ltd, Afidhi Seif  Othman (42),  aliambia mahakama kampuni yake ya Agritanza Ltd ilibadilisha eneo la Chang’ombe na Bakwata na kwamba yeye ndiye alikuwa mmiliki wa eneo la Kisarawe na ndiye aliyeipatia Bakwata eneo hilo na Bakwata ikawapatia eneo la Chang’ombe na kwamba mabadilishano hayo yalifanyika Oktoba 10 mwaka 2010.

Desemba 18 mwaka 2012: Ponda anaishi gereza la Segerea,alishindwa kuletwa mahakamani hapo ambapo kesi yake ilikuja kwaajili ya kutajwa kwasababu wakili Kweka alidai amepokea taarifa toka kwa maofisa wa jeshi la Magereza kuwa Ponda ni mgonjwa.
Novemba 29 mwaka 2012: Shahidi wa kwanza  Katibu Mkuu wa Bakwata, Suleman Said Lolila(61),amekanusha madai yaliyotolewa na Sheikh  Ponda na wenzake kuwa Bakwata siyo chombo cha kuwakilisha waislamu wote hapa nchini.Na siku hii ndiyo ilikuwa ni siku ya kwanza mashahidi wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wake.

Novemba 15 mwaka 2012: Wakili  wa upande wa Jamhuri Tumaini Kweka  aliwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ambapo alidai Bakwata ni chombo ambacho kinawawakilisha waislamu wote, lakini Ponda na wenzake walikanusha madai yao na kusema kuwa Bakwata haipo kwaajili ya kuwawakilisha waislamu wote.

Novemba 8 mwaka 2012: Mukadamu Swalehe aunganishwa kwenye kesi hii Na.245/2012 inayomkabili Ponda na wenzake na hivyo kufanya sasa jumla washitakiwa kuwa ni 51.Na Mukadamu amekuwa ni mshitakiwa wa tano.

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Elezer Feleshi aliwasilisha mahakamani hapo hati ya kumfungua dhamana Mukadamu kwaajili ya maslahi ya taifa chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Kwa upande wake hakimu Nongwa alisema makosa yanayomkabili mshtakiwa huyo yana dhamana ila kwakuw DPP-Feleshi amewasilisha hati ya kumfungia dhamana, mahakama imefungwa mikono,haiwezi kutoa dhamana kwasababu sheria iliyotumiwa na DPP kumfungia dhamana mshtakiwa huyo na Ponda zimetungwa na Bunge, mahakama yenye ipo kwaajili ya kuzifuata sheria hizo zilizotungwa na bunge katika kutoa uamuzi hivyo akaamuru mshitakiwa huyo amepelekwe gerezani.

Pia siku hiyo hakimu Nongwa aliwapatia dhamana washitakiwa wote dhamana isipokuwa Ponda na Mukadamu kwasababu DPP alikuwa amewasilisha hati ya kufunga dhamana ya washitakiwa hao wawili.

Na hadi kesi hii inamalizika kesho,washitakiwa hao wawili bado wanaendelea kuishi katika gereza la Segerea kwasababu dhamana yao imefungwa na DPP tangu siku ya kwanza walipofikishwa mahakamani hapo.

Oktoba 18 mwaka 2012: Ponda na wenzake walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga, ambapo wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka  alidai  shitaka la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2012,kwamba Oktoba 12 mwaka huu, huko eneo la Chang’ombe Markasi washitakiwa wote walikula  kwa nia ya kutenda kosa hilo.

Shitaka la pili wakili Kweka alidai linawakabili washitakiwa wote ambalo ni la kuingia kwa nguvu  kwa nia ya kutenda kosa  kinyume na kiufungu cha 85 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu  na kwamba  Oktoba 12 mwaka huu,  huko Chang’ombe  Markasi , kwa jinai  wasipokuwa na sababu  za msingi  washitakiwa hao waliingia  kwenye kiwanja kinachomilikiwa kampuni ya AgriTanzania  Ltd  kwania ya kujimilikisha  kiwanja hicho isivyo halali.

Kabla ya washitakiwa hakubali au kataa shitala hilo Ponda aliripoka na kusema yeye anakanusha shitaka hilo na kwamba washitakiwa wenzake nao wanalikanusha shitaka hilo,jambo ambalo lilikataliwa na Hakimu Sanga ambaye alimrisha kila mshitakiwa ajibu shitaka hilo kwa kinywa chake ambapo kila mshitakiwa kwa kinywa chake alikanusha shitaka hilo kinyume na alivyokuwa anataka Ponda iwe kwa yeye kukanusha shitaka hilo kwa niaba ya wenzake.

Wakili Kweka alilitaja shitaka la tatu kuwa ni  kujimilikisha  kiwanja kwa jinai kinyume na kifungu cha 86 na 35 cha sheria hiyo  na kwamba kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu huko Chang’ambe  Markasi  pasipo na uhalali wowote washitakiwa wote  katika hali  iliyokuwa ikipelekea  uvunjifu wa amani  walijimilikisha  kwa nguvu ardhi  ya  kampuni ya Agritanza Ltd.

Shitaka la nne, wakili Kweka alidai ni la wizi  ambalo ni kinyume na kifungu cha 258  cha sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, na kuwa kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu,  washitakiwa hao waliiba vifaa na malighafi,matofali 1500,nondo,Tani 36 za Kokoto vitu vyote hivyo vikiwa na thamani ya Sh 59,650,000 mali ya kampuni ya Agritanza Ltd.

Aidha shitaka la tano Kweka alidai ni la uchochezi ambalo linamkabili Sheikh Ponda peke yake  ambalo ni kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha sheria hiyo  kwamba kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu katika eneo hilo la Chang’ombe Markasi  kwa maelezo kuwa yeye ni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu(T) aliwashawishi  wafuasi wake ambao ni washitakiwa hao  kutenda makosa hayo  na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

“Mheshimiwa hakimu pamoja na kuwasomea mashitaka hayo ambayo yanadhamana kwa mujibu wa sheria, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Elizer Feleshi kwa mkono wake amenituma kuwasilisha kwaniaba yake mahakamani hapo hati ya kufunga dhamana kwa mshitakiwa wa kwanza (Ponda) peke yake chini ya kifungu cha  148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2012’alidai wakili Kweka.

Kwa upande wake wakili wa shitakiwa hao Mansoor alidai anashangazwa na DPP-Dk.Feleshi kuwawasilisha hati hiyo ya kumfungia Ponda dhamana wakati dhamana ni haki ya Kikatiba na kwamba hati hiyo ya DPP imetaja sababu mbili ambazo ni mosi kwaajili ya usalama na sababu ya pili ni maslahi ya jamhuri.Nakuongeza kuwa sababu hizo hazijafafanuliwa kwa mabana na kudai kuwa washitakiwa wameishakaa kwa muda mrefu rumande na kwamba mshitakiwa wanne ni mwanamke mwenye umri wa 100 hivyo anaomba wapatiwe dhamana.

Akijibu hoja hizo wakili wa serikali Kweka alidai anashangazwa na hoja za wakili washitakiwa za kuikosoa hati hiyo iliyowasilishwa na DPP kwasababu kifungu cha 184(4) cha Sheria Makosa ya Jinai, kinasomeka wazi kuwa hati hiyo ya DPP  hata mahakama haiwezi kuipinga na kwamba inapowasilishwa mahakamani hati hiyo mahakama inakuwa imefungwa mikono  na kwamba mwenye mamlaka ya kuiondoa makamani hapo ni DPP mwenyewe siku atapoona inafahaa kuiondoa na sivinginevyo.

Hata hivyo hakimu Sanga alisema hivi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili; “Kama nilivyokwisha sema tangu awali naingia kuanza kusikiliza kesi hii kuwa mimi siyo hakimu niliyepangwa kusikiliza kesi hii ,aliyepangwa kusikiliza kesi hii ni Hakimu Victoria Nongwa ambaye yupo kwenye semina  kwahiyo endapo pande zote mbili katika kesi hii mnataka kuwasilisha hoja zenu msubirini Hakimu Nongwa akimaliza semina yake mje muwasilishe hoja hizo mbele yake”alisema Hakimu Sanga.

Hata hivyo wakili washitakiwa Mansoor alionekana kutoridhishwa na jibu hilo aliinuka na kumuomba hakimu Sanga aiarishe kesi hiyo hadi leo ili washitakiwa 49 waletwe leo kwaajili ya kupatiwa dhamana kwasababu makosa yao yanadhamana lakini hakimu Sanga alisema haitawezekana kwasababu Hakimu Nongwa bado yupo kwenye semina na leo hatakuwepo mahakamani hapo na hivyo akaamuru washitakiwa hao warejeshwe rumande hadi Novemba mosi,kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Baada ya  kesi hiyo kumaliza wanausalama walikuwa wamejazana kwa mtindo tofauti ndani ya ukumbi huo wa mahakama waliwataka waandishi wa habari na watu wengine watoke nje na ndani wabaki washitakiwa peke yake na wanausalama na kisha wakatolea mlango wa nyuma washitakiwa hao na kisha kwenye kuwapakiza kwenye mabasi ya Jeshi la Magereza, Karandika na Defenda tayari kwaajili ya kuanza safari ya kupeleka gerezani  ambapo magari ya askari wa usalama Barabarani walilazimika kuifunga barabara iliyopakana na mahakama hiyo kwa muda kwaajili ya kuruhusu msafara wa zaidi ya magari saba yaliyokuwa yamebeba washitakiwa hao,wanausalama kuelekea gerezani.

Baadhi ya watu waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo ,walizungumza na gazeti hili walisema wamefurahishwa na hatua ya serikali ya kuwafikisha washitakiwa hao mahakamani kwani Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa Sheria na Katiba ya nchi na siyo sheria za dini ya Kiisilamu.


Facebook:happy katabazi :Aprili 18 mwaka 2013. 

Simu.0716 -774494.
 

No comments:

Powered by Blogger.